Pages

Pages

Monday, March 04, 2013

VIDA: Nyota nyingine inayoibukia THT


 Vida akiwa amesimama kwa kufotolewa picha....

Vida, akisisitiza jambo kwa Handeni Kwetu Blog.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIPATA nafasi ya kusikiliza wimbo wa 'Baba Awena', hakika utasuuzika nyoyo yako kwa kiasi kikubwa mno, maana umeimbwa kwa hisia na mtazamo wa aina yake katika ulimwengu wa nyimbo za mapenzi, hapa nchini.

Msanii Vida kutoka THT, akizungumza na mwandishi wa habari mwandamizi, Arodia Peter, wiki iliyopita.

Wimbo huo wa aina yake umeimbwa na mwanadada anayeibukia katika taasisi yenye jina la kutisha, Tanzania House of Talent (THT), Pili Juma, anayejulikana kwa jina la Vida.
Vida umeniona?
 
Ni wimbo mzuri na wenye ujumbe wa aina yake, huku akishirikiana na msanii mwingine wa THT, Linex, anayejulikana pia kwa kutunga nyimbo zenye mashairi ya hadithi za kusisimua.
Vida, akiwa kwenye pozi...

Pamoja na mambo mengine yanayoufanya wimbo huo kuwa juu katika vituo vya redio, bali pia wimbo huo ni ishara kuwa nyota nyingine imeibukia katika taasisi hiyo ya THT na kufuata nyayo za wakali wengine, kama vile Mwasiti, Vumilia, Linah na Recho ambao wote wamefanikiwa kupata majina makubwa kisanaa.

Ni hodari haswa, huku akiimba kwa kiwango cha juu pamoja na umakini wake anapokuwa katika kazi hiyo ya sanaa. Katika mazungumzo yaliyofanyika mapema wiki hii, Vida anasema kuwa anafanya juhudi kubwa pamoja na kumuomba Mungu kazi zake zikubaliwe na mashabiki.

Anasema kuwa kutokea katika taasisi yenye mguso na majina ya wasanii wengi wenye mipango kabambe ya kuwapatia mafanikio, kunamfanya aongeze kasi na aina ya utendaji wake wa kazi chini ya jopo la wataalamu wa muziki katika taasisi hiyo.

"Ukiona msanii hapa ndani ya THT anatoka, ujuwe ameshapikwa na kuiva vizuri, ndio maana wengi hulazimika kusubiri kwanza utaratibu uliowekwa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wasanii waliopo wanafikia malengo yao.

"Naamini katika hilo, ukweli utajulikana kuwa nahitaji kufikia malengo kama wenzangu waliotangulia hapa THT, huku nikishukuru kwa kiasi kikubwa jinsi ninavyolelewa na kutolewa tangu chini hadi hapa nilipokuwa sasa,” alisema Vida.

Mwanadada huyo anasema kuwa sanaa ni kitu anachopenda katika maisha yake, ndio  maana hata wazazi wake hawajaweza kumtilia kauzibe walipogundua kuwa anapenda kuwa msanii, huku akianzia na sanaa ya uchezaji shoo.

Anasema alipokuwa na miaka 16 tangu kuzaliwa kwake, alianza kujiwekea mikakati ya kuwika kisanaa kwa kuanzia na sanaa ya uchekeshaji. Mwanadada huyo anasema kuwa aliamua kujipeleka THT kwa sababu ndio sehemu maalum ya kukuza na kulea vipaji.

“Nilipokwenda THT, nashukuru nilipokelewa vyema kama mcheza shoo, lakini sikudumu sana, maana wakati huo bado nilikuwa nasoma, hivyo sikuweza kufanya kazi kwa moyo na muda zaidi, nilikuwa naenda na kuondoka.

“Hata hivyo, baada ya miaka mitatu, nilirudi tena na kufanyiwa usaili ambapo nilipita moja kwa moja kama mwimbaji badala ya densa kama nilivyokwenda mwanzo, maana wakati huo vipaji vyangu vilizidi kujionyesha kwa kasi ya ajabu,” alisema Vida.

