Pages

Pages

Sunday, December 23, 2012

Ukiamini shoga yako imekula kwako




MAMBO FULANI MUHIMU

Mapenzi yenye raha kwa wawili hawa
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAHENGA hawakukosea waliposema ‘kikulacho kinguoni mwako’. Msemo huu muhimu kabisa ni kati ya ile inayotumiwa kwa nyakati tofauti.

Wazee wetu walifahamu hilo, kitu kilichowafanya waiweke kinywani mwao wakiwa na lengo la kutoa elimu kwa jamii, baada ya kuona marafiki wanaojuana hugeuka kama kinyonga na kufanya wanavyojua wenyewe.

Hii ni mbaya sana. Kwa bahati mbaya aina hii ya maisha inatumiwa na watu wengi, jambo linalowafanya washindwe kuaminika mbele ya hadhira.

Msemo huo naweza kuutumia hata katika mambo ya kimapenzi. Baadhi ya watu wasiokuwa na akili timamu, hujikuta wakiwabadilikia marafiki zao na kuwatamani wapenzi au wake zao.

Wale wanaoaminiwa sana na jamaa zao, hutumia muda huo kujiwekea mazingira ya kuwasaliti marafiki zao hao, baada ya kufanikiwa kuwarubuni wenzao.

Huo ndio ukweli. Wapo ambao hadi leo wanatumia nafasi hiyo kwa kujiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi na wake au wapenzi wa marafiki zao.

Ni wengi mno. Wanatumia muda huo kujichanganya kimwili kwa watu hao, tena katika nyumba au vitanda vya hao maswahiba zao.

Hao ndio watu bwana. Maana watu ni wengi ila binadamu ni wachache. Hao kufanya uchafu wa kimapenzi na wapenzi wa wenzao ni rahisi kwao.

Hawaoni uchungu ama kinyaa huku wakijifanya wajuzi wa mapenzi kwa kutoa mitindo ambayo wanajua fika waume hao hawajawahi kuipata kwa wake watu wao.

Huwateka kabisa kiakili na kifikra. Hubarikiwa utundu wa kujihusisha na mapenzi na wasichana hao ambao, anajua kuwa ni mali za watu.

Sio wanaume tu. Hata wanawake mandumilakuwili ni wengi mtaani kwetu. Yule msanii wa Bongo Fleva, Samu wa Ukweli alisema hata kwetu wapo.

Tena wanawake ndio kabisa. Baadhi yao huomba ruhusa kabisa kwa marafiki zao wakitaka kutoka ‘out’ na mashemeji zao.

Wakifika huko huwafanyia vituko kwa kujishaua kwa mengi, ikiwamo kurembua macho ama mitego mingine ambayo ni wanaume wachache humudu kuiugundua na kuvaa ujasiri wa aina yake.

Wengi wao huingia mtegoni na kushindwa kuvumilia, hivyo kujikuta hisia zao zikitamani kulala nao kitanda kimoja kwa ajili ya kuvunja amri ya sita.

Ndio hapo unapotakiwa kusoma alama za nyakati. Hutakiwi kumuamini rafiki yako hata kidogo. Mambo ya mume au mpenzi wako lazima ufanye wewe mwenyewe maana siku hizi waaminifu ni wachache.

Lazima ujuwe kwamba ukimpa nafasi rafiki yako kwa mambo ya mapenzi, huenda ukapinduliwa na nyumba yako akaenda kuishi yeye.

Wapo wengi mtaani kwetu na huko kwenu pia. Baadaye hulia na kusaga meno. Hudanganya kwa mengi likiwamo ‘sijamuita mumeo kaja mwenyewe’.

Hapo jua huna chako muungwana. Hivyo lazima ujuwe mtu wako wa karibu ana uwezo wa kuwa mbaya yako, endapo umemuachia nafasi kubwa kwa mtu wako, hadi kumuingiza mtegoni.

Jua kabisa mtu wako ana uwezo wa kunyakuliwa kulingana na mwenekano wake. Iwe ni uvaaji, usomi wake, ama uwezo wake wa kifedha.

Haya na mengineyo yanaweza kuifanya ndoa ama uhusiano wako ushindwe kuendelea kutokana na wachokonozi hao kuingia kwenye malavidavi yako.

Hakuna njia ya mkato zaidi ya kuhakikisha kwamba rafiki yako, haingii zaidi kwenye ukaribu na mume au mke wako, pamoja na wale wapenzi.

Kuwa mkali, maana siku zote kunguru muoga hukwepesha ubawa wake. 
Ingawa baadhi yao huwaachia waume zao ama wake zao nafasi ya kujenga mazoea ya ajabu kwa wenzao, ila hulia kilio cha mbwa.

Ni pale wanapong’amua kwamba mtu wake ameanzisha uhusiano wa kimapenzi na rafiki yake na kuufanya uhusiano wao uyumbe kama sio kuvunjika.

Akija ndani asubiri sebuleni ila sio kuingia hadi chumbani, huku akijua wewe upo mbali. Ikiwezekana asikae ndani kwa madai anakusubiri wewe.

Ndio ukweli huo. Bila kuwa makini utaibiwa na hao hao marafiki zako, maana uadilifu, uaminifu kwenye uhusiano umekuwa adimu kuliko fedha.
 
kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087

 

No comments:

Post a Comment