Pages

Pages

Thursday, April 18, 2013

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MH. PROF. KULIKOYELA KANALWANDA KAHIGI (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA RAIS – MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014



       Mheshimiwa Kulikoyela

 1.     UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2013, naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya 2012/2013 na makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kipindi hiki itajikita katika mambo machache mahususi katika Ofisi ya Rais - katika Utawala bora, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mahusiano na Uratibu - ambayo tunayaona ni mapungufu. Lengo la kufanya hivyo ni  kuitaka Serikali ama ichukue hatua ya kuyatokomeza mapungufu hayo kwa kutangaza hadharani nia yake ya kuyakomesha, kisha ichukue hatua mwafaka, au ijiuzulu kwa kushindwa kuongoza dola.

2.   UTAWALA BORA 
2.1.        Idara ya Usalama wa Taifa – Ikulu
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA imeitaka Serikali kuwachukulia hatua maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa – Ikulu ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu vya utekaji na utesaji kwa watu wanaoonekana kuikosoa Serikali, lakini mpaka sasa hakuna hatua dhahiri  zinazochukuliwa ilhali matukio hayo ya utekaji na utesaji yanazidi kuongezeka katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, aliyetajwa na Gazeti la Mwanahalisi kuhusika na kitendo cha kinyama cha kumteka na kumtesa Dkt. Ulimboka mwezi Juni, 2012 ni afisa wa Usalama wa Taifa, Ramadhani Ighondu Abeid. Tulitarajia Serikali, kupitia Jeshi la Polisi, ingemkamata na kumhoji mtu huyu ili kujiridhisha na tuhuma dhidi yake na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini mpaka leo hakuna chochote kilichofanyika kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu aliofanyiwa Dkt. Ulimboka, jambo ambalo linaashiria kwamba Serikali iliridhika na kilichotokea. Lakini jambo baya zaidi ni kwamba Gazeti la Mwanahalisi lililosaidia kugundua uhalifu huo lilifungiwa kwa muda usiojulikana.
Mheshimiwa Spika, mazingira ya kuteswa kwa Mhariri wa Shirika la Habari, ndugu Absalom Kibanda yanafanana sana na yale ya kutekwa na kuteswa kwa Dkt. Ulimboka. Aidha, aina ya utesaji (mfano kung’olewa kucha, meno na kutobolewa jicho) unafanana sana na aina ya mateso aliyopata Dkt. Ulimboka. Hivyo, ushahidi wa kimazingira unaonesha kwamba waliomteka na kumtesa Dkt. Ulimboka yumkini ni walewale waliomteka na kumtesa Absalom Kibanda au mawakala wao.
Mheshimiwa Spika, katika sakata la Dkt. Ulimboka, jeshi la polisi lilidai kuwa limemkamata mtu mmoja lililodai kuwa ni raia wa Kenya ambaye hatima ya kesi yake haijulikani mpaka sasa. Kwa tukio la Absalom Kibanda hadi sasa hakuna taarifa rasmi ya watu walioshtakiwa kuhusu uhalifu huu dhidi ya binadamu. Dkt. Ulimboka ambaye angeweza kutoa msaada kwa Polisi kuwakamata waliohusika na uhalifu huo, hajahojiwa mpaka leo ingawa katika kiapo chake alichokiandika mbele ya mwanasheria wake alimtaja afisa wa Usalama wa Taifa - Ikulu kuwa alihusika kumteka na kumtesa. Inashangaza sana kwa nini Serikali haijataka kutumia maelezo ya Dkt. Ulimboka mwenyewe kuwakamata wahalifu. Jambo jingine la kusikitisha ni kwamba kuna dalili za wazi kwamba suala la kutekwa na kujeruhiwa vibaya kwa Absalom Kibanda limesahaulika kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu ya Tanzania (Penal Code), kuteka na kutesa ni makosa ya jinai. Ni aibu kwa Idara ya Usalama wa Taifa iliyokabidhiwa jukumu kubwa na la heshima kubwa la kuulinda usalama na usitawi wa nchi kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kikatili kama hivi. Kitendo cha kuhisiwa tu kwamba chombo hiki cha usalama kinajihusisha na vitendo vya kijinai moja kwa moja kinakikosesha sifa ya kufanya kazi ya usalama wa taifa. Na kwa kuwa chombo hiki kiko chini ya mamlaka ya Rais moja kwa moja  tayari ni doa kubwa kwa  Rais mwenyewe, Serikali yake na hata kwa chama chake.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ujasusi na Usalama ya Tanzania (Tanzania Intelligence and Security Services Act) ya 1996, Idara ya Usalama wa Taifa hairuhusiwi kufanya upelelezi wa ufuatiliaji - “ushushushu” kwa watu wanaoipinga  Serikali kwa misingi ya kisheria na kikatiba (kwa maana ya vyama vya siasa, vyombo vya habari na wanaharakati). Ibara ya 5(2), kipengele ‘a’ na ‘b’ inasomeka hivi:
              “It shall not be the function of the Service :      
a)   to enforce measures for security or;
b)   to institute surveillance of any person or category of persons  by reason only of his or their involvement in lawful protest or dissent in respect of any matter affecting the constitution , the laws or the Government of Tanzania”.

Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi, sheria inasema hivi:
“Haitakuwa kazi ya Idara kufanya yafuatayo:
a)    kutekeleza hatua za usalama, au
b)   kufanya upelelezi wa ufuatiliaji wa mtu yeyote au kundi lolote la watu kwa sababu tu ya kuhusika na kupinga au kushiriki maandamano halali kuhusiana na jambo lolote la kikatiba, sheria au Serikali ya Tanzania”.

Mheshimiwa Spika, nimelazimika kunukuu sheria hii kwa kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, inao ushahidi kwamba maafisa wa Usalama wa Taifa wamekuwa wakifanya upelelezi wa ufuatiliaji (surveillance) kwa watu wanaoipinga Serikali kwa misingi ya Katiba na sharia - jambo ambalo ni  kinyume na sheria iliyopo.

Mheshimiwa Spika, ushahidi wenyewe ni kwamba baada ya  Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama  wa CHADEMA kutuhumiwa kwamba  anahusika na ugaidi na video yake kurushwa kwenye mitandao ya kijamii, Muhidin Issa Michuzi, ambaye ni mpiga picha wa Rais, Ikulu, aliandika barua-pepe kwa Salvator Rweyemamu, Prosper Mbena, Hamis Mwinyimvua, Liberatus Mulamula, Msafiri Marwa, Laurent Ndumbaro na wengine ambao ni watumishi wenzake wa Ofisi Binafsi ya Rais akiwapongeza kwa kazi nzuri na ya ziada waliyoifanya ya kutengeneza video ya Lwakatare, na kuwaeleza  kuwa hiyo ni kete kubwa  kwao hivyo lazima waipigie kelele sana.

Mheshimiwa Spika, kuna ushahidi mwingine kwamba baadhi ya maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) wanawahonga kwa kuwalipa fedha watumishi wa CHADEMA ili watoe ushahidi wa uongo dhidi ya kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na usalama wa CHADEMA. Miongoni mwa maafisa hao ni Sinbard Mwagha. Huyu ni ni afisa usalama wa taifa anayefanya kazi makao makuu ya idara hiyo. Taarifa zilizopo ni kwamba ndiye anayetumika kuendesha michezo ya kuhonga wanasiasa wa CCM na upinzani, na kwamba ndiye anayehusika pia   kuwapanga wabunge wa CCM waongee nini bungeni wakati wa vikao vya bunge kwa maslahi ya CCM.
begin_of_the_skype_highlighting
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu (Penal Code), kutengeneza ushahidi wa uongo (fabrication of evidence) ni kosa la jinai na adhabu yake ni kifungo cha miaka saba gerezani. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inalitaka Jeshi la Polisi kumkamata haraka sana Sinbad Mwagha ambaye tuna imani anafahamika na kumfungulia mashtaka ya kuhusika katika kutengeneza ushahidi wa uongo dhidi ya kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Ndugu Wilfred Lwakatare. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina juu ya hatua ilizochukua hadi sasa dhidi ya maafisa wa usalama wengine ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu.

