Pages

Pages

Thursday, January 24, 2013

Nyota Msondo Ngoma afariki Dunia, kuzikwa leo



Marehemu Ismail Mapanga, enzi za uhai wake.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MPIGA gitaa la besi wa bendi kongwe ya Msondo Ngoma, Ismail Mapanga, amefariki Dunia usiku wa kuamkia leo, katika Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam na kuacha pengo kubwa katika bendi hiyo.

Akizungumza na Handeni Kwetu leo jijini Dar es Salaam, Meneja wa bendi hiyo,  Said Kibiriti, alisema taarifa za msiba wa mwanamuziki ni nzito kwao, huku akitarajiwa kuzikwa leo saa saba mchana.

Kibiriti alisema kifo cha Mapanga ni pigo kubwa kwa bendi yao, hasa kutokana na mchango wake katika tasnia ya muziki wa dansi, akiwa na Msondo Ngoma.

Alisema wamepokea kifo hicho kwa masikitiko makubwa, huku wakiamini kuwa wameumizwa na msiba huo wa mpiganaji mwenzao, aliyewaacha wapweke.

“Ni msiba mzito kwetu sisi wa Msondo Ngoma pamoja na wadau wote wa muziki wa dansi hapa nchini, ukizingatia kwamba marehemu ni kiungo mahiri mno.

“Familia yake imeona azikwe leo saa saba mchana, huku mwili wake ukiwa nyumbani kwake Tandika, baada ya kufariki katika Hospitali ya Temeke, alipokuwa akisumbuliwa na maradhi ya tumbo,” alisema Kibiriti.

Hata hivyo Kibiriti hakutaka kujibu swali la haraka ya mazishi ya mwanamuziki wake, hali inayoweza kuwanyima fursa ya kuzikwa na wadau na mashabiki wa Msondo kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment