Pages

Pages

Thursday, December 27, 2012

Francis Cheka amdunda Mmalawi jijijini Arusha



Francis Cheka akipima uzito
 
Na Rahimu Kambi, Arusha
BONDIA mwenye makali ya kutisha hapa Tanzania, Francis Cheka, jana usiku aliendeleza ubabe wake baada ya kumtandika kwa pointi bondia kutoka Malawi, Chimwemwe Chiotcha na kuleta shangwe kwa Watanzania.

Pambano hilo lilipigwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na Cheka kushinda kwa pointi 118 kwa 114, 114 kwa 112 na pointi za mwisho kutolewa ni 120 kwa 115 dhidi ya Mmalawi huyo aliyekutana na mbabe wa Tanzania.
Mmalawi Chimwemwe Chiotcha

Ushindi wa Cheka ni mwendelezo wa makali yake hasa akiwa na hamu zaidi ya kucheza mapambano ya Kimataifa, baada ya kuona Tanzania amekosa mpinzani na kuwapiga kila siku mabondia wazawa.

Kwa siku kadhaa, Cheka alikuwa akijiwinda kwa ajili ya pambano hilo lililokuwa na upinzani wa hali ya juu, kwani ingawa ameshinda, lakini Mmalawi huyo hakuwa lele mama na kulazimisha apigwe kwa pointi.

Pambano hilo lilikuwa na upinzani wa hali ya juu, kwani tangu asubuhi walipokuwa wakipima uzito katika Hoteli ya Naura Springs, wababe hao walikuwa wakionyeshana umwamba na shari ya kutaka kudundana kavu kavu.

Hali hiyo iliongeza joto na msisimko wa pambano hilo lililomalizika usiku katika Uwanja huo na kuleta shangwe kwa Watanzania, kutokana na bondia wao mwenye maskani yake mjini Morogoro kuendeleza majigambo yake kwa kutoa dawa kwa kila anayekutana naye.

No comments:

Post a Comment