2.2.      TAASISI YA KUPAMBANA NA KUZUIA RUSHWA NA MWELEKEO WA MATUKIO YA RUSHWA NCHINI
2.2.1 Rushwa inavyodidimiza uchumi na Maendeleo ya Taifa
Mheshimiwa Spika, rushwa na ufisadi bado ni tatizo kubwa katika nchi yetu na kikwazo kikubwa katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.  Bado hatujafanikiwa kupunguza tatizo hili kubwa linalodidimiza uchumi wa nchi yetu na linalochangia katika kujenga matabaka ya matajiri haramu na masikini waliosababishiwa umasikini na mfumo wa kifisadi.
 Mheshimiwa Spika, kwa sababu Serikali ina kigugumizi kuhusu rushwa na ufisadi, baadhi ya taarifa zihusuzo mambo hayo hufichwa. Kwa mfano, Serikali imekaa kimya kuhusu baadhi ya mikataba na ripoti mbalimbali – jambo linalotafsiriwa kwamba ni mchakato wa kuwalinda watu waliohusika na vitendo vya rushwa au ubadhirifu.
Mheshimiwa Spika,  ripoti  kwa mfano za  EPA, MEREMETA, Uchunguzi na ukaguzi wa kituo cha mabasi Ubungo, ripoti ya ufisadi katika UDA, ripoti ya sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini David Jairo - ni baadhi tu ya ripoti ambazo bado ni siri.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya “The NATIONAL GOVERNANCE AND CORRUPTION SURVEY ya mwaka 2009,  Ubinafsi na tamaa hasa ya viongozi wa Serikali  inaongoza kwa asilimia 95.5 kama kisababishi cha rushwa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kuna aina ya rushwa anayonufaika nayo afisa wa Serikali kwa kupewa mgawo wa kifisadi baada ya kutoa kandarasi kinyume na utaratibu au upendeleo kwa kampuni fulani. Hivyo, fedha hizo za mgawo zinaelekezwa kwa taasisi ambayo ana uhusiano nayo au kujengewa nyumba ilimradi fedha hizo za kifisadi zisipitie kwenye akaunti yake binafsi.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumetokea maafa ya kuanguka kwa majengo ya ghorofa na kuangamiza maisha ya watu hapa nchini.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba maafa haya yalitokea kwa sababu ya mfumo wa kifisadi na rushwa katika utendaji wa Serikali. Hii ni kwa sababu Serikali ilishashauriwa na na tume ya uchunguzi iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuwa maghorofa zaidi ya 100 Dar es Salaam yamejengwa chini ya kiwango, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, pamoja na Tume hiyo kutumia mamilioni ya fedha za walipakodi kufanya uchunguzi na kuandika taarifa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashawishika kuamini kwamba ukimya wa TAKUKURU kwenye maafa haya ya maghorofa kuporomoka ni kutokana na taasisi hiyo kuwa sehemu ya mfumo wa kifisadi unaoitafuna nchi hii. Ukiukwaji wa makusudi wa kikomo cha maghorofa (maghorofa 10) ulikuwa ni ishara tosha kuwa mradi huu uligubikwa na ufisadi – na TAKUKURU ilipaswa kufanya kazi yake ili kubaini kwa nini maghorofa yalizidishwa, na pia kwa nini hadi wakati huo taarifa za Tume ilikuwa haijatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, sababu moja muhimu iliyotajwa katika Taarifa ya Tume hiyo ni kukosekana kwa usimamizi na uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa serikali (86%), uwezo mdogo wa kusimamia sheria na kuhakikisha zinatekelezwa na upungufu katika utoaji wa adhabu kali kwa wanaojihusisha na vitendo vya rushwa (85.6%).
Mheshimiwa Spika, ili tuweze kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, kwanza kabisa ni lazima tujenge taasisi imara na huru na zenye kufanya kazi zake kwa weledi na umakini mkubwa. Lazima taasisi hizi si tu ziwe huru; bali pia zionekane kuwa huru.  Muundo wa TAKUKURU ni vyema ukaangaliwa upya katika mchakato unaoendelea hivi sasa juu ya kuandika Katiba mpya.
Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi wa TAKUKURU ambaye ni mteule wa Rais, ni vigumu sana kuwa huru na kuvichunguza vyombo vingine ambavyo vipo chini ya mamlaka ya Rais. Kwa maneno mengine, ni vigumu kumchunguza aliyekuteua na kuchukua hatua kali dhidi yake.  Katika mfumo uliopo, Rais huyo huyo ndiye Mwenyekiti wa chama tawala; hivyo inakuwa ni vigumu sana kwa chombo hiki kuchukua hatua kali hata dhidi ya chama; kwani kufanya hivyo kutakuwa pia ‘kumuadhiri’ mkuu wake wa kazi aliyemteua ambaye kwa kofia yake nyingine ni Mwenyekiti wa chama.  Lakini ni mara ngapi katika chaguzi za Chama cha Mapinduzi tumesikia Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM akilalamikia chaguzi hizo kuwa ziligubikwa na rushwa, lakini hatujawahi kusikia kuwa wahusika wa matukio hayo wamekamatwa na TAKUKURU japokuwa ushahidi unakuwepo.
Mheshimiwa Spika,  kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Umasikini  ya mwaka 2011 iliyotolewa  Mei 2012, umma haujaridhika na juhudi zinazofanywa na Serikali katika utendaji mzima wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa  kutokana na sababu kuu kuwa watu wengi  waliokuwa wanahusika na rushwa kubwa  wameachiwa huru.
2.2.2.          Maazimio ya Kongamano la Wadau wa Rushwa
 
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 03.05.2010 kulikuwa na Mkutano wa  kutathmini maazimio ya Kongamano  la Rushwa la  mwaka 2009 ambalo lilihusisha wadau mbalimbali wa kupambana na rushwa nchini wakiwemo kutoka Ofisi ya Bunge na mgeni Rasmi katika kongamano hilo alikuwa Mheshimiwa Samwel Sitta ambaye alikuwa Spika wa wakati huo. Katika kongamano hilo, maazimio zaidi ya 30 ya jinsi ya kukabiliana na kupambana na rushwa katika taifa letu yalipitishwa.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maazimio hayo ni pamoja na azimio namba  (4) ambalo lilikuwa ni kuitaka TAKUKURU kuanzisha gazeti maalum litakalosambazwa mpaka vijijini lenye kuelimisha umma kuhusiana na masuala ya rushwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kulieleza Bunge juu ya hatua iliyofikiwa katika mchakato wa kuanzishwa kwa gazeti hilo.  Aidha, azimio namba 11 lilihusu viongozi kutangaza mali zao pindi wanapokuwa wanaondoka madarakani; utekelezaji wake umefikia hatua gani?

Mheshimiwa Spika, katika azimio namba 15 la Kongamano la Rushwa, TAKUKURU ilitakiwa kuhakikisha kuwa inawekeza zaidi katika fani ya habari za kiuchunguzi (investigative journalism) kwa ajili ya kuwajengea uwezo zaidi wanahabari katika kufichua na kuandika taarifa za rushwa hapa nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua utekelezaji wa azimio hili umefikia wapi na hasa ikizingatiwa kuwa gazeti la Mwanahalisi lililokuwa linaandika habari za kiuchunguzi kuhusiana na rushwa sasa limefungiwa kwa muda usiojulikana.

Mheshimiwa Spika, azimio la 27 la kongamano hilo liliitaka serikali iache mara moja utaratibu wa kuwahamisha watumishi wa umma ambao ama ni wabadhirifu/walarushwa  kama sehemu ya adhabu kutokana na kitendo cha wizi na/au ubadhirifu wa mali ya umma kwenye ofisi za umma na badala yake washughulikiwe kwa mujibu wa sheria za rushwa na za jinai zilizopo katika mfumo wetu wa sheria hapa nchini. Kambi Rasmi  ya Upinzani Bungeni inataka kupata majibu ni hatua gani serikali imefikia katika kutekeleza azimio hili kama kweli tuna nia ya dhati ya kupambana na wabadhirifu wa fedha za umma na walarushwa kwenye Ofisi za umma.


