Pages

Pages

Monday, December 24, 2012

Samatta, Ulimwengu wasiidharau Stars



Mbwana Samatta, akiwa kwenye usafiri anaotumia nchini Kongo. Picha kwa hisani ya mitandao.
SIWEZI KUVUMILIA 
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MBWANA Samatta na mwenzake Thomas Ulimwengu hawana sababu za kuidharaau timu ya Taifa, Taifa Stars, hata kama wamechoka au wanamatatizo ya kiafya.

Sina lengo la kusema kwamba wachezaji hao wanaokipiga katika klabu ya TP Mazembe ya nchini Kongo wacheze tu hata kama ni wagonjwa, bali matatizo yao hayo yasemwe na wataalamu wa tiba wa Stars na kocha wao.

Kwa miezi kadhaa sasa wachezaji hao, hasa Samatta amekuwa kwenye kashfa ya kuidharau timu yake bila sababu za Msingi na kuanza kuleta wasiwasi kwa maendeleo yake.

Kwanini nasema hivyo. Timu ya Taifa ndio jicho la kuonwa wachezaji wengi wa ligi wa ndani na wale waliokuwa nje ya nchi.

Wadau wa soka wanaweza kuangalia zaidi wachezaji wa timu ya Taifa, kuliko wale wanaocheza kwenye vilabu. Huu ndio ukweli. Hata Samatta mwenyewe anajua kuwa mafanikio yake aliyokuwa nayo sasa yamechangiwan kwa kina na Stars.

Ikiwa chini ya Marcio Maximo kabla ya kumaliza mkataba wake na kurudi kwao Brazil, Samatta aliweza kutumika kwenye Stars hiyo na kutangazwa sana.

Kama hivyo ndiyyo, leo hii Samatta anapata wapi jeuri ya kuidharau Stars hata kama iwe haina tija kwake? Stars ni timu ya Watanzania wote, wakiwamo wale wa Simba na Yanga.

Mchezaji anayeweza kuidharau timu ya Taifa, ina maana huyo analidharau Taifa lake lote. Wachezaji wengi wa nje wakiwamo walioendelea wanazithamini timu zao.

Mchezaji asipoitwa kwenye timu yake ya Taifa analia. Hana furaha zaidi ya kuumizwa na matokeo hayo. Tunashuhudia mafanikio yao yanavyochangia kuleta tija kwa soka lao.

Hivi karibuni niliwahi kukutana na mlango wa Stars, Juma Kaseja katika matukio ya Kitaifa. Kaseja alinikimbilia nikiwa na wadau wengine wa soka, akisema kuwa hadi leo ana gazeti la Mtanzania, ikiwa na ukurasa huu wa Siwezi Kuvumilia akisema ulimuandika vibaya kuwa hana mapenzi na Stars.

Kaseja alisema sio kweli bali wakati naandika makala yale, alikuwa ameumia taya. Namimi bila kuleta kelele, nilimwambia kwakuwa upo kwenye shughuli za Taifa, ukirudi tuonane tulijadili hilo.

Nilifanya hivyo kwa kulinda heshima yake. Ningeweza kumwambia pale kuwa, kama uliumia taya saa chache ulipoitwa na Stars, ilikuwaje saa kumi jioni ufanye mazoezi na timu yako ya Simba jijini Tanga?

Ningemuuliza tena, kwanini uliwahi kutupwa nje ya Stars kwakuwa ulionekana ukishangilia baada ya Stars kubugizwa mabao 4-0 kutoka katika moja ya timu za Afrika, huku golini akiwa ni Ivo Mapunda?

Hakika siwezi kuvumilia. Lakini kwake nilijizuia kwakuwa maswali hayaa ningemuuliza Kaseja huenda ningemuumiza zaidi, ukizingatia kwamba ndio ameanza tena kurudi kwenye kiwango cha kuitumikia Stars, ikiwa na Kim Poulsen.

Nilichoshukuru, Kaseja ni miongoni mwa wasomaji wa safu hii ya siwezi kuvumilia kama walivyokuwa Watanzania wengine, nikiamini siandiki bila kufanya uchunguzi.

Kama hivyo ndivyo, Samatta na Ulimengu hawana uwezo wa kuikataa timu yao ya Taifa. Katika mchezo wa juzi dhidi ya Zambia yenye vichwa kama vole Christopher Katongo, Stars iliweza kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Bao hilo lilifungwa na winga machachari, Mrisho Ngassa. Kama vijana hao wangekuwa muhimu zaidi, Stars ingefungwa na wanapokuwa wao ishinde.

Katika mchezo huo wa juzi Jumamosi, kuna mashabiki walikuwa na mabango yanayosema Who’s Samatta. We have Ngassa. Kwa tafsili isiyokuwa rasmi, mdau huyo anauliza.

Samatta ni nani? Tunaye Ngassa na kweli umuhimu wake unaonekana uwanjani kwa kuipachikia bao pekee na la ushindi timu yake ya Taifa, Taifa Stars.

Huu ndio ukweli. Mchezaji yoyote anayeweza kuikataa timu ya Taifa, huyo anashangaza sana. Wakala yoyote hawezi kusajili mtu bila kuangalia mafanikio yake uwanjani na kwenye timu ya Taifa.

Sasa kama hivyo ndivyo, kuna kila sababu ya wachezaji wetu wa Tanzania kuwa na akili timamu katika utendaji wa kazi uwanjani kwa kuangalia harakati zao kimaendeleo.

Vinginevyo, wachezaji wa aina hiyo watakuwa kwenye wakati mgumu, maana mafanikio yao zaidi huenda yakapatikana kwenye timu za Tanzania.

Makala ya Siwezi Kuvumilia hutoka kila Jumatatu katika Gazeti la Mtanzania...
 
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment