Pages

Pages

Monday, May 13, 2013

Sakata la Lady Jaydee lafikia patamu baada ya kutakiwa kupanda kizimbani rasmi Mei 27



                                                                         Lady Jay Dee
Mwandishi Wetu
SAKATA la mvutano wa msanii Judith Wambura ama Lady Jay Dee na Clouds Media Group limechukua sura mpya baada ya leo mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kumkabidhi hati ya mashtaka mwanamuziki huyo tayari kwa kesi yake kuanza kusomwa Mei 27 katika mahakama hiyo.

                                      Ruge Mutahaba
Jaydee ambaye alipewa wito wa kufika mahakamani hapo Mei 11 mwaka huu, kesi yake itasomwa chini ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, AthumaniNyamlani, huku ikiwa kati ya kesi zenye mvuto kutokana na sakata la msanii huyo na mabosi wake wa zamani, yani Clouds FM, ambayo kabla ya kuingia kwenye sanaa aliwahi kuwa mtangazaji kwenye kituo hicho cha burudani Tanzania.

Jay Dee alifika mahakamani hapo akitokea Baraza la Sanaa Taifa BASATA, ambapo huko nako kulikuwa na watu wengi waliokwenda kusikiliza mazungumzo ya msanii huyo nyota hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo leo, mwanadada huyo alisema kuwa hajajua ameshtakiwa kwa kosa gani hadi atakapotulia na kusoma hati yake ya mashtaka.

"Mei 11 nilipokea taarifa kuwa nahitajika mahakamani Jumatatu ya leo,
nilipowasili hapa nimepewa hii hati ya mashtaka hivyo bado sijajua
nashtakiwa kwa kosa gani, yaani hapa ndio nafungua  hii hati nakutana
na habari hizi," alisema Jaydee.

Wakati akifungua nyaraka hizo mbele ilionekana barua kutoka mahakamani
hapo pamoja na nyakara zilizochapishwa na vyombo mbalimbali ya habari
zikiwemo blogu zilizoelezea ugomvi wake kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa
Clouds Media Group Joseph Kusaga na Mkurugenzi wa Utafiti na Matukio
Ruge Mutahaba.

"Hili ndilo shtaka lenyewe kwa hivyo sisi hatuwezi sema chochote kwa
sasa tunaelekea kwa mwanasheria wetu ili kuanza kuishughulikia kesi
hii," alisema Gadna Habash mume wa mwanamuziki huyo.

Kabla ya kufika mahakamani hapo mchana, mwanamuziki huyo alitoa mada
katika jukwaa la sanaa Basata ambako alizungumzia changamoto nyingi
zilizopo katika kufikia mafanikio kwenye sekta ya muziki.

Wakati kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa Mei 27, Mei 31 Jaydee
anasherehekea miaka yake 13 tangu aingie rasmi katika sekta ya muziki,
katika mgahawa wake wa Nyumbani Lounge.

Sakata la Jay Dee na Clouds limezidi kupamba moto huku mitandao ya kijamii kama vile Face Book, Twitter na blog kudaiwa kuchochea mvutano huo ambao hivi karibuni upande wa Clouds kupitia Mkurugenzi wao wa Utafiti na Matukio, Mutahaba alitolea ufafanuzi.

No comments:

Post a Comment