Pages

Pages

Wednesday, March 13, 2013

Lambalamba waiweka mtegoni CCM wilayani Handeni



Mwenyekiti wa CCM Handeni, Athumani Malunda
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kipo kwenye wakati mgumu kutokana na makundi ya vijana kutaka kurudisha fomu baada ya kuwekewa ngumu katika mahitaji yao, yakiwamo ya kutaka kuita waganga wa kienyeji, maarufu kama lambalamba kwa ajili ya kutoa uchawi.


Sakata hilo linawasumbua viongozi na watendaji wa CCM katika wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, hasa kutokana na ushawishi wa watu wanaotaka kurahisisha shughuli hizo za kutoa uchawi.

Habari kutoka katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya Handeni, zinasema kuwa sehemu nyingi za wilaya hiyo, kumekuwa na kelele za wananchi kutaka kuitisha waganga kwa kufanya kazi katika maeneo yao.

Watu wengi waliozungumza na Handeni Kwetu, walisema kuwa kama serikali itaendelea kukataa kwa kile wanachokitaka, basi watarudisha kadi za CCM na kuviunga mkono vyama vingine.

"Sisi kwenye eneo letu tupo wananchi zaidi ya 300 ambao tunaamini ni wanachama hai wa CCM kwa namna moja ama nyingine, bila kuingiza wale wasiokuwa wanachama lakini tunaimba wimbo mmoja.

"Kwanini serikali ikatae kila kitu, kwani pesa wanatoa wao? Kuhusu vurugu, sisi tunataka kufanya mambo yetu kistaarabu kwa kuimalisha ulinzi sisi wenyewe, inashangaza kwanini serikali inashindwa kukubali mawazo yetu,” alisema mmoja wa wananchi ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa CCM, wilayani Handeni, Athumani Malunda, alisema kuwa serikali haiamini ushirikina kama isivyoamini dini za wananchi wake.
Ni kweli kuwa maeneo mengi ya wilaya ya Handeni yanasumbuliwa na mambo hayo, hasa kutokana na wananchi wengi kutaka kuitisha watu wa kutoa uchawi, kadri ya vile wanavyoamini.
Katika suala hili kuna utaratibu wake, hivyo nafikiri watendaji wa serikali, akiwamo Mkuu wa Wulaya ya Handeni analifanyia kazi suala hili kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa mazuri,” alisema Malunda.
Mbali na Handeni, lakini pia wilaya ya Korogwe inatafunwa na suala hilo, huku pia maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam kukutana na zogo hilo la wananchi kuita watu wenye kutoa uchawi.

No comments:

Post a Comment