Pages

Pages

Friday, February 01, 2013

Uchaguzi Mkuu TFF:Kamati ya Uchaguzi yaondoa pingamizi zote

Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais, Michael Wambura

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imetupilia mbali pingamizi zote zilizowekwa dhidi waombaji uongozi wa TFF na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwemo Michael Wambura, Jamal Malinzi, Athuman Nyamlani na Yusuf Manji, waliokuwa wakipingwa.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, kamati ya uchaguzi imetupa pingamizi baada ya kupitia hoja za waweka pingamizi na kubaini zilikosa vielelezo na uthibitisho.

Kamati hiyo, imetupilia mbali pingamizi dhidi ya Said Abeid anayeomba kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi , lililowekwa na Frank Mchaki, aliyeomba imuondoe kutokana na si mwenyekiti wa Klabu ya Azam na hivyo hana sifa na  si mkweli katika maelezo aliyoyatoa kwenye fomu yake ya maombi ya uongozi.

Pingamizi hilo lilitupwa kutokana na kutokidhi matakwa Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kuwa haikuambatanishwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi.

Hata hivyo, kamati hiyo, ilitupa pingamizi dhidi ya Yusufali Manji anayeomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi lililowekwa na Daniel Kamna na Juma Magoma, walioomba aondolewe kuwa hana uzoefu wa uendeshaji wa soka unaofikia uzoefu wa miaka mitano.

Waombaji wengine walioondolewa pingamizi ni  Hamad  Juma anayeomba kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, lililowekwa na  Mchaki,  Athumani  Kambi anayeomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 9 (Mtwara na Lindi) lililowekwa na  Jeremiah  Wambura.

Mwingine ni Eliud P. Mvella anayeomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 7 (Iringa na Mbeya), aliwekewa pingamizi na Said Kiponza, Abu Changawa na Peter Naminga.

Kamati hiyo ilitupa pingamizi dhidi ya  Epaphra Swai anayeomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 3 (Shinyanga na Simiyu), zilizowasilishwa na Ramadhani Sesso na Tsotsie Chalamila.

Vedastus Lufano na Mugisha Galibona wanaoomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 2 (Mwanza na Mara), waliowekewa pingamizi  na Paul Mhangwa.

Kamati hiyo pia ilitupa pingamizi dhidi ya  Michael  Wambura, anayeomba kugombea nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF, zilizowasilishwa na Said Rubea Tamim na  Josea Samuel Msengi.

Hata hivyo, kamati hiyo imetupa pingamizi dhidi ya Jamal Malinzi anayeomba kugombea nafasi ya Rais wa TFF, aliwekewa na Agape Fue na Athumani  Nyamlani anayeomba kugombea nafasi ya Rais wa TFF, aliyewekewa pingamizi na Mintanga Yusuph Gacha na Medard Justiniani.

No comments:

Post a Comment