Pages

Pages

Friday, April 26, 2013

Ligi Daraja la Pili Dar es Salaam kumalizika kesho

Na Rahimu Kambi, Dar es Salaam
LIGI Daraja la Pili Mkoa wa Dar es Salaam hatua ya sita bora inamalizika kesho ambapo timu tatu zitakata tiketi ya kucheza hatua ya Kanda ili kupata nafasi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Msemaji wa DRFA, Mohamed Mharizo
Ofisa Habari wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Mohamed Mharizo, amesema leo mchana kuwa ligi hiyo iliyoanza Aprili 15 ndio itapata wawakilishi watatu watakaouwakilisha mkoa huo katika hatua ya Kanda.

Alizitaja mechi zitakazochezwa leo kuwa ni Red Coast itakuwa ikimenyana na Day Break kwenye uwanja wa Kinesi, wakati kwenye Uwanja wa Makurumla, Friends Rangers wao watakuwa wakichuana vikali na Sharif Stars, huku kwenye Uwanja wa Airwing, Boom FC itakuwa ikikabiliana na Abajalo.

Hadi sasa Red Coast inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 8, ikifuatiwa na Abajalo yenye pointi 7, wakati Sharif Stars inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 6.

Friends Rangers wao wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 5 huku Day Break wakiwa na pointi 3 na Boom FC ikishika mkia kwa kujikusanyia pointi 2.

Mharizo aliwataka mashabiki wa timu hizo kuhakikisha wanafika uwanjani kwa wingi kushuhudia mechi hizo kwa usalama ili kuepuka kuvuruga mashindano.

“Kuna mashabiki wa baadhi ya timu wamekuwa wakifanya vurugu, tabia hiyo si ya kiungwana na DRFA haipendezwi nayo, ndio maana tumeona tuweke ulinzi katika baadhi ya mechi, hata kesho (leo) ulinzi utaimarishwa ili kuhakikisha mashindano yanamalizika kwa usalama,” alisema.

No comments:

Post a Comment