3.      MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA
3.1.    Utaratibu wa Ajira kwa Mkataba kwa Watumishi  waliostaafu
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria za Tanzania, watumishi wa umma hutakiwa kustaafu  kwa hiari wakiwa na umri wa miaka 55, na watimizapo miaka 60 hutakiwa kustaafu kwa lazima. Hata hivyo, baadhi yao wamekuwa wakipewa mikataba ya kuendelea na kazi hata baada ya kutimiza umri wa kustaafu kwa lazima.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haipingi kumwajiri mstaafu kwa mkataba kama mstaafu huyo ndiye pekee mwenye ujuzi na uzoefu wa kazi anayotakiwa kufanya. Ila kuna baadhi ya watumishi waliotimiza umri wa kustaafu kwa lazima, wakapewa mikataba ya kuendelea na utumishi Serikalini, bila kuwa na sifa iliyotajwa. Kambi Rasmi ya Upinzani ilitegemea kwamba, Serikali ingeajiri watumishi wengine kushika nafasi hizo baada ya mikataba hiyo kumaliza muda wake hasa ukizingatia tatizo kubwa la ajira linalowakumba vijana katika nchi yetu. Serikali ya CCM imeendelea kuwaacha wastaafu hao kuendelea na utumishi bila hata kutoa mikataba mipya baada ya ile ya mwanzo kumalizika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaomba iwataje baadhi ya wazee waliotimiza umri wa kustaafu kwa lazima, wakapewa mikataba ya utumishi Serikalini, mikataba hiyo ikamaliza muda wake, lakini bado wanaendelea na kazi:
1.     Ndugu John Tendwa – Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania
Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Ajira wa Msajili wa vyama vya Siasa John Tendwa ulimaliza muda wake tangu Novemba, 2012 lakini bado anaendelea na kazi bila ya mkataba mwingine. Aidha, alipohojiwa na waandishi wa habari juu ya jambo hili alikiri kuwa ni kweli mkataba umeisha lakini sababu za yeye kung’ang’ania ofisi alisema iulizwe mamlaka ya uteuzi wake, yaani Rais. Hata hivyo, Ndugu Tendwa aliwakataza waandishi wa habari kutoa taarifa hii katika vyombo vya habari kwa alichodai kuwa ingeleta mgogoro na malumbano makubwa yasiyo na tija.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haiamini hata kidogo kwamba John Tendwa ndiye mtu pekee mwenye sifa za pekee za kuwa Msajili wa vyama vya Siasa miongoni mwa Watanzania. Hatupendi kusema kuwa ufanisi wake umepungua wala hatupendi pia kusema kwamba kuendelea kwake kubaki ofisini bila hata ya mkataba ni kutokana na kujipendekeza kwake kwa Rais na uhodari wake wa kukipendelea chama tawala na Serikali yake lakini tunapenda kusema  kuwa wapo watu wengine wenye sifa ya kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Ni jambo jema kuwapa wengine uzoefu, na ni jambo jema pia kuzingatia sheria na kanuni zinazoelekeza masuala ya utumishi wa umma.
2.   Mkurugenzi – Manispaa ya Moshi – Bernadeta Kinabo
Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Bernadeta Kinabo, naye alishastaafu kazi, akapewa mkataba kuendelea na kazi na mkataba huo uliisha muda wake tangu mwaka 2011, lakini bado yupo ofisini anaendelea na kazi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe majibu, ni kwa nini Halmashauri na Manispaa ziendeshwe na watumishi wa mkataba wakati kuna watumishi waandamizi katika Halmashauri na Manispaa hizo ambao wangeweza kufanya kazi hizo?

3.2.    Nafasi na Haki za Walimu katika Sekta ya Utumishi wa Umma
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa walimu wamekuwa ni kada ya utumishi wa umma ambayo haitendewi haki na Serikali. Nasema hivi kwa sababu kwa miaka mingi walimu wamekuwa wakilalamika kuhusu mishahara duni, lakini pia baadhi yao (wengi kiasi) wamekuwa hawalipwi stahili zao kwa mfano malimbikizo ya mishahara, fedha za uhamisho, n.k. Mara zote walimu kupitia chama chao wanapolalamika kupata maslahi yao Serikali imekuwa ikiwajibu kwa jeuri kuwa madai yao hayalipiki na pia wanapotangaza mgomo halali kama njia ya kuifanya Serikali iwasikilize, Serikali imekuwa na tabia ya kukimbilia mahakamani kuweka zuio la mgomo huo na hivyo kuwaacha walimu njia-panda bila kujua la kufanya.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya bajeti ya Elimu mwaka 2012/2013, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitoa angalizo kwamba Serikali isiwaburuze walimu wasije wakabaki na kinyongo na kufanya mgomo baridi ambao matokeo yake huwa ni mabaya kuliko mgomo halisi. Serikali hii ya CCM, kama kawaida yake, iliendelea kuziba masikio, na matokeo yake tunaona jinsi ambayo elimu ya nchi hii inavyozidi kuporomoka. Kwa mara ya Kwanza katika historia ya Tanzania, wanafunzi zaidi ya asiliami 60 waliofanya mtihani wa kidato cha nne kidato cha nne 2012 walipata daraja sifuri. Bila shaka mojawapo ya sababu kubwa za anguko hili ni Serikali kupuuza madai ya walimu kama Kambi Rasmi ya Upinzani ilivyodokeza mwaka jana.
Mheshimiwa Spika, hukumu ya mahakama juu ya mgomo wa walimu mwaka jana 2012, ni kwamba Serikali ilitakiwa kukaa na chama cha walimu (CWT) na awepo msuluhishi katika yao (third party) katika kutafuta ufumbuzi wa madai ya walimu dhidi ya Serikali. Kwa kuwa mpaka leo hapajakuwepo na kikao cha usuluhishi kati ya Serikali na Chama cha Walimu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliomba Bunge sasa kama chombo cha uwakilishi lakini pia kama muhimili wa dola unaojitegemea kuwa msuluhihishi kati ya Serikali na Chama cha Walimu ili haki itendeke kwa pande zote mbili.
3.3.    Utaratibu wa Kupima Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma
Mheshimiwa Spika, mwaka 2004 Serikali  ilitoa waraka wa utumishi namba 2 wa mwaka 2004 kuhusu utekelezaji wa utaratibu na kupima utendaji kazi wa watumishi kwa uwazi. Lengo na madhumuni ya waraka huu ni kupima na kuongeza ufanisi kwa watumishi wa umma ili kuleta tija, na hivyo kustawisha maendeleo ya nchi yetu. Zaidi ya hayo, waraka huu unaondoa utaratibu wa zamani wa kupima utendaji kwa watumishi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iliambie Bunge hili na wananchi wa Tanzania kwamba ni mafanikio kiasi gani yamepatikana tangu kuanza kwa utekelezaji wa waraka huu.

