Pages

Pages

Monday, December 17, 2012

Sera ya umeme vijijini ipo kwenye makaratasi

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo


Na Kambi Mbwana, aliyekuwa Handeni
LICHA ya baadhi ya vijiji kupitiwa na line za umeme kwenye paa za nyumba zao, nishati hiyo muhimu kwa uchumi duniani kote inaendelea kuwa kitendawili kwao. Nashangaa na kujiuliza maswali kila ninapoangalia nguzo hizo za umeme vijijini humo.

Katika suala kama hilo, si tu watu wanashindwa kufahamu utendaji kazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linalojipambanua kutaka maoni jinsi ya kujiendesha kwa mafanikio makubwa nchini, ila wao na serikali yao wanaendelea kudharauliwa kutokana na sera zao na mipango yao kuwa kwenye makaratasi zaidi.
 Mkuu wa Mkoa Tanga, Chiku Galawa

Hakuna mipango zaidi ya porojo katika majukwaa yao, hasa wanaposema kuwa kila kijiji au Mtanzania lazima apate huduma ya umeme. Ni kweli au tunadanganya?

Hawawezi kufanya kazi kama timu moja. Badala yake, wanayatatua kwa kupitia maandishi katika karatasi zao, hivyo kushangaza umma. Nasema hivi huku nikijua baadhi ya vijiji havina umeme bila sababu za msingi.

Kwa mfano, ukitoka katika wilaya Korogwe kwenda Handeni, utashangaa kuona njia nzima kumepitishwa umeme unaopelekwa Handeni mjini.
 Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu

Kwa sababu hiyo, vijiji vyote vilivyopitiwa na huduma hiyo, hakika ni aibu kama hadi leo, wananchi wake hawaipati, licha ya kuwa walinzi wa nguzo na waya hizo.

Kwanini nasema hivyo? Njia ya umeme inayokwenda Handeni, ingeweza kuwanufaisha pia wananchi wa vijiji vyote hadi kufika Handeni Mjini, kama ilivyofanya hivyo kwa vijiji vya Sindeni, Misima na Kwenjugo. Lakini, hadi leo, vijiji hivi vya Komsala na Kwakiliga huduma hiyo hawaipati zaidi ya kuangalia kwa wenzao.

Kwa jinsi nilivyozungumza na wananchi hawa, wamechoshwa na mwenendo huu, huku wakiona ajabu ya vijiji vyao kupitwa kimaendeleo na kukumbukwa pia katika suala zima la nishati ya umeme yenye kuchochea maendeleo kwa watu wengi.

Hapa ndipo ninapojiuliza maswali. Kwanini? Ni tatizo gani linalokwamisha wananchi wa vijiji hivi wakose huduma hiyo muhimu? Wizara ya Nishati na Madini inajua kuwa ili Taifa lao liwe na maendeleo, lazima huduma ya umeme itumiwe na kila mtu.

Ni umeme tu unaoweza kuboresha kipato cha mtu mmoja mmoja. Leo hii mwananchi anaweza kuuza hata maji baridi na akaingiza visenti. Leo hii vijiji vya aina hiyo vinaweza kuboresha huduma za afya kwakuwa umeme upo kijijini kwao.

Vituo vya afya, maduka ya dawa za binadamu na mifugo vitapatikana kwa wingi. Lakini hali ikiendelea hivi, ina maana wananchi hawataendelea.

Huduma zao zote watazipata katika wilaya ya Korogwe, hasa kwa vijiji hivi viwili visivyokuwa na umeme kwa miaka 51 sasa ya Uhuru na watendaji wakiwa wamefumba macho.

Hakuna sababu ya msingi. Ni uzembe na ubabaishaji wa aina yake. Utashangaa kama kuna watendaji kutoka katika Shirika hili la umma la Tanesco. Kiutendaji, vijiji vya Komsala, Kwamatuku na Kwakiliga vinastahili kuhudumiwa na wilaya Korogwe.

Wamefanya hivyo kwasababu ni ngumu watendaji kutoka wilayani Handeni hadi katika vijiji hivi ambavyo vipo karibu kabisa na Korogwe. Sawa. Sio tatizo la kuangalia nani au wapi wanatakiwa uhudumia upande Fulani.

Ila wasiwasi wangu ni huu uzembe unaofanywa na watu bila sababu za msingi. Ingawa vijiji hivi vipo wilayani kwao, lakini Handeni haina sauti juu ya kero hii. Badala yake wanawaachia wilaya ya Korogwe, ambayo kwa hakika ina mapungufu mengi.

Wao Korogwe walitakiwa waandike bajeti na kuviombea vijiji hivi ambavyo kwahakika vinastahili kupata huduma ya umeme. Endapo Shirika la Umeme halitakuwa na uwezo wa kutatua kero hiyo, basi wafikishe kwenye ofisi za Rural Energy Agency (REU), waliopewa jukumu la kusambaza umeme vijijini.

Hichi ni kitengo kinachofanya kazi chini ya Wizara ya Nishati na Madini yenye Waziri makini na mchapakazi, Profesa Sospeter Muhongo. Hakuna asiyetambua utendaji wake. Lakini, watu waliokuwa katika baadhi ya vitengo ni wadhaifu.

Kutokana na hilo, kuna haja ya kujipanga upya. Hatuwezi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, kama hadi leo kuna vijiji ambavyo havina umeme na wapo kwenye underline. Huu ubabaishaji unaletwa na nini?

