Pages

Pages

Sunday, December 09, 2012

MGODI UNAOTEMBEA



 Watanzania wanahitaji hoja, si vurugu
 Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA chochote cha siasa lazima kijiendeshe kwa taratibu na sheria, bila kuweka mihemko ya aina yoyote itakayosababisha kuvuruga mustakabali wa Taifa hili linalodaiwa kuwa masikini wa kutupwa.

Nasema hivyo kwa kujua kuwa huo ndio mpango wa kukuza uchumi wetu. Huo ndio mkakati wa kuweza kuwakomboa Watanzania na sio kuwadidimiza zaidi, maana wanasiasa wao wanajadili machafuko.

 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Chama cha aina hiyo, kinachojadili hoja nzuri za kuwakomboa Watanzania, kinahitaji ‘sapoti’ na watu wote na sio kuvikumbatia vile ambavyo wanatumia nafasi zao vibaya na kuwaweka watu mtegoni.

Najua ninachokisema, ingawa sina imani kuwa kutakubaliwa na watu wote, hasa wale wanaopenda kuwaza kama wanavyowaza wao. Hilo ni jambo ambalo haliwezekani. Tutofautiane fikra na mtazamo kwa ajili ya kujenga Taifa letu.

 Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba

Hivi karibuni, nilipata kumuona Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, akijadili hoja, namna ya kuwakomboa Watanzania kutoka katika dimbwi la ufukara.

Lipumba alitumia muda mwingi katika mkutano wao uliofanyika Viwanja vya Jangwani kusema namna ya kukuza uchumi wa Mtanzania.

 Askari wakionekana wamejipanga imara kwa ajili ya kuzuia vurugu zinazoweza kujitokeza katika mikutano ya kisiasa katika baadhi ya mikoa yetu hapa nchini.

Nitakuwa mchoyo wa fadhira kama sitamsifia mwanasiasa huyo, licha ya kuwa na kasoro zake za kibinadamu.

Hata kama atakosolewa kwa tofauti ya kivyama, lakini kichwani mwake kumekuwa kukitoa majibu sahihi ya maisha bora kwa kila Mtanzania, ingawa baadhi yao wataona CUF imekufa.

Sijaona akitoa matamshi ya kuibua vurugu kwa kutumia nafasi yake ya uenyekiti, jambo linalotakiwa kuigwa na wote, wakiwamo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao kwa bahati nzuri, wanaaminiwa na Watanzania wengi.

Kwa bahati mbaya, wasioliafiki zaidi ni wale waliokuwa upande wa pili, yani Chadema, inayoongozwa na mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk. Willbroad Slaa, aliyegombea Urais mwaka 2010 na kuangushwa na Jakaya Mrisho Kikwete, aliyetetea kiti chake.

Mbowe na viongozi wake wengi katika chama chao wamekuwa wakipanga zaidi namna ya kulikomboa Taifa kwa njia ambayo si salama. Hili likisemwa, tutaambiwa kuwa eti tunahitaji vyeo katika serikali ya Rais wake, Jakaya Mrisho Kikwete.

Si kweli. Na kama tutakuwa na mawazo ya aina hiyo, basin chi haiwezi kwenda. Wopte tutaogopa kuwakosoa viongozi, wanasiasa na watu wengine kwa madai kuwa watatona vikaragosi vya wengine.

Kuna msomaji wangu mmoja wa Mgodi Unaotembea alisema kuwa eti nipo katika kundi la wanaoendeshwa kwa rimoti. Akasema sitaweza kuikosoa CCM kwa nguvu zote, zaidi ya kuisema Chadema.

Nikamshangaa yeye na mtazamo wake ulioganda. Namnukuu msomaji wangu huyo mwenye namba iliyoishia na 036. “Unajitahidi kuipamba CCM na viongozi wake. Ongeza bidii ukuu wa wilaya utaupata tu”. Haya ni mawazo mgando.

Kwa wasomaji wangu haswa, wanaelewa kuwa sijawahi kuwa upande na mtu yoyote, zaidi ya kukisimamia ninachokiamini. Chadema wenyewe nimeshawakosoa na kuwasifia pia, kama nifanyavyo kwa CCM na CUF.

Hata hivyo naheshimu mawazo ya msomaji wangu. Pamoja na kumheshimu, ila hakunifanyi nione zuri zaidi ni kuchekea wanasiasa ambao malengo yao  ni kupata nafasi za uongozi kwa njia ya mkato.

Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na vyama vingine vya siasa, waandae mikakati yao na kuisimamia, kabla ya kusambambaza watu wa kuhubiri kuitwaa nchi 2015 kwa njia yoyote ile.

Hilo haliwezekani. Ukiangalia kwa haraka, utangudua kwamba Chadema wamekuwa wakijiendesha vibaya. Amani kwao sio jambo jema. Wapo tayari kuvunja sheria, wakiamini kuwa mvuto wao kwa wanachama wao na wafuasi wao wengine, utawafanya viongozi wa serikali washindwe kuchukua uamuzi mgumu.

Kwa mfano, Mbowe wa leo anaweza kufanya mkutano wake bila kufuata kibali alichopewa na jeshi la polisi. Inajulikana kana kuwa mikutano yote, mwisho wake ni saa 12 jioni.

Lakini baadhi ya wanasiasa wetu wa Tanzania, hasa Chadema, wanaweza kufanya mkutano wao nje ya muda walioambiwa. Na kama askari wanapoamuru mkutano huo usitishwe, wanagoma.

Utaona jinsi gani wanasiasa hao wasivyostahili kuchekewa, hata kama tunawapenda ama ni maswahiba zetu. Tuwe wa kwanza kusimamia sheria zetu, ili tuweze kuongoza Taifa hili kwa amani na usalama.

Ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha Amani, basi wanasiasa wawe wa kwanza kutii sheria walizoweka wenyewe. Hakuna ubishi kuwa Chadema kinakubalika kwa sasa. Na kama kikifanya mikutano yake huku ikitetea amani, sidhani kama wananchi wao watashindwa kuwapigia kura.

Muda uliobaki kwa Chadema ni kuongeza wafuasi wale wanaoona kuwa chama hicho kina mapungufu kama hayo ya kutangaza vurugu katika mikutano yao. Viongozi wao wawanyekee wananchi badala ya kuwalazimisha polisi watumie mabomu ya machozi au ya moto na kutoa roho za wenzao.

Lazima tuelewe kuwa chochote kinachofanyika sasa, hakika kitajirudia mbele ya safari. Chadema wanapovunja amani leo, hata kesho watakapoingia Ikulu, vyama vingine vya siasa vitatumia mwanya huo ili wapate ridhaa ya kuingia Ikulu.

Ugumu wa maisha, ndio unaowafanya Watanzania wengi wakubali kufanya maandamano hata yale haramu, wakiamini kuwa huo ndio mpango wa kuwakomboa siku za usoni.

Kwa bahati mbaya, wanasiasa wanaowahangaikia, napata wakati mgumu kuamini kweli wana ndoto za kuwakomboa walalahoi. Kama huo ndio ukweli basi hata leo hii Chadema ikiingia Ikulu, migomo, maandamano na  machafuko katika Taifa hili itashika hatamu.

Huyu atashika panga na yule jiwe kwa ajili ya kuwapopoa viongozi waliokuwa madarakani, ambao hapana shaka watakuwa Chadema, CUF na wengineo, kama CCM itaanguka kama wenyewe wanavyotaka iwe.

Hata CCM wanajua kuwa upinzani unazidi kushika kasi. Wanaelewa pia, wananchi wengi wamewachoka baada ya kuongoza taifa hili tangu Uhuru. Lakini, ki nachoendelea kuwaweka madarakani, ni kuhubiri kwao amani.

Kutoa nafasi kwa kila mtu na sio kubebana kaka na dada au mjomb a na shangazi katika nafasi muhimu. CCM wanafanya hayo kwa kufuata njia ya waasisi wa Taifa hili, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wakati leo Morogoro kunapokuwa na vurugu na kugharimu roho ya mtu, sio kama wananchi wote wamependezwa na suala hilo, hata kama wakiambiwa chanzo chake ni polisi wa CCM .

Wapo watakaojua chanzo chake ni Chadema kufanya mkutano, maandamano bila kufuata sheria au maoni ya vyombo vya usalama. Mbaya zaidi, wanakataa hata ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa, John  Tendwa.

Chadema wameambiwa kama wakiendelea tabia zao za machafuko kwenye mikutano yao, chama chao kitafutwa kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha vyama vya siasa hapa nchini.

Badala ya kujisahihisha, Chadema wanaingilia kati na kumkosoa mwenyekiti huyo, wakisema ajaribu kukifuta aone. Hapa Chadema wanategemea nini kama sio mgongo wa wananchi wasiojitambua.

Chadema wanajua kwa sasa wanakubalika. Hivyo kitendo cha kufutwa kwa ubabaishaji wao, ni mwanzo wa kuitisha maandamano makubwa zaidi, huku wakiamini watu wao wasiojua namna gani watayaweka maisha yao rehani wataingia barabarani, wakionyeshwa kukerwa na uamuzi huo.

Hata hivyo, Chadema na vyama venye mtindo huo, vinajidanganya kwamba Watanzania wote wameichoka amani yao. Huo ni uongo. Wapo wengi wanaopenda amani iendelee kuwapo kwa Watanzania wote.

Uwezo wa kupita mtaa hadi mtaa, nyumba hadi nyumba kukosoa mwenendo wa chama hicho upo, tena kwa kiasi kikubwa, hivyo kukibomoa zaidi chama hicho cha upinzani kinachoshika nafasi ya kwanza kwa sasa.

Ndio maana nasema, wanasiasa wa Tanzania, wana kila sababu ya kuangalia amani ya Taifa letu, kabla ya kutanguliza mbele maslahi ya matumbo yao kwa kuitisha mikutano feki yenye kuleta balaa.

Kila mwanasiasa ajuwe kutoa hoja zinazoeleweka, badala ya kusimama jukwaani kukosoa wenzao kwa ajili ya kuonekana zaidi.

Unaposema serikali ya CCM haina jipya, wewe ongea namna ya kuwapatia maisha bora Watanzania kwa kupitia chama chako na sio kusema itang’oka itake isitake.

Nani kasema Watanzania wote leo hii wanaipenda Chadema au CUF? Kila mtu ana mapenzi na chama chake. Na lazima tujuwe idadi kubwa ya watu wanaohudhuria katika mikutano hiyo, sio kama wanakipenda.

Wengine wanakwenda kupiga porojo na baadaye hukaa wanapopenda. Hivyo basi huu ni wakati wa wanasiasa wetu kujiendesha kwa kutumia akili zaidi. Tanzania ni nzuri zaidi kuliko chama chochote cha siasa.

Leo hii CCM itaondoka madarakani lakini Tanzania itaendelea kuwapo. Tusione haya kuambiana ukweli, hasa hili la kushuhudia jinsi barafu ya amani yetu linavyozidi kuyeyushwa na wanasiasa wenye mihemko.

Hili lipo kwa vyama vyote, bila kuangalia amefanya John Mnyika, mbunge wa Chadema au Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, au Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais, wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK).

Mwanasiasa anayetoa matusi, kuzungumzia umasikini bila kusema namna ya kuundosha, kutangaza hatari na serikali iliyokuwa madarakani, huyo hana hoja zaidi ya kutegemea mgongo wa walalahoi.

Huo ndio mtaji wao kisiasa. Hana njia nyingine zaidi ya hiyo, hasa katika Tanzania ya leo ambayo wengi wanaibuka huku wakiamini CCM imeshindwa kuwaongoza na ipo haja ya kuwaweka wapinzani, wakiwamo Chadema madarakani.

Mawazo yao mazuri, ingawa yanaendeshwa tofauti, huku ile hamu ya kuleta siasa za vyama vingi kwa nchi yetu kutoka kwa kasi ya ajabu, maana ndugu zetu wanapoteza maisha sababu ya vyama hivyo.

Kuchekea kinachofanywa na wanasisa hao leo hii ambapo vijana wengi wanaamini CCM sio chama cha kuwakomboa, ni kubariki machafuko yatakayotuacha kwenye majonzi makubwa, huku mtaji wao wanaotegemea ni wale wananchi wenye mawazo ya kuishi kwa mlo mmoja na chuki zao nyingi wakizielekeza kwa serikali ya Jakaya Mrisho Kikwete, aliyeingia madarakani mwaka 2005.

JK aliingia madarakani akiwa na kauli mbiu zake kama vile maisha bora kwa kila Mtanzania, ingawa hadi sasa, umasikini kwa watu wake umezidi kuwa tishio, huku vijana wengi wakikosa ajira.

Hili Kikwete analijua, ndio maana watendaji wake wanahaingikia kulitatua, maana yeye peke yake hawezi. Wapinzani nao wanatakiwa kulifanyia kazi hilo kwa kutokana na wabunge wao, madiwani wao pamoja na mawaziri kivuli.

Zaidi ya hapo tutapiga porojo usiku na mchana, huku silaha kubwa inayotumiwa ni ile, CCM wameshindwa kuongoza, wananchi waitenge serikali yao, huku wakifika mbali zaidi kwa kutajwa kuhusika kwenye migomo ya wafanyakazi nchini.

Njia tunayopita kuelekea mabadiliko ya kisiasa siyo nzuri, itagharimu roho za Watanzania wengi, hivyo ipo haja ya kujitazama upya na kuhubiri siasa za amani kwa ajili ya watu wote.

Kinyume cha hapo, ni kweli nchi haitatawalika kutokana na wanasiasa wenye machungu na matumbo yao.

Mungu ibariki Tanzania.

0712 053949
0753 806087

Makala hii iliwahi kutumika katika Gazeti la Mtanzania, kwenye safu yangu ya Mgodi Unaotembea, inayotoka kila Jumatano.
 

No comments:

Post a Comment