Pages

Pages

Monday, June 10, 2013

Maisha ya mjasiriamali baada ya kustaafu ujasiriamali


Na, Albert Sanga, Iringa
Wiki iliyopita nilifika katika moja ya mifuko ya pesheni ili kujiandikisha kwa ajili ya utaratibu wa kujiwekea akiba kwa mpango wa kuchangia kwa hiari. Baada ya kutoka katika ofisi za mfuko huo wa pesheni nikiwa na fomu na makabrasha mengi nikakutana na mtu mmoja ambaye maongezi kati yangu na yeye ndiyo yaliyonipelekea kuandika makala hii.
Mjasiriamali Albert Sanga, pichani.....
Rafiki yangu huyu ambaye ni mfanyakazi alipigwa na bumbuwazi sana kuona ninaeleza habari za mfuko wa jamii. Swali lake kubwa lilikuwa ni hili, “Je, mifuko ya hifadhi ya jamii inahusika na wajasiriamali?” Haraka haraka nikabaini tatizo lake ya kuwa anafahamu kuwa mifuko ya kijamii ni kwa ajili ya wafanyakazi walioajiriwa ama na serikali au na mashirika na makampuni makubwa pekee.

Kutoka na maarifa na ufahamu nilionao kuhusu mifuko hii ya hifadhi ya jamii; nilipata wasaa mzuri sana wa kumuelekeza rafiki yangu huyu kwa kina kuhusu mifuko ya hifadhi ya kijamii na namna inavyowagusa watanzania wote bila kujali ikiwa wapo serikalini, kwenye sekta binafsi ama katika sekta isiyo rasmi.

Wajasiriamali ni sehemu ya nguvu kazi ya jamii. Kile kinachowapata wale walioajiriwa kwa maana ya kuchoka kiumri na kiafya, kutakiwa kupumzika baada ya miaka mingi ya kazi pamoja na maandalizi ya maisha ya baadae; vivyo hivyo kinawahusu pia wajasiriamali.

Ndio maana baada ya kumaliza mazungumzo na rafiki yangu huyu nikabaini kuwa ipo haja nishirikishane na wajasiriamali wenzangu dhana nzima kuhusu umuhimu wa mifuko ya hifadhi ya jamii na umuhimu wa mjasiriamali kujiandaa kustaafu katika ujasiriamali.

Ni vema tukafahamu kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ina histoia ndefu nchini Tanzania. Awali kulikuwepo na mifuko isiyo rasmi ya hifadhi ya Jamii (Informal safety nets) ambayo ilikuwa ni vijana kusaidia wazee ama ukoo kusaidiana.

Kuanzia mwaka 1942, wakoloni wakaja na utaratibu rasmi ambapo GEPF ilikuwa ya kwanza ikifuatiwa na NPF (NSSF), 1964, PPF-1978, PSPF-1999 kwa kutumia shera ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 1954. Sheria hizo za mifuko zilikuwa na utaratibu wa kisekta.

Lakini mwaka 2008 kuliundwa mamlaka ya udhibiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii ambapo utaratibu wa kuchangia kwa hiari ulianzishwa. Hata hivyo sheria hii ilitanguliwa na sera ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2003.

Lengo la sera hii lilikuwa ni kuweka mazingira mazuri ya taratibu mbalimbali za hifadhi za jamii, kuruhusu mwanachama kuhama kutoa mfuko mmoja kwenda mwingine na stahili zake pamoja na kuanzisha mifumo ya uchangiaji wa ziada kwa hiari.

Ni kutokana na sheria na taratibu zilizoboreshwa ndipo kumekuwepo na fursa ya Mpango wa uchangiaji wa Hiari ambapo watu mbalimbali kutoka serikalini, kutoka sekta binafsi na kutoka katika sekta isiyo rasmi wanapata fursa ya kuwa wanachama katika mifuko hii ya kijamii.

Hivyo utabaini kuwa mjasiriamali yeyote anayo nafasi ya kujiunga na mfuko wa Hifadhi ya jamii na kuanza kujiwekea akiba. Ni muhimu sana wajasiriamali kutafakari kwa kina maisha ya baadae badala ya kujisemea “Atajua Mungu”. Maisha ya sasa na baadae kwa mjasiriamali yamo katika maamuzi ya mjasiriamali mwenyewe. Unachoamua leo ndicho utakachopata kesho.

Nimekuwa nikieleza mara kwa mara katika chambuzi zangu kupitia safu hii; kuhusu athari za mabadiliko ya kibiashara kwa wajasiriamali. Nimepata kueleza kuwa biashara za sasa zinahitaji akili nyingi, ubunifu mwingi na kuona mbali kwa tofauti sana.

Hii ina maana kuwa wewe mjasiriamali upende ama usipende kuna wakati biashara zinaweza kukoma. Kukoma huku kuna namna mbili. Mosi ni kukoma mwendo wa kibiashara kutokana na mabadiliko ya kimzunguko. Hapa ni pale unapojikuta biashara iliyokupa faida jana leo imegoma na haina faida tena.

Pili: ni kukoma kwa biashara kwa maana ya wewe mjasiriamali kuishiwa uwezo wa kuendelea na biashara. Kuna wakati utafiki umri utakuwa umeenda sana, afya inaweza kuwa matatani au akili yako mjasiriamali kuchoka kabisa; kiasi kwamba hakuna namna isipokuwa kuachana na biashara.

Jawabu kwa kukoma kwa namba mosi ni wewe mjasiriamali kubadilisha biashara ama kuingiza mbinu mpya katika hiyo biashara iliyokoma. Jawabu la kukoma kwa pili ni wewe mjasiriamali kustaafu. Hapa kwenye kustaafu ndipo ambapo wajasirimali wengi hawajui. Kimsingi kama ilivyo kwa watu walioajiriwa, ndivyo ilivyo kwa mjasiriamali ya kuwa kuna wakati utafika na utalazimika kustaafu katika ujasiriamali.

