Pages

Pages

Saturday, December 22, 2012

THE GREEN PASTURE COLLEGE



Chuo na shule zinazowajali wanafunzi wake
 Mkuu wa Chuo, Filbert Paschal

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
ILI Tanzania iweze kunufaika kuungana kwa nchi za Afrika Mashariki (EAC), watu wengi wamekuwa wakijitokeza kuanzisha shule na vyuo ili kuwaandaa watendaji wa baadaye.
Wanafunzi wa The Green Pasture
 
Mbali na shule hizo, wengineo nao hujaribu kuanzisha hata vibanda kwa ajili ya kuwapa tuition wanafunzi, wakiwamo wa msingi, sekondari na vyuoni.

Siku hizi sio ajabu kukutana na kibao kimeandikwa, tunafundisha kingereza na kifaransa hapa. Wengine wanaandika, tunatoa masomo ya jioni, kwa wale wanaofanya kazi.

Huu ni ujumbe mzuri mno. Hakika unafurahisha machoni, hasa kwa kuona kuwa ni juhudi za Watanzania wenzetu, kutaka kuwaandaa wenzao.

Miongoni mwa chuo hicho ni Green Pasture College chenye maskani yake, pembeni mwa barabara ya Mwananyamala, kituo cha Komakoma.

Ukifika hapo tu, utakutana na ghorofa lenye maandishi ya chuo hicho, ambacho pia hutoa masomo ya asuhubi na jioni kwa wale wanaoshindwa kuingia darasani asubuhi.

Akizungumza na Mtanzania mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Chuo hicho, Filbert Paschal, anasema chuo chao kinatoa elimu ya juu, huku wakijitahidi kuhakikisha kuwa wanafunzi wao wanakuwa na sifa za kuajiriwa.

Anasema kwamba tangu walipoanzisha chuo hicho, wamekuwa wakipata wanafunzi wengi kutokana na ubora wao pamoja na elimu nzuri wanayoitoa.

“Tumeanzisha chuo hichi ambacho pia kimechanganyika na elimu ya Sekondari kwa miaka miwili yani (QT) pamoja na sekondari ya kawaida, yani wanaosoma kwa miaka minne.

“Lakini katika hilo, tumekuwa tukipokea sana wanafunzi wale waliofeli kidato cha nne na kutaka kurudia mitihani, hasa wale wenye ndoto za kwenda kidato cha tano na sita pamoja na wanaosoma kozi mbalimbali,” alisema.

Paschal anazitaja kozi hizo kuwa ni pamoja na Hoteli Management, International Technology (IT), Business Education, Ualimu wa Chekechea.

Kozi nyingine ni kujifunza na lugha mbalimbali, ikiwamo Kingereza kinachopewa mkazo kwa ajili ya kuwapa mbinu za mawasiliano wanafunzi ambao muda mchache ujao watakuwa waajiriwa katika ofisi mbalimbali.

Paschal anasema katika kuhakikisha kuwa wanatoa elimu nzuri, wameamua kuwapa kipaumbele na kuwatafutia ajira wanafunzi wanaofanya vyema katika mitihani yao, hasa kwa upande wa chuo chao.

Anasema wanafanya hivyo kwasababu baadhi ya wanafunzi wamekuwa na uwezo wa juu lakini wanashindwa kupata kazi, hivyo chuo chao kimejaribu kuweka utaratibu wa kuwasaidia kwa njia nzuri na zinazokubalika.

Mkuu huyo wa Chuo anasema kwamba wameanzisha chuo hicho kwa ajili ya kuwafundisha watu wa lika mbalimbali bila kuangalia jinsia zao, huku suala la ada likiwekwa kwa mpangilio mzuri unaomuwezesha mtu kumudu.

“Sisi tunajua kuwa mtu ambaye yupo chini ya miaka 18 na ambaye anasoma elimu ya Sekondari huyo kuna uwezekano mkubwa kuwa analipiwa na wazazi au walezi wake, hivyo ada yake tunaweza kufikia makubaliano ya ulipaji wake kabla ya kuanza masomo yake, ingawa uungwana zaidi huwekwa.

“Lakini kwa watu wazima ambao tunajua wakati mwingine husoma na pia kuwa na familia zao, hivyo tunawaruhu walipe kidogo kidogo ili tuweze kuelimishana na kupeana elimu hii ambayo kwa hakika si gharama kubwa kwetu,” alisema.

