Pages

Pages

Sunday, December 16, 2012

Natamani kuandaa ligi Handeni



Mbunge wa Handeni, Abdallah Kigoda

Na Kambi Mbwana
KUTOKANA na uhaba wa ukosefu wa ajira, Tanzania ingeweza kuwapatia ajira vijana wake, endapo ingewekeza kwa dhati katika michezo, hususan huu wa mpira wa miguu unaotesa duniani.

Kama hivyo ndivyo, basi kuwekeza huko kungeanzia katika vijiji, wilaya na baadaye mkoa, katika hali ya kuona kwamba wenye vipaji vya michezo wanaingia kwa wingi na kujiendeleza zaidi.

Hakika natamani kuandaa ligi ya aina hiyo, hasa kwa wilaya ya Handeni ambayo nina uhakika vipaji vingi vipo, ingawa hakuna mwenye nia ya dhati ya kuandaa mashindano hayo ya vijana.

Natamani kuandaa mashindano hayo, maana vijana wana vipaji vingi ila wanakosa sehemu ya kuvionyesha. Nashindwa kuvumilia kila ninapoona vipaji vinatokomea msituni, wakichimba mawe au kukata mkaa.
 Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu

Inauma kuona wenye vipaji vyao wanaishia kulala kwenye vichaka, maana hakuna mwenye lengo la kuwaendeleza. Huu ndio ukweli.  Wilaya ya Handeni, imesheheni vijana wenye vipaji.

Watoto hao wa masikini wanacheza soka la uhakika. Lakini wanakufa njaa. Hakuna hata Kombe la Mbuzi linaloweza kuwaweka sawa wachezaji na kutafuta maisha ya juu zaidi kutokana na michezo.

Kama kila diwani au Mbunge angeandaa ligi yenye ubora katika wilaya hiyo, mambo yangekuwa mazuri zaidi. Najua wapo watakaosema kwanini iwe Handeni tu na sio wilaya nyingine?

Tatizo ni mwanzo tu. Kila mmoja sasa na afanye juhudi zake kwa nafasi yake ili kuibua vipaji na kuendeleza maisha ya wachezaji hao. Kama kila Kata ingekuwa na kombe imara, basi mambo yangekuwa mazuri.

Wilaya ya Handeni yenye kata 19 inaweza kuboresha maisha ya vijana kama kungewa na mipango ya dhati. Ligi ya Kata itakayozaliwa ya wilaya. Sipati picha hali ingekuwaje na vipaji vingetangazwa vipi.

Ndio maana nasema natamani kuanzisha ligi ya Handeni, ingawa mfuko wangu unanisuta. Nimeamua kuandika hivi, nikiamini wale wenye uwezo wao ni wakati wa kulifikiria hilo kwa kina.

Kila Kata ifanye mchanganuo wake kwa ajili ya kuwa na mashindano ya vijana yenye nguvu, ambayo naamini vipaji vyao vitaongezeka na kupata nafasi ya kuvionyesha machoni mwa watu.

Zipo timu nyingi mno ila jinsi ya kufika huko ndio tabu. Sio Handeni tu bali na wilaya zote za Tanzania kuwa na mipango hiyo ambayo kwa hakika ni dalili njema za kutangaza vipaji vya watu wao.

Sio Handeni tu katika Mkoa wa Tanga, bali mipango hiyo iwe ya nchi nzima. Wakifanya hivyo, nadhani mambo yatakuwa mazuri zaidi. Tutakuwa na wanamichezo mahiri na sio wachache wanaojulikana sasa.

Juhudi hizo zitakuwa na matunda makubwa, maana ukiangalia kwa sasa, vipaji vyote vya mikoani huko, vinaishia kwenye kukata mkaa au kulima kwa jembe la mkono, ingawa Mungu aliwapa vipaji.

Huo ndio ukweli wa mambo. Ningekuwa na uwezo huo ningefanya sasa, maana kwakweli nimeshindwa kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kuona vipaji vinafanyiwa mzaha. Itakuwaje?

Je, ni kweli tumeamua kuzalisha wanasiasa wengi na sio wanamichezo? Kama sio kweli, basi upo mbali na uongo. Tuamuwe sasa na kuvaa vibwebwe kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya Watanzania wenzetu.

Kwakuwa najua ubora wa vipaji vya wananchi hao wa Handeni, naamini wanakufa na vipaji vyao, maana hakuna mpango wa kuwaendeleza na kuwapatia maisha bora kwa kupitia michezo.

kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment