Pages

Pages

Sunday, May 26, 2013

Diamond: Hata mimi huwa naachwa na wapenzi

Asifia nidhamu ya mpenzi wake mpya Penny

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKALI wa muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva, Nassib Abdulmalick (Diamond) ni mmoja kati ya vijana wanaoendelea kuchanua na kulitafuta soko la Kimataifa.
Diamond, Mwimbaji wa Bongo Fleva Tanzania

Kila kona za Tanzania jina lake huwa mbele, hivyo kuonyesha kuwa msanii huyo hana mpinzani. Diamond ametoa vibao motomoto kama vile Mbagala, Nataka Kulewa, huku kwa sasa akiwa juu kutokana na wimbo aliyoshirikishwa na Ney wa Mitego, Muziki Gani.

Mbali na kutamba katika muziki, Diamond amekuwa na vituko vya kila aina, hasa vile vya kutajwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mabinti wengi na kuacha watu midomo wazi.

Mara baada ya kuwa Star wa Bongo, Diamond alikuwa na Wema Sepetu, kasha akawa na Jokate Mwigelo na sasa Penny anayedaiwa kuwa amefanikiwa kumpa ujauzito.

Mbali na hao, pia wapo mabinti mbalimbali waliotajwa, akiwamo Linah Sanga, Jacqueline Wolper, Irene Uwoya na wengineo, hivyo jina la Sukari ya warembo kuibuka na kushika kasi.

Hivi karibuni, Diamond alifanya mahojiano na mwanadada Sporah nchini Uingereza na msanii huyo kufunguka zaidi kuelezea maisha yake ya sanaa na mapenzi.

“Mimi ni binadamu, ukiacha kazi yangu ya muziki ambayo imefanikiwa kuniweka hapa nilipo sasa, hivyo hata kwenye suala zima la mapenzi, wakati mwingine huwa naachwa mimi.

“Inapotokea nimeachwa na kutafuta msichana mwingine, jamii inaona mimi ndio msumbufu na kuacha wasichana bila sababu, jambo ambalo si kweli hata kidogo,” alisema Diamond.

Msanii huyo anayetamba ndani na nje ya Bara la Afrika, anasema kuwa katika suala zima la mafanikio kwa kupitia ring tone za nyimbo zao, bado kuna mapungufu mengi na wao hawanufaiki.

Fedha kiduchu hupatikana wakati kiasi kikubwa kikienda kwa watu ambao hawajashiriki kwa kitu chochote katika kuandaa nyimbo ambazo baadaye huzitaka katika biashara zao.

Diamond anasema kuwa anapenda sana wasichana wa kileo, warembo na wenye mvuto, bila kusahau wale wenye adabu na nidhamu mbele ya jamii, huku akiwa ni mwenye kumpenda mama yake.

Mkali huyo wa Bongo Fleva, anasema kwa sasa akili yake yote ipo kwa mama watoto wake mtarajiwa Penny ambaye ni mjauzito, huku akisema kuwa mwanadada huyo ana nidhamu ya hali ya juu.

Mkali huyo anayetumia uchawi wa kuzungusha kiuno kuwalainisha mabinti anapokuwa jukwaani anasema kuwa anatamani amuowe Penny hata leo, huku akidai kuwa hana mpango wa kutoka kimapenzi na msichana mwingine, licha ya kuvumishwa habari hizo kila wakati.

“Mtu hata kama awe mzuri vipi, bado nitahitaji nidhamu kwa wote pamoja na kumuheshimu mama yangu, hivyo katika suala hili hakika nalizingatia kwa kiasi kikubwa mno,” alisema.

Msanii huyo anasema kuwa kwa sasa anaendeleza juhudi kuhakikisha kuwa anakuwa na mafanikio makubwa kimuziki, ikiwa ni pamoja na kufanya nyimbo na wakali mbalimbali Afrika na Ulaya.

No comments:

Post a Comment