Pages

Pages

Thursday, April 25, 2013

MGODI UNAOTEMBEA



Ni aibu, thamani ya kura yao imegeuka matusi
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BUNGE la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma, limeleta picha mpya inayochefua kuitazama mara kwa mara. Ni picha isiyofurahisha macho wala hisia za ndani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
Ni kutokana na baadhi ya wabunge wetu kujiondoa kwenye uwakilishi wa wananchi kwa kutetea maslahi ya wapiga kura wao, badala yake wanaparuana wenyewe pamoja na kupeana maneno ya shombo, kejeli, matusi ya kila aina.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freemani Mbowe
Katika mfululizo wa makala zangu, nilijaribu kupinga maoni ya Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan aliyechangia kwa kuwataka watu kabla ya kugombea Ubunge, wapitie kwanza jeshi ili wajifunze uzalendo.

Sio kweli, maana uzalendo wa kweli hauwezi kupatikana JKT wanapofundishwa kwa wiki moja au mbili, tena wakiachwa wafanye kila wakipendacho, ikiwapo kupigana picha na kuziingiza kwenye mitandao ya kijamii, hasa wa facebook.

Ajabu. Suala hili haliwezi kuleta uzalendo kamwe. Kwanini nasema hivyo, kabla ya bunge la bajeti kuanza mjini Dodoma, wabunge wengi walipata nafasi ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Licha ya kujiunga na jeshi hilo, lakini tunashuhudia vitendo vichafu vya utovu wa nidhamu bungeni. Lugha chafu zenye ukakasi zinachukua nafasi kubwa katika vinywa vya wabunge wetu.

Ina maana hakuna uzalendo. Tena kama maneno hayo yanatoka kwa watu waliopitia mafunzo hayo ya wiki mbili, ina maana walichofundishwa huko hakuna walichoambulia.

Ni jambo la kushangaza umma. Kila mbunge kwa sasa angekuwa na walau robo ya huruma na wananchi wake angejaribu kutembea katika maduka ya vyakula kujionea hali inavyotishia uhai wa wananchi wao.

Mbunge mwenye uzalendo na huruma na wananchi wake, kila sekunde inayopita, asingekubali iende bila kuwa na faida yoyote, hasa katika Bunge hilo la Bajeti linaloendelea.

Kwa bahati mbaya, Bunge ni sehemu ambayo kila kinachojadiliwa kinazalisha mguso na hisia kwa wanaofuatilia. Kama mbunge husika atatoa maneno ya utumbo, ina maana anayemuangalia, anaweza kujifunza kulingana na uwezo wake wa kupambanua mambo.

Ndio hapo tunapotakiwa kuwaangalia kwa kina watu hao waliochaguliwa kwa sababu moja tu, kuwawakilisha wananchi wao na kuyapata maisha bora, kama ilivyokuwa kauli mbiu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenyekiti wa CCM.

Kinachoendelea sasa ni ishara kuwa moja ya adui katika Taifa hili, umasikini hatuwezi kuushinda kamwe. Hakuna mipango zaidi ya kelele na porojo za baadhi ya wabunge.

Kwa bahati mbaya zaidi, maneno ya shombo, matusi, kejeli kutoka katika vinywa vya wabunge wetu yamezidi kupamba moto baada ya masuala ya udini na kutetea vyama yakichukua nafasi yake.

Laiti kama wote wangekuwa wanajadili jambo moja la umasikini kwa Watanzania, sidhani kama wangefikia kupeana maneno machafu kama yanavyoendelea mjini Dodoma.

Kwa mfano, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, anapochangia kwa kirefu tatizo la ajira kwa wananchi wake, sidhani kama Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, angepinga, tena kwa matusi.

Sidhani kama Tundu Lissu, moja ya wabunge makini katika Taifa hili, angepinga kama hoja ya inayowahusu Watanzania wote, hata kama ingetolewa na Juma Nkamia, John Komba, Murtaza Mangungu, Peter Selukamba na webunge wengine kutoka CCM.

Bali matusi bungeni yamezidishwa na wabunge hao kuanza kupigiana chapuo la vyama vyao, dini zao, jambo ambalo hakika litaiweka nchi katika mazingira magumu mno.

Hili linatakiwa kuangaliwa kwa kina. Hatuna uwezo wa kuyapata maisha bora, kama hoja thabiti, zenye mguso na watu zitawekwa kando na kushuhudia ujinga ukishamiri katika vinywa vya baadhi ya wabunge wa 
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni vyema sisi wananchi pia tukawa wakali zaidi. Madamu siku hazigandi, nadhani swali moja tu, ulipokuwa Bungeni kwa miaka mitano ulinifanyia jambo gani zuri ili nikuchaguwe tena?

