Pages

Pages

Monday, April 08, 2013

Wataipenda Simba yao na wataichukia pia kwa ubaya wao



SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATU wanaipenda klabu yao ya Simba, ndio maana inapotokea inafanya vibaya, wapo wanaolia na kuziona ndoa zao chungu. Ni ukweli wa aina yake, hasa tunapokutana na ndugu zetu wanaolia na kusaga meno kwasababu ya matokeo mabaya ya timu yao ya Simba.
Mlinda mlango namba moja wa Simba, Juma Kaseja.
Sina tatizo la kufanya vibaya kwa timu kama ya Simba, ukizingatia kuwa kufungwa, kutoka sare au kushinda ndio matokeo ya kawaida katika mchezo wa soka duniani kote.

Pamoja na yote hayo, lakini wadau halisi ya soka hasa mashabiki na wanachama wa Simba, malalamiko yao hayatatajwa kwa sababu ya timu yao kushindwa kutetea ubingwa wake wa Bara.

Mashabiki, wanachama na wadau wa soka kwa ujumla watalalamika Simba yao inavyobaki nyuma licha ya kuona wenzao jinsi wanavyoendelea katika mafanikio ya mpira wa miguu Tanzania.

Alhamisi ya wiki iliyopita, nilibahatika kuwapo kwenye kikao kilichowahusisha viongozi wa Yanga, akiwamo Mjumbe wa Bodi ya Udhamini wa Yanga, Francis Kifukwe, Katibu wake Lawrence Mwalusako na watendaji wa Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group katika kuonyeshwa ramani ya Uwanja wa kisasa unaotarajiwa kujengwa watakapofikia makubaliano mwishoni mwa mwezi wa tano mwaka huu.

Ni kikao kilichoibua ari na mapambano ya kuhakikisha kuwa Yanga sasa inajikomboa katika mchakato mzima wa kumiliki uwanja wao, kama ilivyokuwa kwa klabu ya Azam.

Hakika, katika kikao hicho ambacho mengi yalijadiliwa, ikiwapo Mkataba utakaoingiwa hivi karibuni, nilipata hisia kuwa Yanga wao wameshaamua kufunga mkanda.

Pamoja na yote hayo, hakika siwezi kuvumilia kuona kumbe klabu ya Simba, yenyewe bado imelala usingizi wa pono. Ndio maana nasema kuwa, ingawa klabu ina wanachama au wapenzi wengi, lakini hao hao wataichukia kwasababu ya aina ya viongozi iliokuwa nao.

Simba ikiwa chini ya Ismail Aden Rage, ipo katika mazingira magumu kutokana na kuongozwa na viongozi ambao wameshindwa kuwa wabunifu na kutumia changamoto za kimaendeleo.

Klabu kama ya Simba, ni aibu kama haina kitu cha kujivunia, ukiacha rasilimali watu inayolipia kadi zao. Haya ni mambo ya kushangaza sana. Katika kuliangalia suala hilo, najikuta nikiiwazia zaidi na kuona ipo kwenye mazingira ya kuiweka klabu kwenye hatari zaidi.

Hii siwezi kuvumilia na katu sitabaki kimya, japo watu wachache wanaweza kusema kuwa mimi ni shabiki wa Yanga, Azam au nyingine yoyote, jambo ambalo wadau tunapaswa kuliangalia kwa kina.

Kwa miaka kadhaa sasa, klabu ya Simba baadhi ya viongozi wake, akiwamo Rage wamekuwa wakitumia kauli za kudanganya, hasa zile za Uwanja wa Bunju, ambao haueleweki kichwa wala mguu.

Eneo hilo linalodaiwa na viongozi wa Simba bado si mali halali ya klabu hiyo, kutokana na kauli za kudanganya zinazotolewa mara kwa mara. Kama hivyo ndivyo, Simba yenye migogoro lukuki, haiwezi kamwe kuweka mambo sawa kwa ajili ya maendeleo ya klabu husika.

Huo ndio ukweli wa mambo. Na hakika kila mwanachama, shabiki na wadau wa michezo hasa wa Simba wanapaswa kuangalia aibu inayoweza kujitokeza miaka mwili ijayo, endapo wazo la klabu ya Yanga kuwa na uwanja wake litatimia kutokana na juhudi zao.

Kwa mujibu wa kikao cha Yanga na watakaowapa kazi ya kujenga uwanja, inaweza kukamilika kwa kipindi kifupi endapo makubaliano yatakwenda vizuri na kufanikisha suala hilo.

Haya ni maendeleo makubwa katika soka la Tanzania, lakini pia yatakuwa sehemu ya kuitusi klabu ya Simba na vinginevyo vyenye kujiendesha kiubabaishaji na kuiweka nchi kwenye mashaka.

Katika hilo, hakika siwezi kuvumilia na kuna kila sababu ya kujiangalia upya kwa ajili ya Tanzania yenye maendeleo katika michezo na sio kushuhudia yale yenye kukera na kushangaza umma.

Ndio maana nasema, wataipenda Simba yao na kuichukia kwa ubaya wa viongozi wao wasiokuwa na dhamira ya kuikomboa kutoka hapa na kuipaisha juu kama zinavyoelekea klabu za Azam na sasa Yanga kama nayo itafanikiwa.

Mungu ibariki Tanzania.
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment