Pages

Pages

Monday, April 15, 2013

Baada ya kumfungia mmoja, DRFA yapiga mkwara mzito



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimesema kitaendelea kuwa wakali na kuwafungia kwa wale wasiokuwa na vitendo vya kiungwana, vikiwapo kusaini zaidi ya timu moja, kama alivyofanya Sued Lucas wa Boom FC na kufungiwa kwa mwaka mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kusaini timu zaidi ya moja.
Msemaji wa DRFA Mohamed Mharizo
Mchezaji huyo licha ya kufungiwa, klabu yake ya Boom FC, imetozwa faini ya Sh 200,000.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, Kamati ya Rufaa ya DRFA, iliyokutana Aprili 11 mwaka huu, chini ya Mwenyekiti wake, Salehe Njaa, kupitia Kanuni ya 50 (a) imemfungia mchezaji huyo na kuyaacha kama yalivyo matokeo ya mechi zote alizocheza.
 

“Mchezaji huyo alisaini Boom FC kwa kutumia jina la Sued Lucas, wakati huo huo akasaini timu ya Kumbukumbu kwa jina la Issa Rashid Mwamlima.
 

“Hivyo Kamati ya Rufaa imeirudishia Boom FC pointi zake tatu na mabao 2-0, waliyoupata katika mechi yao dhidi ya Kumbukumbu, iliyochezwa Aprili Mosi mwaka huu, uwanja wa Msasani.
 

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kumbukumbu kumwekea pingamizi mchezaji huyo dhidi ya Boom,” alisema Mharizo.

Alisema DRFA inapenda kusisisitiza uadilifu kwa wachezaji na kuheshimu Kanuni na taratibu zilizowekwa, kwa maslahi na maendeleo ya mpira wa miguu.

Kutokana na hatua hiyo, Ligi Daraja la Pili hatua ya sita bora, iliyokuwa ianze Aprili 9, ilisitishwa na sasa itaanza leo kwa mechi tatu.

Boom FC watacheza dhidi ya Shariff Star uwanja wa Airwing, Abajalo dhidi ya Red Coast, uwanja wa Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere na Friends Rangers watachuana na Day Break, uwanja wa Kinesi.

No comments:

Post a Comment