Pages

Pages

Thursday, February 14, 2013

Pengo auweka kando U-papa






 


 
Mwadhama, Polycarp Kadinali Pengo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ASKOFU wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, amesema hafikirii kuwa Papa.

Kauli ya Pengo ameitoa jana nyumbani kwake, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kujua mtazamo wa Kanisa baada ya Papa Benedi
ct XVI, kutangaza kujiuzulu ifikapo Februari 28 mwaka huu.

Akijibu swali la waandishi wa habari, bila kueleza kwa kina, Pengo alijibu: “Sifikirii kuwa Papa, na hili halina mjadala.” Akizungumzia alivyochukulia suala la kujiuzulu kwa Papa Benedict XVI, Pengo alisema wamepokea kwa mshangao na mshituko.
Alifafanua kwamba ingawa jambo hilo si mara ya kwanza kwa Papa kujiuzulu, lakini hali kama hiyo iliwahi kutokea karne sita zilizopita. Mwaka 1415, Papa Gregory XII alijiuzulu katika mpango wa kumaliza mgogoro uliokuwepo wakati huo kati ya makadinali wa Nchi za Mashariki kugombea kiti hicho.
“Ni wazi kuwa kitu kinatokea baada ya miaka 600 ni kitu cha kushangaza na kujiuliza na maswali yanapita vichwani mwa watu, lakini hili si jambo la kwanza kutokea. 

Papa ameweka wazi sababu zake kuwa anajisikia kupungukiwa nguvu si za kiakili wala ugonjwa fulani,” Pengo alisema yeye anaona hatua iliyochukuliwa na kiongozi huyo wa juu wa Kanisa Katoliki, ni jambo la unyenyekevu alionao, kwa kuona ukweli ndani ya nafsi yake.
Viongozi ving’ang’anizi “Ni mfano kwa viongozi wanaong’ang’ania madaraka. Wanakaa madarakani kwa muda mrefu pamoja na kutokuwa na faida kwa watu wao na wakati mwingine hawatambui hilo, wanazidi kuona uongozi ni haki yao na kuona bila wao nchi haipo. Nadhani wanapaswa kujifunza kwa Baba Mtakatifu,” alisema.
Vipi Afrika?
Alipoulizwa kuwa haoni wakati umefika kwa Afrika kutoa Papa, Pengo alisema hisia hizo ni za kisiasa zaidi ya imani ya kidini, kwani Papa huchaguliwa kwa msingi wa Roho Mtakatifu kupitia makadinali na si kwa kujuana.
“Kumchagua Papa ni shughuli inayokwenda na tafakari nzito, na sala na tunafanya tukiwa mbele za Mungu, ni jambo linalofanyika mbele ya msalaba na kila mmoja anaweka kura yake kwa kueleza dhamira yake na Kristo ndiye atahukumu siku ya mwisho,” alisema.
Alisema kutamka kuwa wakati umefika wa kuwa na Papa kutoka Afrika au Muitaliano, ni kumwekea masharti Roho Mtakatifu na kuwa nje ya imani ambayo Roho Mtakatifu ndiye anayetenda kazi.
“Endapo itatokea akachaguliwa Papa kutoa Afrika, basi Roho Mtakatifu atakuwa ameona kuwa ni wakati wa Afrika, hiyo kazi tunamwachia Roho Mtakatifu atende kazi,” alisema.
Alisema hatua ya Papa kujiuzulu si jambo la kutia shaka, bali ni la kujenga imani na kuwa kamwe Kanisa halitasambaratika kwa sababu misingi ya Kanisa haimtegemei mtu mmoja, bali anayechaguliwa anaongoza kwa matakwa ya Mungu.

No comments:

Post a Comment