Pages

Pages

Tuesday, April 09, 2013

Rungu zito la TFF latua Yanga, bu....



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KLABU ya Yanga na Kocha Msaidizi wa timu ya Toto Africans, Athuman Bilali wamepigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja kutokana na makosa mbalimbali katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea nchini.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji akizungumza na waandishi wa habari.
Adhabu hizo zimetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Jumapili (Aprili 7 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za waamuzi na makamishna kwa michezo namba 108 hadi 171.

Yanga imepigwa faini hiyo baada ya kupata kadi tano za njano katika mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Februari 7 mwaka huu. Vilevile Kagera Sugar imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) dhidi ya African Lyon iliyochezwa mjini Bukoba, Februari 23 mwaka huu.

Naye Kocha Bilali amepigwa faini hiyo na kufungiwa mechi tatu za ligi hiyo kwa kumshambulia kwa maneno kocha wa timu pinzani, hali iliyosababisha mwamuzi amtoe kwenye benchi la wachezaji. Alifanya tukio hilo kwenye mechi kati ya Toto Africans na Tanzania Prisons iliyochezwa Aprili 3 mwaka huu jijini Mwanza.

African Lyon na Simba zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa kushindwa kuchezesha timu zao za U20 kwenye mechi za utangulizi wakati zilipocheza na Oljoro JKT na Coastal Union, Machi mwaka huu kwenye viwanja vya Azam Complex na Uwanja wa Taifa.

Suala la Meneja wa Coastal Union, Akida Manchai kumshambulia kwa maneno yasiyo ya kiungwana Makamu Mwenyekiti wake Steven Mnguto baada ya kwenye mechi kati ya African Lyon na Coastal Union iliyochezwa Machi 30 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex limepelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu, huku adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom.

No comments:

Post a Comment