Pages

Pages

Monday, March 18, 2013

TFF hawajui kuwa Watanzania leo hii ni wajuzi wa mambo?

 Rais wa TFF, Leodgar Tenga kulia akiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho hilo, Sunday Kayuni.
 
SIWEZI KUVUMILIA

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SASA nimeamini kuwa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodgar Tenga, hana washauri. Na kama anashauriwa, basi wanamdanganya katika baadhi ya uamuzi unaoleta utata katika Shirikisho hilo.

Kwanini nasema hivyo? Kwa mtu makini, ambaye anajua fika kuwa kila atakaloamua kwa maslahi ya Tanzania, basi kitachunguzwa kwa kupimwa na wenye akili na wasiokuwa na akili pia.

Katika hilo, nilifikiri kuwa kila jambo linalofanywa sasa, lazima lipimwe na kuwekwa sawa kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu. Hakika siwezi kuvumilia. Nimeshindwa baada ya kuona Tenga akiwadanganya Watanzania, kuwa eti Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (FIFA), wametoa tishio la kuifungia Tanzania.

Sawa FIFA wanaweza kutufungia kwa sababu ya makosa yetu ya kizembe yaliyofanywa au yanayoendelea kufanywa, hasa pale wanapokataa kuwa masuala ya mpira wa miguu yasifanywe na serikali.

Hadi sasa, ni kama vile tunastahili kufungiwa. Amri na kanuni za serikali kuwa mbali na maamuzi ya soka, imevunjwa hasa pale Waziri wa Habari, Vijana, Uramduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuwaagiza TFF watumie Katiba ya mwaka 2006 na kuiacha ile ya mwaka 2012.

Mbali na Katiba hiyo, kikao kilichofuata kati ya serikali na TFF, pia waliamuliwa waitishe Mkutano Mkuu na kufanya Uchaguzi, baada ya ule waliopanga kufanya awali, kuvunjwa kwa sababu za kupingana kikanuni.

Pamoja na hayo yote, lakini nimeshangazwa na jambo moja kubwa. Hivi hawa FIFA, kwanini watangaze kuifungia Tanzania kwa kupitia magazeti?

Hivi kweli chombo kama FIFA kinachoaminika duniani, kinaweza kukaa na kujadili yalioandikwa kwenye magazeti?
 
Wakati nawaza haya, nakumbuka kuwa siku tatu kabla ya Tenga hajazungumza hayo, alikuwa kwenye mkutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ambao huko alikutana pia na watendaji wa FIFA, sasa kwanini wasingempa ujumbe huo hadi watume kwa barua.
 
Kiukweli kabisa, nina hofu na utendaji wa TFF pamoja na malengo yao, hasa kwa kuamua kuwadanganya Watanzania. Huu ni uongo wa aina yake.
 
Kwa mujibu wa TFF, eti ujumbe huo umetumwa unaoleza kuwa itaifungia Tanzania kama serikali yake itakuwa inaingilia mambo ya michezo, huku ujumbe huo ukitumwa na Jerome Valke, ambaye ni Katibu Mkuu wa chombo hicho kikubwa duniani kwa sekta ya mpira wa miguu.

Sawa, lakini hapa wakubwa wamejaribu kukimbia kivuli. TFF inapaswa kujua kuwa hata kama FIFA itaifungia nchi, lakini si jambo la busara kujaribu kuifanya serikali yetu haina meno kwa yale inayokusudia kuyafanya.

Kila mtu anajua kuwa Watanzania hatuna maendeleo katika sekta ya michezo, hivyo ili tufike tunapohitaji, hatuhitaji ubabaishaji wa aina yoyote. Viongozi wanaofanya ‘madudu’ wasichekewe.

Ndio inauma,  hasa kama TFF itafungiwa na FIFA, lakini hata wao wanapaswa kuambiwa kuwa TFF ipo chini ya serikali japo inajiendesha yenyewe bila kutegemea chochote kutoka serikalini.

Na ndio maana tuna Waziri wa Michezo. Kama uamuzi wa serikali hauwezi kuheshimiwa, basi sheria zetu zitakuwa na matege. Huo ndio ukweli wa mambo na hapana shaka unapaswa kufuatwa.

Tenga na jopo lake anapaswa kujua kuwa alichokisema, kila mtu anajua kuwa sio kweli, zaidi ya kukaa na watu wake kupanga la kuwadanganya watu ili waone kuna umuhimu wa kuwafuata wanachosema.

Wakati mwingine nafika mbali zaidi kwa kuwaza; labda ni bora tufungiwe ili tujipange, maana hata hapa hatujafungiwa hatuna maendeleo kwasababu ya wachache wao kutokuwa na dhamira ya kweli.

Nayasema haya kwa uchungu, maana siwezi kuvumilia kuona kuwa kumbe mtu anaweza kukaa na kujipangia mambo kwa faida yake. Hii sio njia nzuri kwa ajili ya kukuza sekta ya michezo.

Ni wazi katika haya yanaoendelea sasa, mgogoro huu utaendelea kushika kasi, maana wachache wao hawataki kufuata maagizo ya serikali kwa kufanya vikao na marafiki zao, kasha wakaandika barua za kuwapiga mkwara serikali ili kesho ionekene si lolote katika Taifa hili.

Hapana. Na katika hili, ni bora wadau na viongozi wa michezo kuwaambia FIFA, kuwa kwenye masuala ya ndani watuachie wenyewe. Hata kama wakiamua kutufungia, lakini itakuwa njia ya kujiandaa, kujiweka sawa katika kipindi cha miaka ambayo watafungia.

Bila hivyo hatuwezi kufika pale tunapohitaji, maana wapo watu wanaofanya mambo ama kwa bahati mbaya au wanafanya makusudi kwa faida wanayojua wenyewe, jambo ambalo hatuwezi kukubaliana nalo.

Hakika katika hili, kamwe siwezi kuvumilia na iwe tiba kwa wale wanaona kuwa Watanzania sasa ni majuha, eti hatujui lolote katika ulimwengu huu.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment