Pages

Pages

Friday, December 14, 2012

WATUHUMIWA WA UTAPELI WA FEDHA WATIWA MBARONI


RPC KILIMANJARO-ROBATH BOAZ
JESHI la Polisi Mkoani Kilimanjaro, linawashikilia watu sita, wakazi wa Moshi mjini,  ambao wanasadikika kuhusika na kundi kubwa la Matapeli ambalo limekuwa likiwasumbua wakazi wa Moshi, kwa muda mrefu sasa  kwa  matukio ya utapeli ambayo yameshamiri mjini hapa kwa muda mrefu sasa.

Watuhumiwa hao  walikamatwa jana katika maeneo ya Boma Ng’ombe, wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro baada ya wananchi kutoa taarifa ya uwepo wao katika kituo kidogo cha polisi cha Boma Ng’ombe wakiwa na vifaa vyao vya utapeli.

Kundi hilo limekuwa likisakwa na Jeshi la Polisi kwa muda mrefu ambapo inadaiwa kuwa wamekuwa wakiwatapeli watu kwa kuwadanganya wananchi watu kuwa wanauwezo wa kuwatengezea fedha nyingi kwa kutumia mitambo yao.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robath Boaz alisema watu waliokamatwa ni Athumani Ally (39), ambaye anadaiwa kuwa ni mganga wa kienyeji , Emanuel Jacob (20), Christian Samwel (23), Jolvin Joseph (26), Aziza Athumani (26) na mtu mmoja mwenye asili ya kihindu ambaye anadhaniwa kuwa ndiye kiongozi wa kundi hilo Kasim Somji (31).

Kamanda Boaz alisema kuwa watu hao kwa sasa wanashikiliwa na jeshi la polisi na kuongeza kwamba uchunguzi unaendelea kuwasaka wanachama wengine wa mtandao huo na mara tu uchunguzi utakapomalizika watafikishwa mahakamani.

“Kwa sasa watuhumiwa wote wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na mara tu baada ya kumaliza uchunguzi sheria itafuata mkondo wake,” alisema Kamanda Boaz.

Wakati huohuo Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia, mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Wasiwasi John (28),  ambaye ni mmakonde, mkazi wa Pasua Matindigani, kwa tuhuma za kukutwa na Noti bandia.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa majira ya saa mbili na nusu usiku akiwa anajaribu kutumia noti hizo bandia, zenye namba za usajili BC 2937831 na BK 3153543 kufanya manunuzi dukani.

Kamanda Boaz, alisema kuwa mtu huyo atafikishwa mahakamani mara tu baada ya uchunguzi kukamilika na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa inapotokea kuna kundi lolote la watu wanawashuku au kubaini jaribio lolote la utapeli na uhalifu.


No comments:

Post a Comment