Miaka 51 ya Uhuru Tanzania tunavuna nini? Haya lazima watu wayajuwe. Mapema wiki hii nilipata kuzungumza na watendaji zaidi ya watatu kutoka wilayani Handeni, Korogwe na Tanga, ambapo ndipo kwenye ofisi za mkoa.

Nisingependa kuwataja watu hao ambao kwa hakika wana sauti na nafasi kubwa katika ofisi hizo za Tanesco katika kila wilaya na Mkoa kwa ujumla. Maneno yao niliyaelewa.

Maana wote wameonekana kulia na serikali na kukosa mbinu za kiutendaji kwa ajili ya kufanikisha maisha bora kwa kuwafikishia kwanza huduma ya umeme wananchi vijijini.

Mmoja alisema, “vijiji vingi vinashindwa kuunganishiwa umeme kwasababu ya ukosefu wa bajeti kutoka serikalini. Kumbe?

Tatizo ni bajeti au kuna lingine? Nauliza hivyo kwasababu vipo vijiji vilivyopitiwa na njia ya umeme na visivyohitaji gharama kubwa kuwaunganisha kwenye huduma hiyo muhimu duniani kote.

Mbaya zaidi, wenzao wameipata huduma hiyo. Nadhani haya ni matatizo makubwa na mfumo mbaya wa watendaji wetu. Watu wanaostahili waendeshwe kwa viboko. Sio lazima mpaka watu waseme au kulia hata pale pasipostahili.

Akili ya kawaida tu, inaweza kumuongoza mtu kuamua namna ya kuongoza kwa faida ya mwananchi mmoja mmoja na serikali kwa ujumla. Sina ugomvi na REA.

Hawa wanapelekewa muongozo na maombi kutoka kwa ofisi za Tanesco wilayani au mkoani kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini hasa kama kwa fedha zao wenyewe wameshindwa.

Naamini fedha wanazo. Huo ndio ukweli. Katika kila nyumba iliyounganishwa huduma ya umeme hapa nchini, anakatwa kodi asilimia 22. Kiasi hiki kimeganywa katika makundi matatu ambayo ni VAT asilimia 18, REA asilimia 3 na EWURA wanapata asilimia moja.

Kwa maana hiyo, asilimia tatu hizi za REA zinazolipwa na wananchi, lazima zitumike kwa mafanikio sambamba na kusambaza huduma hiyo vijijini. Tanesco katika wilaya hadi mikoa lazima wafanye kazi yao kama inavyotakiwa.

Watembelee kwenye vijiji visivyokuwa na gharama katika uunganishaji wake. Huo ndio ukweli. Muda huu sio wa kupiga porojo ofisini huku tukiwaacha watu katika umasikini wa kutupwa kutokana na utendaji wetu mbovu.

Watu wanashangaa. Haya maisha bora yanayosemwa yameshafika au bado yanasubiriwa baada ya kuhubiriwa kila uchao na wanasiasa wetu? Kama bado tunafanya bidii kuyatafuta? Kwa njia gani? Ni biashara, kilimo na viwanda.

Lakini biashara au viwanda haviwezi kwenda vizuri kama umeme wa uhakika haupatikani. Haya ni matatizo makubwa. Nadhani Waziri wa Nishati na Madini, Muhongo angekutana sasa na watendaji na kuwakemea vikali.

Ni aibu kubwa. Kama vijiji ambavyo wapo kwenye underline na hawana umeme, vipi vile vijiji vinavyohitaji kupelekewa njia kwanza, tena katika umbali mrefu na kutumia gharama za fedha na muda kwa ujumla?

Haya lazima tujiulize. Tunawekaje mazingira ya kujiendesha kwa mafanikio na sio kukaa ofisini kutumia fedha za umma bila mpango. Tanesco Korogwe, Handeni na mkoa kwa ujumla waone hii ni aibu yao na jamii inawacheka.

Serikali ya Jakaya Mrisho Kikwete itakuwa na changamoto nyingi, maana kati ya sera au urendaji kazi wake unakwamishwa na watu wake. Anahubiri kweli maendeleo, lakini ndoto hii inaishia njiani na kuwaumiza watu wengi.

Kwanza lazima tujuwe, kijiji chenye hadhi ya kupata umeme na ikakosa, basi watalaamu wanajua jinsi serikali imavyokosa mapato kutoka kwao.

Mbali na serikali kutopata mapato kwasababu ya vijiji hivyo kutokuwa na umeme, bali pia wananchi wanaendelea kulowea kwenye umasikini maana hawawezi kufanya biashara imayohitaji umeme.

Simu inapokwisha chaji, ina maana mwananchi huyo inamlazimisha atoke kijijini kwao hadi wilayani Korogwe na kutumia muda mwingi njiani. Matokeo yake mtu huyo anashindwa kufanya kazi nyingine za kimaendeleo.

Hii haiwezi kukubaliwa. Serikali kwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini, REA na ofisi za Tanesco katika wilaya hadi mkoa kuna haja ya kujipanga kwa ajili ya kuondoa kero hizi kwa namna moja ama nyingine.

Ni rahisi sana. Ni nzuri. Heshima kwa serikali itarudi, ukizingatia kwamba kiongozi wa serikali kuzungumzia maendeleo anapata kazi kubwa, maana njia anayopita ni ndefu na wananchi wanajua jinsi watu hao wanavyoweza kupiga soga.

Huu ndio ukweli wa mambo. Tuukubali kwa ajili ya kusonga mbele kwa kuhakikisha kwamba watu wengi zaidi wanapata huduma ya umeme ili waangaze maisha yao. Vinginevyo kazi ipo.

Tukutane tena wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment