Mkuu wa Wilaya Kilindi, Selemani Liwowa.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MGANGA Mkuu wa Zahanati ya Saunyi, wilayani Kilindi, Rashidi Mhande, amekamatwa
na polisi, ikiwa ni agizo la Mkuu wa wilaya hiyo, Selemani Liwowa, baada ya
kuiba dawa.
Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita katika zahanati hiyo, ambayo mganga
huyo aliiba dawa zenye thamani ya Sh Milioni tano na kukimbia kusipojulikana.
Akizungumza na Handeni Kwetu muda mchache uliopita, Liwowa alisema Mhande
amekamatwa, baada ya kutafutwa kwa siku kadhaa.
Alisema baada ya mganga huyo kukimbia, aliagiza atafutwe ili sheria
zifuate mkondo wake, endapo atakutwa na hatia katika sakata hilo la wizi wa
dawa.
“Mara baada ya kupata taarifa za wizi huo na yeye kukamatwa, niliagiza
kuwa asakwe popote alipokimbilia, hasa baada ya kufanikiwa kuondoka hospitali
ya wilaya, alipotibiwa kwa kudanganya kuwa alipigwa na wananchi jamii ya
wafugaji wilayani hapa.
“Nashukuru sasa amekamatwa, hivyo taarifa zaidi zitatoka na
kitakachofuata juu ya tukio la kuiba dawa lililofanywa na Mhande, kama Mganga
Mkuu wa zahanati hiyo,” alisema Liwowa, DC wa Kilindi.
Kukamatwa kwa Mganga huyo ni tukio jema kwa maendeleo ya watu wa Kilindi,
hasa kwa kuzingatia kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakifanya vitendo vya uhujumi
uchumi.
No comments:
Post a Comment