Pages

Pages

Friday, January 04, 2013

Kikwete ashudia Sajuki akiingizwa kaburini Kisutu

Rais Jakaya Kikwete akitia mchanga kaburini.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, leo ameongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya msanii Juma Kilowoko, maarufu kama Sajuki, katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, yaliyofanyika saa saba za mchana.

Baba wa marehemu, mzee Juma Kitilu.

Mbali na Kikwete, wengine walioshiriki kwenye mazishi hayo ni pamoja na Zitto Kabwe, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Idd Azzan, Mbunge wa Kinondoni na Said Mtanda, Mbunge wa Mchinga, sanjari na wasanii na wanamichezo, akiwamo mlinda mlango wa Simba, Juma Kaseja.
Kaburi la Sajuki lifukiwa.

Katika mazishi hayo, ambayo hata hivyo Kikwete hajaongea lolote, alionekana kufuatilia zaidi tukio hilo la mazishi ya Sajuki, aliyefariki Dunia juzi, katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili.
Msanii Profesa Jay wa tatu kutoka kulia.

Awali katika maandalizi ya mwili wa Sajuki katika makaburi hayo, wadau waliojipanga kuanzia lango la kuingilia, walijikuta wakipigwa chenga na jeneza la msanii huyo lililoingizwa kwa kupitia geti ka nyuma na kuibua mkanyagano mkubwa kutoka kwa wadau wa filamu waliokwenda kuzika.

  Kama ilivyokuwa kawaida ya wasanii kuwa na mvuto na misiba yao kugonga hisia za watu wengi, kuanzia nyumbani hadi makaburini, watu wengi walijitokeza, wakiwamo baadhi ya akina dada waliojipanga kando ya barabara inayoingia katika makaburi hayo.
 Jeneza la Sajuki likishushwa kwenye gari.

Awali marehemu Sajuki alipangwa kuzikwa saa tano za asubuhi, lakini ratiba ilibadilishwa na kuzikwa saa saba baada ya swala ya Ijumaa. Mazishi ya Sajuki yalivuta watu na kuwapa majonzi makubwa.

Wasanii wengi walijitokeza kuanzia nyumbani hadi makaburini kwa ajili ya kushiriki mazishi ya msanii huyo ambaye pia amesababisha arobaini ya mchekeshaji maarufu, Hussein Mkiety, Sharomillionea kusitishwa jana na kupangwa kufanyika leo kijijini kwao Lusanga.

Mara baada ya gari lililobeba mwili wa marehemu Sajuki kufika makaburini hapo, mkanyagano ulizidi kuwa mkubwa, hasa baada ya mashabiki kuvamia wakitaka kuubeba mwili huo na kuusindikiza katika nyumba yake ya milele.

Hata hivyo, waliokuwa kwenye jukumu la mipango ya mazishi, walielekea kufanikiwa kuwadhibiti watu hao wenye mapenzi mema na Sajuki, ingawa baadaye hali ilikuwa tofauti kidogo pale msukuamano ulipoibuka kila mmoja akitaka kukaa karibu na kaburi.

Hali hiyo ilisababisha malalamiko kutoka kwa waandishi waliokuwa wakichukua tukio hilo kwa ajili ya kuwahabarisha wadau na mashabiki wa sanaa wa Tanzania, juu ya safari ya mwisho ya msanii Sajuki, aliyefariki Dunia juzi.

Sajuki aliyeacha mke na mtoto mmoja, amefariki juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huku akifanikiwa kuzikwa na watu mbalimbali, akiwamo rais, wabunge na wasanii wengine maarufu wanaotamba hapa nchini.

Viongozi ambao nao wameshiriki msiba huo ni pamoja na Mwigulu Nchemba, Naibu Katibu Mkuu wa Chama ha Mapinduzi (CCM), Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalumu, Junuary Makamba, Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga na wengineo.

Marehemu Sajuki alizaliwa mwaka 1986 Songea alipopata elimu ya msingi na sekondari, kabla ya kuhamia jijini Dar es Salaam na kujiunga moja kwa moja katika kundi la Kaole Sanaa Group na kuingia kwenye mchakato wa kutafuta jina kwenye tasnia hiyo.

No comments:

Post a Comment