Pages

Pages

Sunday, April 28, 2013

Extra Bongo kukamua Garden Breeze leo

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BENDI ya Extra Bongo, leo inafanya shoo ya aina yake katika viwanja vya Garden Breeze Magomeni, jijini Dar es Salaam, huku ikiwa na mipango kabambe ya kuteka nyoyo za wapenzi wao.
         Wacheza shoo wa Extra Bongo
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki alisema kuwa shoo yao itakuwa ya aina yake kutokana na mipango kabambe wanayoendelea kuifanya.

Alisema kwa sasa kiu yao ni kuhakikisha kuwa mashabiki wao wanapata kazi ya aina yake, hivyo wadau na mashabiki wa muziki waende kwa wingi kuangalia vitu vyao.

“Extra Bongo imesheheni wakali kila upande, wakiwamo waimbaji, marepa pamoja na wacheza shoo ambao kwa hakika dhamira yao kubwa ni kuona wadau wao wanaburudika.

“Tunaomba waje kwa wingi katika shoo yetu ya Garden Breeze kwa ajili ya kuangalia namna gani tupo imara katika tasnia ya muziki wa kizazi cha dansi hapa nchini,” alisema Choki.

Safu ya ucheza shoo ya Extra Bongo inaongozwa na Super Nyamwela, wakati waimbaji wanaofanya vyema katika bendi hiyo ni Banza Stone, Khadija Kimobiteli, Athanas, Rogati Hega Katapila, Choki na wengineo wanaotesa katika ramani ya muziki wa dansi.

No comments:

Post a Comment