4.       MAHUSIANO NA URATIBU
4.1.    Mchakato wa Katiba Mpya na Mapungufu yake
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni, aliyoitoa kwenye mkutano huu wa bunge tarehe 11 Aprili, 2013 ni kwamba kulikuwa na makubaliano kati ya kamati maalum ya CHADEMA na Rais juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, marekebisho yalitakiwa kufanywa kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza ilifanyika katika Bunge la Februari, 2012. Aidha, kwa mujibu wa makubaliano hayo, awamu nyingine mbili za marekebisho ya sheria hiyo ya mabadiliko ya Katiba yalitarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka jana, yaani 2012. Mwaka 2012 ulimalizika kabla ya makubaliano hayo kutimizwa.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake ya kuukaribisha mwaka 2013, Rais Kikwete, alipokuwa akilihutubia taifa kama ulivyo utaratibu wake wa kila mwisho wa mwezi alisema hivi, nanukuu:
“Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Februari, 2012, nilieleza kwamba katika mazungumzo baina ya Serikali na vyama vya siasa na wadau wengine juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulikubaliana tushughulikie marekebisho ya Sheria hiyo hatua kwa hatua. Tulikubaliana kuanza na mambo yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi ili Tume iundwe na ianze kazi. Baada ya hapo tuangalie vipengele vinavyohusu Bunge Maalum na Kura ya Maoni.

Tulifanya hivyo kuhusu Tume ya Katiba na sasa tunajiandaa kuanza mazungumzo kuhusu ngwe iliyobaki yaani, Bunge Maalum na Kura ya Maoni. Kama mazungumzo yatakamilika mapema kunako Januari, 2013 mapendekezo hayo yatafikishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano katika kikao cha Februari kwa uamuzi. Vinginevyo itakuwa katika Bunge la Aprili, 2013.

Ndugu Wananchi;
Kuhusu Kura ya Maoni, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza kuwa Kura ya Maoni itatungiwa Sheria yake maalum. Ni matumaini yangu kuwa matayarisho yake yataanza mapema iwezekanavyo. Nawasihi wananchi wenzangu, viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kijamii tuwe watulivu, tuendelee kushirikiana katika mchakato huu wa Katiba mpaka tulifikishe jahazi ufukweni salama kwa mustakabali mwema wa nchi yetu na watu wake”.
Mheshimiwa Spika, ahadi ya Rais kwamba Serikali ingeleta awamu zote mbili za marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa mwaka 2012 haikutimizwa. Aidha ahadi nyingine aliyotoa Rais wakati akitoa hotuba ya kuukaribisha mwaka 2013 kwamba marekebisho hayo yangefanyika katika mwezi Februari 2013 au Aprili 2013 bado haijatekelezwa na hatuoni dalili ya kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, nataka kuweka kumbukumbu vizuri kwamba, madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya katiba siyo ya kuokoteza. Ni makubaliano halali kati ya wadau mbalimbali kama vile vyama vya siasa, asasi/mashirika n.k. na Rais. Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Rais asimamie ahadi zake, na taifa lina haki ya kujua nini kilitokea mpaka ahadi hizi kushindwa kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, jana tarehe 16.04.2013, Waziri Mkuu, wakati akihitimisha hotuba yake alitoa ahadi kuwa “huenda serikali ikawasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria hiyo kwenye Bunge hili la Aprili kama muda ukipatikana kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza”. Kwa maelezo hayo, ni wazi kuwa Waziri  Mkuu hana hakika na kutekelezeka kwa ahadi ya Rais katika Mkutano wa Bunge wa Kumi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, kwa kutambua kwamba mambo haya yako chini ya Ofisi ya Rais,  tunaitaka serikali itamke mbele ya bunge hili ni lini marekebisho hayo yatafanyika. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inayoongozwa na CHADEMA inarudia tena, kwamba: haitakuwa tayari kuendelea na mchakato wa katiba mpya endapo marekebisho ya sheria hiyo hayatafanyika pamoja na utekelezaji wa mambo ambayo tuliyasema wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu.

4.2.    Tume ya Mipango na Majukumu yake
Mheshimiwa Spika, jukumu kubwa la Tume ya Mipango, pamoja na mambo mengine, ni kuratibu utekelezwaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina mgogoro na utendaji kazi wa tume hii, ila inashangazwa na uundaji wa chombo kingine chini ya Ofisi ya Rais ambacho kimsingi kazi zake zingepaswa kufanywa na Tume ya Mipango.

