Pages

Pages

Wednesday, April 03, 2013

Japhet Kaseba ajipa matumaini katika masumbwi



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Japhet Kaseba, amesema kuwa kwa sasa uwezo wake unaonyesha umezidi kuimarika katika mchezo wa masumbwi kutokana na kufanya mazoezi ya kutisha.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Kaseba alisema kuwa amekuwa kwenye mikakati ya kuwa juu katika masumbwi, jambo linalomfanya asifanye mzaha katika mazoezi.
Japhet Kaseba
Alisema mabondia wote wa Tanzania watarajie ngumi nzito kutoka kwake, hasa baada ya kufanikiwa kumpiga Maneno Oswald katika Ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa na kuwafurahisha mashabiki wake.

Mwanamasumbwi huyo aliyewahi kuwa Bingwa wa Kick Boxing, alisema kuwa anaamini kuwa utaratibu wake katika suala zima la mazoezi ni jambo linalomuweka juu katika mchezo huo.

“Kwa sasa sina mzaha kabisa katika ngumi, hivyo naamini kila atakayetia pua mbele yangu atakula kichapo, maana najitahidi kadri ya uwezo wangu kujifua kwa kuona ndio mtaji katika ngumi.

“Kikubwa ni kuhakikisha kuwa nafanya maajabu zaidi kwa kutoa upinzani kwa kila mtu, ukizingatia kuwa baadhi ya watu wamekuwa wanaogopa kukutana na mimi kwa kujua sio bondia mwenye mzaha,” alisema.

Pambano la Kaseba na Oswald lililofanyika katika Ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa, liliandaliwa na bondia wa ngumi za mateke nchini, Pendo Njau na kukutanisha wakali mbalimbali wa mchezo wa ngumi nchini.

No comments:

Post a Comment