Pages

Pages

Tuesday, April 09, 2013

Mhaya wa kwanza aliyeziba pengo la Jose Mara FM Academia


AHMED ABRAHAM MPENDA
UKIENDA kwenye shoo za bendi ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma, utashangaa kusikia sauti ya Jose Mara ikirindima katika nyimbo alizowahi kuimba hapo.
 Levy Boy akiwa katika pozi zito alipokutwa New Msasani Club mwishoni mwa wiki.
Levy Boy kulia akionyesha manjonjo yake jukwaani.
Baada ya kusikia, hasa kama hutaona anayeimba hapo, utashangaa na kujiuliza maswali lukuki, ukizingatia kuwa kwa sasa Jose Mara hayupo tena Ngwasuma.

Hupaswi kujiuliza maswali hayo, maana vipande vyote vya mwanamuziki huyo kwa sasa vinaimbwa na Ahmed Abraham Mpenda ama Levy Boy, ambaye kabila lake la Mhaya linazidisha maswali kwanini ameamua kuwa mwanamuziki?

Sauti yake inafanana kabisa na Jose Mara, ingawa mwenyewe anakiri kuwa ameamua kutumia sauti hiyo kwasababu ya kuwaridhisha mashabiki wake, huku akijigamba kuwa ana sauti yake na aina yake nzuri ya uimbaji.

Katika mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Levy Boy anasema kwamba kuimba sauti ya Jose si kama ameshindwa kuwa na yake kwa ajili ya kuonyesha zaidi uwezo wake katika muziki wa dansi nchini.

Alisema mara baada ya Jose ambaye kwa sasa yupo Mapacha Watatu kuondoka, uongozi uliona yeye ashike nafasi hiyo, hasa baada ya kusikika akiimba kwa ufanisi wa hali ya juu.

“Namshukuru Mungu maana nimepata nafasi ya kuimba mbele ya wanamuziki mahiri, akiwamo Rais wa Vijana, Nyosh El Sadaat, Patchou Mwamba, Pablo Masai na wengine wenye uwezo wa hali ya juu wa kuimba.

“Hii ni njia nzuri kwangu, ukizingatia kuwa kabla ya kupewa kipaza sauti, nilikuwa ni mcheza shoo na hakuna aliyewahi kufikiria kuwa naweza kusimama jukwaani kama mwimbaji au kutumikia nafasi zote kwa pamoja,” alisema.

Levy Boy anasema kuwa uwezo wake wa kuimba kwa ufanisi jukwaani umetokana na kufuata nyayo za Nyosh, mmoja ya wanamuziki wenye vipaji vya kutisha.

Anasema kitu kinachompa nguvu katika kutafuta nafasi ya kuwika katika muziki kunatokana na kutamani kulipaisha kabila lake, hasa baada ya kukosekana Wahaya katika tasnia nzima ya muziki wa dansi nchini.

Mwanamuziki huyo anayefanya makubwa katika bendi hiyo ya Wazee wa Ngwasuma anasema kuwa ingawa kwa sasa anatumia sauti ya Jose Mara, lakini tayari ameshafanikiwa kuingiza vipande vyake katika albamu yao mpya itakayokwenda kwa jina la Chuki ya Nini.

Kijana huyo anasema kuwa itakuwa vibaya kama ataendelea kutumia sauti ya mtu mwingine kila siku, hivyo anaamini kuwa mara baada ya nyimbo alizotumia sauti na mtindo wake mwenyewe watu watampokea vizuri.

“Lengo ni kuendeleza makali yangu na kuonyesha kipaji changu cha uimbaji, hivyo naomba mashabiki wangu wakae mkao wa kula kupata vitu adimu kutoka kwangu.

“Katika hili siwezi kujisahau kamwe kama wanavyofanya wengine, hivyo kubwa ninalofanya ni kuhakikisha kuwa namuomba Mungu ili aniwezeshe katika maisha yangu ya muziki,” alisema.

Levy anasema ili kipaji chake kiweze kutokea pazuri na kila mtu aone mchango wake, hatakuwa karibu na masuala ya ushirikina, badala yake atatumia nguvu za Mungu na dua za wapenzi wake katika tasnia ya muziki wa dansi.

Kijana huyo anasema kuwa tangu mwanzo alikuwa akipenda muziki, ndio maana alivyopata nafasi ya kucheza shoo Ngwasuma, alijiona kuwa anaelekea kwenye hatua nzuri.

Anasema kuwa alifanya kazi zake kwa ufanisi na kumvutia kila mtu, hatua ambayo imekuwa kubwa zaidi alipoibuliwa pia katika uimbaji, akiziba pengo la Jose.

Mwanamuziki huyo anasema kwamba siku ya kwanza anapanda jukwaani kama mwimbaji, Jose hakuamini na kujikuta akienda kumtunza kutokana na kukubali sauti yake.

“Awali nilijua labda Jose atanichukia, lakini nashukuru alinitia moyo na kuniomba niendeleze makali yangu, akiamini ni kipaji kipya kimetokea.

“Naamini hata kesho Jose atakaporudi tena Ngwasuma au kukutana naye sehemu nyingine kwenye maisha ya muziki wa dansi, bado tunaweza kufanya kazi pamoja na kufikia hatua nzuri, maana kila mmoja ana uwezo wake,” alisema.

Kubwa analofanya ni kuona naweza kufikia malengo ya wanamuziki wengine wakubwa, ikiwa ni baada ya kutokea pazuri nikiwa na waimbaji wengine wenye uwezo wa juu katika bendi nzima ya Wazee wa Ngwasuma.

Mbali na kuingia katika uimbaji, lakini bado anaendelea na makali yake ya uchezaji kwakuwa vyote ni vipaji vyake, huku akijua kuwa mwimbaji anayeweza na kucheza huwa na matokea mazuri katika maisha yake.

Anasema siyo tu, bali waimbaji wote wa FM Academia wanasimama katika nafasi zote za uimbaji na uchezaji, akitolea mfano wa shoo yao ya mitindo 360 inayoonyeshwa kila Jumapili katika Ukumbi wa New Msasani Club.

“Hii ni shoo kubwa inayoshangaza wengi, maana waimbaji wote pamoja na wacheza shoo hujumuika katika jukwaa moja na kuonyesha mitindo hiyo bila kuchoka na kufurahisha wadau wengi katika bendi yetu.

“Kila mmoja anafurahia matokeo ya kazi zetu, ndio maana Ngwasuma imezidi kutesa kileleni na hakuna anayepinga kuwa sisi hatustahili kuwa kileleni,” alisema.

Levy anasema kamwe hatalewa sifa na kujiona amefika, zaidi ya kuwa mnyenyekevu kupokea ushauri wa waimbaji wengine na mashabiki ili awe juu zaidi.

Levy anasema kuwa yoyote anayependa kuona uwezo wake ajaribu kuhudhuria shoo za bendi yao au kusubiria albamu ya Chuki ya Nini ambayo ameimba kwa uwezo wa aina yake akitaka kutangaza kipaji chake.

Levy aliyezaliwa mwaka 1983 Bukoba vijijini mkoani Kagera, anasema kuwa kubwa analofanya ni kuangalia nyendo za wakali wa muziki wa dansi ili iwe njia yake ya kufika mbali kisanaa.

No comments:

Post a Comment