Paschal anasema kuna wanafunzi ambao umri wao ni mkubwa kuliko walimu wao, lakini wamekuwa wakipeana ujuzi huo kutokana na wote kuwa na malengo sawa ya kuwa na Watanzania wenye elimu na sifa za kuitumikia Taifa lao hasa tunapoelekea kwenye muungano wan chi za Afrika.

Mkuu huyo wa Chuo anasema kwamba kabla ya kufikia kwenye muungano huo, lazima wazazi na walezi pamoja na serikali yao kwa ujumla kupigia kelele sana suala la elimu.

Anasema ni mbaya tunapoelekea huko huku watoto wetu au wanafunzi wakiwa wazito kuzungumza lugha ya kigeni nay a biashara hasa ya Kingereza na kuwataka wakagombanie ajira kutoka kwenye taasisi zao.

Mkuu huyo wa Chuo anasema ni ngumu Mtanzania wa aina hiyo kufanikiwa kupita mbele ya Wakenya, Waganda waliopiga hatua katika nyanja nyingi, ikiwamo elimu na nyinginezo.

“Tuna kila sababu ya sisi walimu tunaowapika wataalamu kuanzia shule za Msingi, sekondari na vyuoni kuhakikisha kuwa tunakazania masomo muhimu, likiwamo la lugha ya kingereza, Kiswahili na mengineyo.

“Tukifanya hivyo, hata mwanafunzi anapokwenda chuoni, kusomea mambo ya mitambo, udaktari na mengineyo atamudu kwakuwa lugha hiyo ya kigeni anayofundishiwa yeye anaijua na atafika mbali katika masomo yake,” alisema.

Paschal anasema hadi sasa chuo chao kwa pamoja kina wanafunzi zaidi ya 350, wakiwamo wale wanaosoma elimu ya Sekondari kwa miaka miwili au wale wanaojiandaa kufanya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012.

Mkuu huyo anasema kutokana na weredi na aina ya ufundishaji wao, wanafunzi wote wanaojiunga na chuo chao wanafika mbali na kumudu taaluma zao.

Malengo yao katika siku za usoni ni kuhakikisha kuwa chuo chao kinakuwa bora zaidi kwa kuongezea zana za ufundishaji pamoja na ubunifu wa namna gani ya kumuandaa mwanafunzi katika mazingira mazuri kimaisha.

Anasema wamekubaliana na walimu wao kutokwenda mbele kama anajua baadhi ya wanafunzi wake hawajaelewa, hivyo njia hiyo ni nzuri na inawanufaisha wanafunzi wake.

“Ni mbaya mwalimu kwenda kwenye (topic) mada nyingine kama anajua wapo wanafunzi ambao hawajaelewa chochote alichofundisha kwenye kipindi chake ili asiweze kuwa na mizigo au watazamaji wa somo lake.

“Tunashukuru tunaelewana na tunaamini utaratibu huu ni mzuri kwetu sisi walimu pamoja na wanafunzi wetu, ukizingatia kwamba hizo ni juhudi, harakati na maarifa tunayopeana kwa pamoja kwa ajili ya kuwa na wanafunzi bora ambao tunaamini siku sio nyingi wakitoka hapa watakuwa wafanyakazi,” alisema.

Paschal anamaliza kwa kuwataka Watanzania wenye nia ya kujiendeleza na masomo kujiunga na chuo chao, wakiwamo wale wanaotaka kufanya mtihani wa QT kuchukua fomo kwa ajili ya mwaka wa masomo unaoanza mapema mwezi Januari 2013 na 2014.

Kuhusu IT, elimu ya kompyuta, wanafunzi wote wanaosomea taaluma hiyo kila mmoja na kompyuta yake kwa ajili ya kumpa muda mrefu zaidi kwenye kifaa hicho.

Kwa mujibu wa Paschal, elimu wanayotoa ni dira kwa watu wote hivyo ni jukumu la wazazi, walezi pamoja na watu wazima wenye ndoto za kujiendeleza kielimu kuchangamkia fursa katika Chuo chao cha The Green Pasture College, kilichokuwapo Komakoma jijini Dar es Salaam.

Mwisho


No comments:

Post a Comment