MGODI
UNAOTEMBEA
Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BAADHI ya watu wanajidanganya kuwa rais
mzuri wa Watanzania atatokana na jina lake au umaarufu wake kisiasa katika
Tanzania ya leo yenye changamoto.
Edward Lowassa, Mbunge wa Monduli
Si kweli. Wengi wenye uelewa wa mambo ya
siasa na umahiri wa kupambanua mambo, wanajua kuwa mtu huyo ambaye ndio tegemeo
la nchi, atatokana na ujuzi wake wa kubuni na kuchambua changamoto kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa lake.
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe
Katika kulisema hili, nashangaa kuona baadhi
ya watu wakitembea Mashariki na Magharibi kunadi majina ya watu wao wanaotajwa
kugombea urais mwaka 2015.
Professa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF
Sipingi nia ya watu hao kuwania urais
katika Taifa lao, ila nitashangaa kama wanasiasa hao watapitishwa kwa umaarufu
wa majina yao.
Tukifanya hivyo tutaumia. Ikulu ni mahali
patakatifu na kamwe hapatastahili kwenda kwa sababu tu ya umaarufu wake wa jina
linalopambwa na wafuasi wake.
Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere aliwahi kulisema hili enzi za uhai wake. Alipinga wale walioanza
kuingia kwenye dhambi ya kutaja majina ya wanasiasa wao eti wanafaa kugombea
urais.
Sakata hili limezidi mno mara baada ya Rais
Jakaya Mrisho Kikwete kushinda awamu yake ya pili, mwaka 2010, ambapo wenye
malengo ya kugombea urais mwaka 2015 walianza kujipanga.
Mengi yalianza kusikika au kuonekana, pale
wanasiasa hao wanavyojipambanua katika kutilia mkazo hoja zao au mahitaji yao
siku za usoni.
Kwa bahati mbaya, ndani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), hakuna hata mwanasiasa mmoja aliyetangaza nia ya kurithi
mikoba ya Kikwete.
Ingawa
hawajatangaza hadharani, lakini wachambuzi wa mambo ya kisiasa,
wamewabaini, hasa kwa kuorodhesha kauli zao au vikao vyao vya siri.
Kwa mfano, Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, ametajwa kuwa na nia ya kugombea
urais mwaka 2015.
Japo
Lowassa hajasema popote lengo hilo, lakini kila analofanya kwa sasa,
linaingizwa katika mlengo wake wa Uchaguzi Mkuu, ikiwamo chaguzi za ndani ambazo
zilitajwa kama silaha ya kwanza ya waziri huyo aliyejiuzulu.
Viongozi
wengi walioshinda katika chaguzi za ndani za CCM mwaka jana, walitajwa kuwa na
uhusiano mzuri na Lowassa, wakiwamo washindi kutoka Jumuiya ya Vijana (UVCCM)
Taifa, ambapo Sadifa Khamis Juma, alishinda nafasi ya Mwenyekiti, wakati Mboni
Mhita alishinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo.
Ukiacha
Lowassa, bado wapo wanasiasa wengine kutoka CCM, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anayetajwa kuwania nafasi hiyo ya
urais mwaka 2015 na wengineo.
Mbali na
CCM, lakini bado wapo wanasiasa kutoka vyama vingine ambavyo huko nako kuna
majina makubwa na yenye kutishia katika harakati hizo za urais.
Wapo watu
kama vile Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Willbroad
Slaa, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe pamoja na mwenyekiti wao, Freeman
Mbowe wanaotajwa kuwania urais.
Vita vyao
ndani ya chama watavimaliza wenyewe, kama itakavyokuwa ndani ya Chama cha
Wananchi (CUF), chini ya Profesa Ibrahim Lipumba, Maalim Seif Sharif Hamad na
wengineo kutoka NCCR-Mageuzi, TLP na vyama vingine vyenye kusimamisha wagombea
wa nafasi ya urais.