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu, katika hotuba yake ya bajeti alisema kwamba: “Serikali imeona ni muhimu kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa kuanzisha mfumo imara zaidi wa kupanga vipaumbele, kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo. Mfumo huo ambao utasimamiwa na Chombo maalum (President’s Delivery Bureau) chini ya ofisi ya Rais, Ikulu, unazingatia uzoefu wa nchi ya Malaysia”.

Mheshimiwa Spika,
 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inatambua kwamba  Serikali imeuchukua mpango huu kutoka Malaysia,  kutokana na mkutano wa kimataifa wa 'Langkwi' uliofanyika mwezi Juni 2011 ambao Rais Jakaya Kikwete alishiriki kwenye “mkutano wa tafakuri” 'Putrajaya' ambapo Waziri Mkuu wa Malaysia Mhe. Dato' Razak aliuelezea mpango huu kuwa ulileta mabadiliko ya kiuchumi katika nchi yake. Katika mkutano huo wa tafakuri, Waziri Mkuu wa Malysia alisema kwamba mafanikio ya mpango huo ulitokana na misingi ifuatayo:
                               i.            Uongozi shupavu na ulio tayari kwa mabadiliko ya kuipeleka nchi mbele.
                             ii.             Kuweka mipango ya kimaendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa
                          iii.            Nidhamu katika utendaji na utekelezaji
                           iv.             Uwajibikaji wa serikali na kuwa tayari kukiri madhaifu yake.
Mheshimiwa Spika, mpango huu wa kuanzishwa kwa idara hii ambayo inajitegemea kwenye Ofisi ya Rais tayari umeshaanzishwa kama alivyokiri Waziri Mkuu katika hotuba yake na kwamba   Rais tayari ameshazindua  awamu ya kwanza ya maabara tangu tarehe 22.02.2013, na vipaumbele  ambavyo vimepitishwa ni sita kama ifuatavyo: Nishati, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji na Ukusanyaji wa Mapato.

Aidha, kwa mwaka huu wa fedha mpango huo umeweka bayana kuwa kwa upande wa Nishati lengo ni kuongeza uzalishaji wa nishati kutoka Megawati 1,438 hadi kufikia Megawati 2,780. Katika usafirishaji kipaumbele ni kufungua korido ya kati kwa kufikia uwezo wa kusafirisha tani milioni 5 ifikapo 2015 na hatimaye tani milioni 8 ifikapo mwaka 2025. Kwa upande wa elimu kipaumbele ni kuboresha elimu ya msingi na sekondari na kuhakikisha kuwa kiwango cha ufaulu kinafikia asilimia 70. Kwenye  kilimo mkakati  kipaumbele ni kufungua mashamba ya kibiashara wakati  upande wa maji ni kuhakikisha kuwa asilimia 67 ya Watanzania wanapata maji safi na salama. Kwa upande wa ukusanyaji wa mapato, lengo ni kuhakikisha kuwa tunaongeza mapato kwa kiwango cha asilimia 50.

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari  imeshatenga fedha kwenye bajeti ya mwaka huu wa 2013/2014 kiasi cha shilingi bilioni 8 na imeomba fedha kutoka kwa wafadhili wa nje kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kitengo hiki kipya chini ya Ofisi ya Rais Ikulu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kutoa majibu kwa Watanzania juu ya mambo yafuatayo:
                                                i.            Je, vipaumbele vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano uliopitishwa na Bunge hili mwaka 2011 ndio vimeachwa au vitatekelezwa sambamba na vipaumbele hivi vipya?
                                              ii.            Je, Kwa nini Serikali imeanzisha kitengo kipya cha Performance Management and Delivery Unit (PEMANDU) (Kitengo cha Usimamizi na Ufanisi wa Utendaji) chini ya Ofisi ya Rais wakati kuna Tume ya Mipango ambayo kimsingi ndiyo yenye wajibu wa kusimamia vipaumbele vya Taifa na Mpango mzima wa Maendeleo wa Taifa?
                                           iii.            Je, ikitokea tena, Rais akakaribishwa kwenye “mkutano mwingine wa tafakuri” kama uliofanywa na kiongozi wa Malaysia, na kukuta mipango mizuri zaidi, Serikali italazimika tena kupanga upya vipaumbele vya Taifa na Mpango wa utekelezaji kama inavyofanya sasa?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, ni mdau mkubwa wa maendeleo na inauheshimu mpango wa Taifa wa Maendeleo lakini namna Serikali inavyotekeleza Mpango huo hatuna hakika kama malengo ya Mpango huu yatafikiwa. Kambi Rasmi ya Upinzani haioni sababu yoyote ya msingi ya kuanzisha kitengo kipya cha usimamizi wa mpango wa maendeleo wakati Tume ya Mipango ipo. Kinachoonekana dhahiri ni kwamba Serikali hii ya CCM kila kukicha inatafuta mbinu mbalimbali za kutumia fedha za walipa kodi wa Tanzania bila kujali sana matatizo ya Watanzania. Nasema hivi kwa sababu kitengo hiki kipya kilichoanzishwa bila sababu ya msingi, hivi punde kitaanza nacho kuomba mabilioni ya fedha kwa ajili ya uendeshaji wake wakati tayari kuna Tume ya Mipango ambayo ndio mratibu na msimamizi wa Mpango wa Maendeleo.
4.3.    MAHUSIANO YA MADHEHEBU YA DINI NA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, Kiongozi wa Kambi Rasmi Bungeni alieleza vizuri tatizo la udini katika hotuba yake aliyoitoa hapa Bungeni tarehe 11 Aprili, 2013. Hapa itatosha tu kusema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo matukio ambayo yanaashiria udini. Baadhi ya matukio hayo ni:
·        Kushambuliwa kwa viongozi wa dini, na wengine kuuawa
·        Kuchomwa moto nyumba za ibada
·        Mgogoro wa nani achinje
Yapo matukio mengine; na haya yote yamesababisha taharuki, vilio, na utovu wa amani na usalama miongoni mwa wananchi walioguswa na matukio haya.
Mheshimiwa Spika, wakati watu wakizidi kuathirika na matukio yanayoashiria udini, serikali haijachukua hatua kali kukomesha matukio hayo.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali kushindwa kukemea au kusuluhisha kwa haraka migogoro wa kiimani uliotokea hapa nchini, umesababisha kutolewa kwa matamko makali na madhehebu ya dini ambayo kimsingi yanaonesha jinsi mahusiano kati ya Serikali na taasisi za dini yanavyozidi kudorora.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa kati ya migogoro yote ya kijamii hakuna mgogoro mkubwa na tete kama ule wa kiimani, kwani mgogoro huo hauna itikadi za kisiasa na kwa maana hiyo athari zitakazotokana na mgogoro wa kidini unaathiri jamii nzima. Ni jukumu la Serikali kuwaeleza Watanzania ni hatua gani za maksudi zinachukuliwa katika kutatua mgogoro huo unaoelekea kusambaratisha amani na mshikamano wa Taifa letu?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali yetu na vyombo vyake vya usalama, sheria na amani kuchukua hatua mara moja bila kuchelewa dhidi ya watu au vikundi vyovyote vinapoanza uchochezi wa kidini. Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea pasipo hatua madhubuti kuchukuliwa ni udhaifu mkubwa wa uongozi na uwajibikaji wa Serikali ambayo jukumu lake la kwanza ni kulinda usalama wa nchi na watu wake.

5.       MASUALA MENGINE
5.1.    Utawala Bora Ngazi za Halimashauri, Kata na Vijiji
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa dhana ya utawala bora imekuwa ikionekana kuwa inapaswa kutekelezwa kwenye ngazi ya serikali kuu. Katika ngazi ya serikali za mitaa utawala bora kwa jumla umeachwa bila kuwekewa msisistizo. Ni muhimu serikali ihakikishe kuwa utawala bora unakuwa ni sehemu ya utendaji wa kila siku kwenye ngazi zote – kitongoji, kijiji, kata, wilaya na mkoa. Ni muhimu Serikali ihakikishe kuwa waliopewa wajibu wa kusimamia hilo wanatimiza wajibu wao kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, hali ya utawala bora imezorota sana kwenye ngazi ya serikali za mitaa, na hasa ikizingatiwa kuwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa mbalimbali nchini wamekuwa na  utamaduni wa kuingilia maamuzi mbalimbali yanayofanywa na vikao halali vya Halimashauri za Manispaa na Wilaya.  Sasa hivi Wakuu wa Wilaya na Mikoa  wamekuwa wakiingilia na hata kushurutisha maamuzi mbalimbali  na hivyo kukwamisha utekelezaji wa maamuzi yanayofanywa na vikao hivyo na kuathiri utendaji kazi wa Halimashauri hizo.
Mheshimiwa Spika, tabia ya kutokuheshimu utawala bora kwenye ngazi ya Halimashauri umekua na kusambaa mpaka kwenye ngazi za Kata na Vijiji kwani sasa watendaji wa vijiji na Kata wamejigeuza na kuwa wao ni Polisi, Mahakama na Magereza. Viongozi hawa wamekuwa  wakiwanyanyasa sana wananchi kwa kuwakamata, kuwahukumu na hata kuanzisha magereza kama ambavyo wengi wanavyoweza kushuhudia kuwa yapo baadhi ya maghala ya mazao ambayo sasa yamekuwa ndio mahabusu kwa wananchi wa vijijini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa majibu ya kina kuhusiana na suala la utawala bora kwenye ngazi za Halimashauri, kata na vijiji. Ni hatua gani Serikali imewachukulia viongozi wa Halmashauri, Kata na Vijiji wanaowanyanyasa wananchi kutokana na itikadi zao za siasa na sababu nyingine? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza: Wananchi wachukue hatua gani ili kuukomesha uonevu wa aina hiyo pindi unapotokea ?

