Pages

Pages

Wednesday, April 17, 2013

Wapinzani wa Azam, AS Far Rabat ya Morocco sasa kutua saa saba mchana leo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TIMU ya AS FAR Rabat ya Morocco itakayoikabili Azam kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho inatua nchini leo (Aprili 17 mwaka huu) saa 7.30 mchana kwa ndege ya Qatar Airways.
Msemaji wa TFF, Boniface Wambura
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, msafara wa timu hiyo wenye watu 28 kwa ajili ya mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa Jumamosi (Aprili 20 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utafikia hoteli ya Sapphire iliyoko maeneo ya Kariakoo.

Wakati Azam imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa timu ya Barrack Young Controllers II ya Liberia kwa jumla ya mabao 2-1, AS FAR Rabat imeingia raundi hiyo moja kwa moja kutokana na nchi hiyo kufanya vizuri kwenye michuano ya klabu Afrika.

Timu nyingine ambazo zimeingia raundi hiyo moja kwa moja katika Kombe la Shirikisho kama ilivyo AS FAR Rabat ni Asec Mimosas ya Ivory Coast, Atletico Petroleos (Angola), C.S.S. (Tunisia), DC Motema Pembe (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Ahly Shandy (Sudan), Enppi (Misri), Heartland (Nigeria), Ismaily (Misri), Lobi Stars (Nigeria), U.S.M. Alger ya Algeria na Wydad Casablanca (Morocco).

Mwamuzi Emile Fred atakayesaidiwa na Steve Maire, Jean Ernesta na Jean Claude Labrossa wote kutoka Shelisheli ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Kamishna ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda. Waamuzi watawasili nchini kesho (Aprili 18 mwaka huu) jioni.

No comments:

Post a Comment