Kama
nilivyosema hapo juu kuwa yeyote anaruhusiwa kuwania nafasi hiyo, lakini
aangaliwe umahiri wake, sifa zake zinavyoweza kulikomboa Taifa letu.
Mtu huyo
asipewe nafasi hiyo nyeti eti kwa kuwa anapopita barabarani wapo wachache
wanaolala na yeye kupita juu yao, au kutandikiwa kanga za sandukuni kama ishara
ya kumlaki mwanasiasa huyo.
Tanzania
yenye changamoto nyingi kama vile ugumu wa maisha, magonjwa na elimu duni,
haitapiga hatua kama rais wake hatakuwa makini.
Tutaanguka
zaidi, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuwa makini katika mchakato huo wa
kupatikana mrithi wa Kikwete, ambaye hapana shaka naye anaumiza kichwa jinsi
gani ya kumuachia mrithi wake.
Najua
wapo ambao majina na haiba zao ni kubwa, lakini suala la urais si jambo la
kitoto. Hivyo tuwahoji na kuwapima kama kweli wanaweza kuvaa kiatu hicho.
Na kama
tunajua kuwa hawawezi basi uungwana ni kuwaambia na kuwaweka kando bila kuleta
chuki na uhasama katika siasa za Tanzania zinazozalisha matatizo kwa baadhi ya
wanasiasa wetu.
Huu ndio
ukweli. Kuusema wakati huu ambao watu wanapita na wapambe wao kusafisha njia
kunataka moyo wa chuma, hasa kwa kuangalia kuwa kila mtu anataka kuweka mtandao
wake kwa ajili ya kumpatia nafasi hiyo.
Rais wa
Tanzania ni yule atakayeinua uchumi wa Taifa lake kwa kuwasimamia vyema
watendaji wake pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali za Taifa zinawanufaisha
wazawa.
Kwa
mfano, licha ya kujengwa shule za kata kwa ajili ya kuwafanya watoto wa
masikini wapate elimu ya sekondari, lakini shule hizo hazina walimu wala vifaa
vya kufundishia.
Ukirudi kwenye
elimu ya msingi, nako kuna changamoto nyingi, wakiwapo walimu kugoma kwenda
katika maeneo yao ya kazi kwa sababu ya kukwepa maisha magumu.
Shule
nyingi zilizokuwapo vijijini zimekumbwa na balaa hilo, hivyo tunahitaji rais
mwenye mipango na ambaye atahakikisha kila mtu anafanya kazi yake kama
inavyotakiwa.
Naamini
watu wa aina hiyo wapo, ingawa kwa bahati mbaya, wanaweza kufichwa na wale
wenye nyota zao au uwezo wa kipato wa kununua watu wa kupita nyumba hadi nyumba
kuwahamasisha wajumbe wawapigie kura siku ya kutafutwa nani anaweza kupitishwa
kuwania urais.
Ingawa
Kikwete amejitahidi katika kipindi cha uongozi wake, lakini bado hatuwezi kukaa
na kubweteka na badala yake tunahitaji mwingine mwenye ujasiri, mtu makini,
mbunifu na mwenye kuendeleza miradi inayowanufaisha Watanzania wote.
Mwenye
kujua uwezo anao, basi asifikirie tu kuwa watu watamuingiza kutokana na jina
lake na atakayefanya hivyo, atakuwa amekosea na kuwasaliti Watanzania.
Huu ndio ukweli wa mambo. Ndio maana Mgodi
Unaotembea umeona ulijadili suala hilo kwa kina, maana rais bora ndiye
anayeweza kuwakomboa Watanzania.
Mengi yapo yanastahili kujadiliwa kwa kina,
hivyo naamini kila mmoja atakaa na kujiangalia mara mbili, huku wale wanaomwaga
fedha kwa ajili ya kunufaisha majina yao, nikiwashangaa kwa kitendo hicho, huku
nikiamini kuwa malengo yao yana matege na wanadanganya nafsi zao.
Mungu
ibariki Tanzania.
0712
053949
0753
806087
No comments:
Post a Comment