Pages

Pages

Wednesday, February 06, 2013

CUF, Chadema kuwasha moto upya sakata la gesi

  Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa kamanda John Heche.

BARAZA la Vijana la Chadema (Bavicha), limesema linaungana na wakazi wa Mkoa wa Mtwara kupinga uamuzi wa serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.

 
Wakati Chadema wakisema hivyo, Jumuiya ya Vijana ya CUF, imesema itafanya maandamano makubwa kuunga mkono wananchi wa Mtwara kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.


Pia, Bavicha lilisema rasilimali zinazopatikana nchini, zisiposimamiwa ipasavyo zitakuja kugeuka kuwa laana badala ya neema.

Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche wakati akifungua mkutano wa wenyeviti wa Baraza hilo nchini uliofanyika Dar es Salaam.


Heche alisema hatua ya kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam wakati uwezekano wa kuizalisha mkoani humo ukiwapo, ni kuendelea kuwanyima fursa ya maendeleo wananchi wa Mtwara.


“Vijana wa Bavicha tunaungana na wakazi wa mkoa huo kuhakikisha wananufaika na gesi hiyo, kwani itasaidia kuinua hali ya maendeleo katika mikoa ya Mtwara na Lindi,” alisema Heche na kuongeza:

“Inawezekana viwanda vikajengwa mkoani humo, gesi ikazalishwa na ajira zitapatikana lakini ikipelekwa Dar es Salaam ajira zitapatikanaje huko.”

Hatua ya Heche imetokana na siku chache zilizopita maelfu ya wakazi wa Mtwara kufanya maandamano, wakipinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.

Heche aliwataka wenyeviti wa mkutano huo kujadili kwa kina mambo mbalimbali yatakayojenga Baraza hilo.


“Vijana ndiyo msingi wa maendeleo popote duniani, kupitia mkutano huu tunatakiwa kuja na majibu ambayo yatasaidia kukijenga chama,” alisema Heche.

Naye Katibu Mkuu wa Bavicha, Deogratias Munishi alisema kikao hicho kitatoa nafasi ya kuangaliwa uhai wa chama hicho.

Munishi alisema Kamati Kuu ya Chadema imetangaza mwaka huu kuwa wa nguvu ya umma.

Mwenyekiti wa Vijana CUF, Katani Katani alisema wanashangazwa na kauli za viongozi wa Serikali ya CCM kwamba Mtwara wanataka gesi iwanufaishe wao wakati siyo kweli.


“Tunaomba ifahamike wananchi wa Mtwara wanataka uwekezaji unaotokana na gesi ufanywe Mtwara na Lindi kama ilivyokuwa kwenye viwanda vya sukari, miwa inalimwa Turiani, Mtibwa na Kilombero na uwekezaji wote upo maeneo hayo,” alisema Katani na kuongeza:

“Serikali ya CCM inapindisha jambo hilo sasa kwa kuwaunga mkono wananchi wa Mtwara tutafanya maandamano makubwa Dar es Salaam, ili kuhakikisha madai ya wananchi yanafanyiwa kazi siyo kuyapuuzia.”

No comments:

Post a Comment