Msanii huyo anayevutiwa kwa kiasi kikubwa na muziki wa Ali Kiba, anasema kuwa mpaka sasa ameshakamilisha nyimbo tano zinazoweza kuwapo kwenye albamu yake ya kwanza itakayokamilika hibi karibuni, kadri ya mashabiki watakavyoendelea kumpokea.

Nyimbo hizo ni pamoja na Malingo, Nahisi, Umenikumbuka, Rafiki na Baba Awena ambao umezidi kufanya vyema katika vituo vya redio; huku makali yake yakizidi kuimarika kwa kiasi kikubwa katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva.

Vida anasema kuwa matarajio yake ni kuwa msanii mkubwa kwa kuhakikisha kuwa anafuata ushauri wa wadau wake, wakiwamo wataalamu wa muziki waliokuwapo katika taasisi ya THT yenye kutoa wasanii bora na wenye makali ya kutisha.

Wasanii ambao wanafanya vyema na wametokea katika taasisi hiyo ni pamoja na Linah, Mwasiti, Barnabas, Mataruma, Dito, Kwea Pipa, Amini, Recho pamoja na makundi zaidi ya matatu ambayo nayo yapo ndani ya taasisi hiyo.

Msanii huyo anasema kuwa wasanii wote waliokuwapo katika taasisi hiyo ni wakali na wanaweza kufanya vyema zaidi katika muziki wa kizazi kipya. Kilichopo hapo ni utaratibu na namna inavyowekwa mipango ya kuwatoa kwa mpango.

“Naomba kuwataka wadau na mashabiki wangu wakae mkao wa kula, maana nimejipanga kwa kiasi kikubwa kuona kuwa mwaka huu nakuwa imara na mwenye mafanikio makubwa zaidi, nikiwa chini ya taasisi ya THT.

“Naamini kwa kushirikiana kwa pamoja na wasanii wenzangu, malengo yatatimia, ukizingatia kwamba najifunza kwa kupitia wenzangu waliotangulia, huku nikiomba dua njema kwa wazazi wangu, ukizingatia kuwa tangu zamani walinipa moyo,” alisema Vida.

Mwanadada huyo anasema kuwa mbali na kuwa na kipaji cha uimbaji na uchezaji, lakini pia anahusudu mambo ya urembo, hasa katika tasnia ya uanamitindo, ikiwa ni kazi ambayo ina nafasi katika maisha yake leo au siku za usoni.

Vida ni mzaliwa wa mkoani Morogoro, katika wilaya Kirombelo, huku sanaa yake ikionekana kama amerithi kwa mama yake, ambaye naye anafanya sanaa ya maigizo, akicheza filamu kadhaa, ikiwamo ile ya Pigo.

Kwa sasa msanii huyo anaishi Mbagala, huku akiwa na imani kuwa Mungu ataendelea kumuongoza na kumbariki uwezo wa juu katika maisha ya sanaa duniani.

Mwanadada huyo anasema kuwa serikali inatakiwa kufanyia kazi changamoto zinazoyumbisha maisha ya wasanii, maana wote wanategemea sanaa kama sehemu za ajira zao, hivyo ukimya huo unaweza kuwa sumu kwa nguvu kazi ya Taifa.

Msanii huyo alizaliwa mwaka 1994, huku elimu yake ya msingi akiipata katika shule ya Annex iliyopo Mbagala, jijini Dar es Salaam alipoanza mwaka 2002 na kumaliza mwaka 2008.

Kutokana na matatizo ya kiafya yaliyodumu kwa muda mrefu, mwanadada huyo alilazimika kukomea elimu ya kidato cha pili, huku akiwa na mikakati ya kuendelea na shule mara baada ya kuweka mambp yake sawa.

Vida mwimbaji wa Baba Awena, anamaliza kwa kuwataka wasanii waendelee kuongeza bidii katika maisha yao, ikiwa ni njia ya kutangaza muziki na sanaa kwa ujumla, ingawa kumekuwa na changamoto za aina yake kwenye tasnia hiyo.

 

No comments:

Post a Comment