Baada ya swali hili nadhani jibu lake litakuwa zito mno. Mbunge ambaye muda wake mwingi ameutumia kusikiliza au kutoa maneno machafu dhidi yaw engine, atajifikiria mara mbili.

Ndio hapo Mtanzania atakapojua nani anafaa kurudi au kuondoshwa katika nafasi hiyo nyeti. Ubunge ni zaidi ya uwakilishi. Kushuhudia mguso na utitiri wa watu wanaotaka kuingia bungeni, kunaonyesha kuwa hapo ni mahali pazuri.

Watu wanakwenda kufanya biashara zao, hivyo nafasi ya ubunge kwao ni sahihi ili iwanufaishe. Mfanyabiashara ambaye yupo bungeni, si kama atakavyokuwa mwingine ambaye hana cheo chochote serikalini.

Ndio maana mtu yupo radhi atumie Milioni 100 akijua fika ndani ya miaka mitano, atavuna fedha nyingi pamoja na heshima anayopewa kwa kofia yake ya ubunge.

Huu ni wakati wa kujitazama upya. Maisha ya Mtanzania, yule anayelala nje, anayezagaa mtaani bila kuwa na ajira sidhani kama ni jambo zuri kumuona Mbunge akipiga soga tu.

Maisha yamezidi kuwa magumu. Wapo wananchi ambao siku zote si hodari wa kujadili siasa, wala kuchanganywa na siasa. Hawa wanapokutana na vitu vya kustaajabisha, wanazidi kuwa na hasira na kukosa hamu ya kupanga mstari kupiga kura.

Huu ndio ukweli wa mambo. Ndio maana wanaharakati wanaumiza kichwa juu ya Watanzania wengi kukosa hamu ya kupiga kura, tofauti na watu wa Kenya, ambao kwenye suala la kupiga kura hawana utani.

Hapa kwetu wenye uwezo wa kupiga kura ni 2000 katika mtaa husika, lakini mwisho wa siku waliopiga kura ni watu 150 tu. Hili ni jambo la kusikitisha mno.

Linachangia kwa kiasi kikubwa kudumaza Demokrasia pamoja na kiu ya kuchaguliwa wale wenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi wao wanaoendelea kuishi kwa kubangaiza.

Pamoja na hayo, mengi yanayosababisha watu kukosa hamu ya kupiga kura ni kutokana na wachaguliwa hao baadaye kufanyaa vitendo visivyokuwa vya kiungwana, kuwatumikia kwa nguvu moja watu wao, kutoka kwenye nkundi la viongozi na kuwa wafanyabiashara wa siasa, jambo ambalo linamuongezea utajiri wa kutisha ndani ya kipindi kifupi, wakati aliyemchagua hajui atakula nini.

Haya na mengine mengi yamewafanya baadhi ya Watanzania waone hawana haki, au sababu ya kupanga foleni kupiga kura, akiamini hakuna cha maana anachoweza kukipata.

Hili ni jambo linalotakiwa liangaliwe upya na kila Mtanzania, kama lengo ni kuweka utaratibu mzuri wenye dhamira ya kupandisha chati ya maisha ya kila mmoja wetu.

Hayo tutayajua na kuyadhibiti kwa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa maisha, utendaji kazi wa wale tuliowapa dhamana ya kutuongoza, huku tukiwakalia kooni katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu.

Tusiwachaguwe bila kuwabana, ukihakikisha kuwa kukua kwa sayansi na teknolojia, kumesababisha Tanzania kuwa kama kijiji. Ingawa mtu anaishi wilayani Handeni, Iramba, Hai, Mvomero, Manyoni, Maswa, Ifakara, lakini anao uwezo wa kujua nini anafanya Mbunge wake ili apate nafasi ya kumwajibisha ndani ya sanduku la kura, hasa kwa wale ambao wamekuwa watawala wa maisha, wakitaka kila siku wagombee tena na tena.

Kama wilaya haina jipya, hakuna huduma za afya za uhakika, elimu ya kujikongoja, watu wanakufa njaa bila kujua la kuwakomboa, kuna haja gani ya kumchekea mtu ambaye ndani ya miaka mitano alipokuwa bungeni aliitumia kupiga stori na mafariki zake, kuzunguuka na kula upepo pamoja na kula posho nyingi, huku akishindwa kuzikabiri nchangamoto za watu wake hata kwa asilimia 10 tu.

Huu ni wakati wa kujiangalia upya, hasa katika kipindi hiki ambacho Bungeni kunaendea filamu ya maneno ambayo katu si yaliyowapeleka katika jengo hilo muhimu kwa Watanzania wote, ukizingatia kuwa ni aibu thamani ya kura yao kugeuka matusi.
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment