Pages

Pages

Sunday, April 28, 2013

Baada ya kutwaa Ubingwa wa Bara, Yanga sasa waidhalilisha Simba


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema hauwezi kuifikiria mechi yao dhidi ya Simba, badala yake nguvu zao zote wamezielekeza kwa timu ya Coastal Union ya Tanga, mechi itakayopigwa Mei Mosi, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto

Maneno ya Yanga yanatafsiriwa kama tusi kwa Simba iliyoonekana dhaifu katika mzunguuko wa pili na kushindwa kutetea ubingwa wao ulionyakuliwa na Jangwani wakiwa na mechi mbili mkononi.

Mechi ya Yanga imepangwa kufanyika Mei Mosi, wakati ile ya Simba watacheza Mei 18 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, ambapo pia itakuwa ni hitimisho ya patashika ya Ligi ya Tanzania.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa mechi yao na Simba ni ya kawaida kama ilivyokuwa ya Coastal Union, hivyo wameiweka kwanza pembeni.

“Tunakutana na Coastal kwanza kabla ya Simba, hivyo sioni kama akili zetu, nguvu zetu zitakuwa huko, maana tumeshakuwa mabingwa hivyo mechi zote zilizosalia zina hadhi sawa.

“Naamini tutakapofanikiwa kuifunga Coastal Union akili zetu zitahamia kwa Simba, ukizingatia kuwa timu yetu ni nzuri na ina uchungu wa kumaliza ligi vizuri, hivyo hili naamini tutafanikisha,” alisema Kizuguto.

Yanga imefanikiwa kutwaa ubingwa msimu huu na kupeleka shangwe na nderemo kwa wapenzi wao, huku mechi mbili zilizosalia zikibaki kama kukamilisha ratiba tu.

No comments:

Post a Comment