Wakati wafanyakazi hupangiwa muda wa kustaafu, mjasiriamali unatakiwa ujipangie muda wa kustaafu. Kwa mfanyakazi;  tafsiri ya kustaafu ni pale ambapo taifa linaona kuwa mtu amelitumikia vya kutosha hivyo yafaa apumzike.

Kwa upande wa wale wafanyakazi walioajiriwa na serikali ama mashirika, inapofika wakati wa kustaafu walau mwajiri na serikali wanakuwa wamejiridhisha kuwa huyu mstaafu anayoakiba itakayomtosha kuishi katika maisha yake yaliyobaki hadi kufa. Akiba hii ndio kile kinachoitwa mafao na pensheni.

Niseme tu kuwa nafahamu changamoto inayowakumba wataafu wengi kuhusu pesheni ndogo wanayoendelea kulipwa kila mwezi baada ya kustaafu; lakini lengo na mpango wa mtu kustaafu kwa sheria za ajira za nchini ni kumsaidia kuishi maisha mazuri hata baada ya kustaafu kwake.

Kwa kuwa nia yangu ni kusemezana na wajasiriamali juu ya hatma yao ya kustaafu; naomba niachane na hayo ya walioajiriwa bali nijikite kwa wajasiriamali wenzangu. Kama nilivyosema pale juu ni kuwa katika ujasiriamali kuna kustaafu na kama hutaki kustaafu kwa hiyari biashara zitakustaafisha kwa lazima.

Swali hapa linalokuja ni hili, Je, mjasiriamali utaishije ukistaafu? Nimesema kuwa umri wa kustaafu kwa mjasiriamali anajiamulia mjasiriamali mwenyewe. Unaweza kustaafu ukiwa na miaka 30, 45, 50, 60, 70 au katika umri wowote ule utakaojiamulia wewe mwenyewe.

Kama mjasiriamali ukiamua kustaafu ukiwa na miaka 30 na tuchukulie umri wa kuishi wa mtanzania ni miaka 60+ (nimetumia kigezo cha ustaafu wa serikalini); ina maana kuwa utakuwa umebakiza miaka 30 mbeleni. Je, katika miaka 30 ijayo utaishije? Vivyo hivyo ikiwa utastaafu ukiwa na miaka 40, utakuwa na miaka 20 mbele.

Ukistaafu na miaka 50, utauwa na miaka 10 mbele. Kubwa ninalotaka mjasiriamali ujiulize ni hili utaishije ukifika wakati ambao biashara haziendi ama ule mda utakaokua umechoka kiumri na kiafya kuweza kumudu biashara? Tumeona kuwa wenzetu walioajiriwa huendelea kula pensheni yao hata baada ya kustaafu, Je, mjasiriamali unampango gani?

Ni vema nizitaje fursa zote alizonazo mjasiriamali kujiandaa mapema kwa ajili ya kustaafu. Kwanza mjasiriamali anaweza kuwekeza katika vitega uchumi vya muda mrefu ili vimsaidie pindi atakaokuwa hawezi tena kufanya biashara (kustaafu).

Pili anaweza kusomesha watoto kwa lengo la kuja kumsaidia baadae, tatu anaweza kuweka hisa ama kuwa na biashara katika mifumo rasmi zitakazoweza kumfaa kwa miaka mingi baadae. Fursa nyingine(ambayo ni ngeni kwa wajasiriamali weng) ni hii ya kuweka akiba katika mifuko ya hifadhi ya jami

Hata hivyo kwa mazingira ya ujasiriamali wa kitanzania sio wengi wanaoweza kumudu kuwekeza kenye vitega uchumi vikubwa vya kuwasaidia miaka na miaka baadae. Pia sio wengi wanaoweza kuwekeza katika hisa na biashara za mifumo rasmi. Sasa, wajasiriamali wa kawaida wanafanyaje kujihami na maisha baada ya kustaafu katika ujasiriamali?

Suluhu inapatikana kupitia fursa ya kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii. Kwa kuwa mwanachama katika moja ya mifuko hii inakupa wasaa mjasiriamali hata mwenye mtaji mdogo kabisa kujiwekea akiba kidogo kidogo kwa ajili ya mafao ya kustaafu kwako.

Taratibu, sera na kanuni za namna ya kujiunga zinatofautiana kutoka mfuko mmoja hadi mwingine sambamba na aina ya mafao yanayotolewa. Hata hivyo kuna mifuko ambayo ina mafao mazuri mno kwa ajili ya wajasiriamali.

Mathalani mifuko hii ina faida mbalimbali ikiwemo mafao ya ujasiriamali (mtaji) pamoja na mikopo ya kibiashara kupitia SACCOSS. Mbali na faida za kibiashara mifuko hii inakupa wasaa wa kutoogopa kuhusu familia na afya yako wewe mjasiriamali kwa sababu wana mafao ya matibabu, mikopo ya nyumba, mikopo ya samani, mafao ya elimu pamoja na mafao ya uzazi.

Nitoe wito kwa wajasiriamali wote nchini mjaribu kutembelea moja kati ya mifuko hii ya kijamii iliyokaribu nanyi ili kupata maelekezo na namna ya kujiunga. Furaha yangu itakamilika pale nitakapoona wajasiriamali wadogo na wakubwa wengi iwezekanavyo wakijiunga na mifuko hii ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya usalama wa ujasiriamali wao.

No comments:

Post a Comment