5.2.    Ukosefu wa Ajira na Ongezeko la Umasikini kwa Wananchi
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa jarida la “The African Executive” toleo Na. 415 la tarehe 3-10 Aprili, 2013, ni kwamba: tatizo kubwa kabisa la binadamu kwa siku hizi ni umasikini. Ili kuondokana na umasikini huo, hitaji la msingi kabisa ni kupata kipato kizuri ambacho chanzo chake  kikubwa ni ajira. Kwa hiyo njia madhubuti ya kupambana na kutokomeza umasikini ni kutengeneza nafasi nyingi za ajira iwezekanavyo na kuwapatia watu ujuzi na utaalamu ili kujaza nafasi hizo.
Mheshimiwa Spika, jarida hilo linaelezea pia kwamba, kutengeneza nafasi za ajira bila kuwajengea wananchi ujuzi na utaalamu wa kufanya kazi hizo ni kazi bure kwa kuwa kazi hizo zitafanywa na wataalam kutoka nje na hivyo kutowanufaisha wananchi wetu. Kwa hiyo kama Serikali inawapa watu wake elimu bora na kuwajengea watu wake ujuzi na utaalamu na  kama Serikali inaweka mazingira mazuri ambayo watu wanaweza kufanya biashara na kupata fedha, basi watu hao watajinufaisha wenyewe, watawanufaisha wengine na wanaweza kuisaidia Serikali kuondokana na umasikini. Hivyo uwezo wa watu kupata ajira na kipato unategemea sana jitihada za Serikali.
Mheshimiwa Spika, tatizo la ukosefu wa ajira hapa nchini linazidi kuwa kubwa na Serikali ya CCM imeshindwa kabisa kutatua tatizo hili. Tangu mwaka 2005 Rais kikwete aliwaahidi Watanzania Maisha Bora kupitia kaulimbiu yake ya “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania”.  Hiki ni kipindi cha pili cha utawala wake na maisha ya Mtanzania yanazidi kusinyaa, umasikini unazidi kuongezeka, na tatizo la ajira linazidi kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, pamoja Serikali hii ya CCM kushindwa kutoa ajira za kutosha tofauti na ilivyoahidi bado imekuwa ikiwakejeli wananchi kuwa eti hata kufungua visoda ni kazi.
5.3          Kufukuzwa Kazi kwa Kuonewa
Mheshimiwa Spika, baadhi ya waajiri wa serikali wamekuwa wakinyanyasa na kuwanyanyapaa watumishi wa umma kutokana na itikadi za kisiasa. Unyanyapaa huu umechukua sura mpya kiasi ambacho mtumishi anapotoa mawazo mazuri ambayo ni ya kukosoa mfumo wa uendeshaji wa taasisi ya umma ili ufanye kazi vizuri zaidi anaitwa kuwa ni pandikizi la CHADEMA. Jambo hili linawavunja moyo watumishi wa umma kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuogopa kuitwa ni wapinzani na matokeo yake utendaji katika sekta ya umma unazidi kudorora.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kusikitisha, Ndugu Emmanuel V. Gwalanje, ambaye ni Afisa Mifugo Msaidizi daraja la II katika Halmashauri ya Mufindi, alifukuzwa kazi kwa  mashtaka dhidi yake kwamba anajihusisha na masuala ya siasa wakati wa kazi. Katika utetezi wake, Emmanuel V. Gwalanje alieleza bayana kuwa hajawahi kujihusisha na mambo ya siasa akiwa kazini na wafanyakazi wenzake ni mashahidi; pia rekodi yake ya mahudhurio kazini ni nzuri lakini amesingiziwa hivyo kwa kuwa alihudhuria mkutano wa siasa baada ya saa za kazi.
Mheshimiwa Spika, mchakato wa kumfukuza Ndugu Emmanuel V. Gwalanje ulikuwa mfupi sana. Notisi ya Mashitaka iliandikwa tarehe 18.03.2013, utetezi uliwasilishwa tarehe 21.03.2013, barua ya kufukuzwa kazi tarehe ilitoka tarehe 28.03.2013. Kambi Rasmi ya Upinzani inashawishika kuamini kwamba uamuzi wa kumfukuza kazi Emanuel Gwalanje haukuwa wa haki ikizingatiwa kwamba hakuwahi kupewa onyo hata moja kama kweli alikuwa akijihusisha na kazi ya siasa wakati wa kazi. Aidha, muda mfupi wa mchakato wa kufukuzwa kwake unatia shaka kama kuna uchunguzi wa kina uliofanyika  kubaini bila shaka yoyote kuwa Emmanuel Gwalanje kweli alihusika na kazi ya siasa wakati wa saa za kazi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inamtaka Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mufindi, E. Kaduma, pamoja na Afisa wake wa Mamlaka ya Nidhamu kuwasilisha mchakato na hukumu ya mashitaka dhidi ya Emmanuel Gwalanje kwa Waziri wa Utumishi wa Umma ili kubaini uhalali wa mchakato mzima.
Mheshimiwa Spika, nimetolea mfano shauri la Emmanuel Gwalanje wa halmashauri ya Mufindi, lakini yapo matukio mengi ya watumishi wanaofukuzwa kazi kiholela katika halmashauri na taasisi za Serikali kutokana na chuki binafsi na unyanyapaa wa kisiasa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kukemea tabia hii.


5.4          Huduma kwa Watumishi wa Umma wanaoishi na VVU
Mheshimiwa  Spika, mwaka 2006 Serikali  ilitoa Waraka wa utumishi wa umma namba 2 wa mwaka 2006 kuhusu huduma za watumishi wa umma wanaoishi na virusi vya ukimwi. Chini ya waraka huu waajiri wa watumishi wa umma wanapaswa kuhamasisha watumishi kupima VVU, na kutoa huduma muhimu kwa wale watakaokuwa wameathirika. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe taarifa katika bunge hili kuwa ni kwa  kiwango gani waraka huu umetekelezwa na  ni gharama kiasi gani imetumika mpaka sasa katika kuwahudumia watumishi wa umma wanaoishi na VVU kwa maana ya lishe broa, madawa, nauli za kuhudhuria matibabu na stahili nyingine?




________________________________________________
PROF. KULIKOYELA KANALWANDA KAHIGI (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
OFISI YA RAIS -
MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA, UTAWALA BORA NA
MAHUSIANO NA URATIBU
17 APRILI, 2013



No comments:

Post a Comment