Pages

Pages

Wednesday, December 26, 2012

Dkt Kigoda aifurahia barabara ya Mkata-Handeni


Mbunge wa Handeni, Abdallah Kigoda

Na Mashaka Mhando, Handeni
MBUNGE wa Handeni mkoani Tanga, Dk. Abdallah Kigoda, amesifu ukamilikaji wa barabara ya Mkata hadi Handeni iliyojengwa na serikali kwa kiwango cha lami hatua ambayo amesema itarahisisha mawasiliano kwa wananchi wa wilaya hiyo.

"Kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yangu, nimetembelea Jimbo langu kutoka nyumbani kwangu mjini Handeni, kwenda Mkata na kufanya mikutano ya hadhara, nikarudi kwa kupitia njia ya lami pekee, ni faraja kubwa sana, tuitunze, haya ni moja ya maendeleo ya wilaya yetu hii" alisema Dk Kigoda.

Dk Kigoda ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, aliyasema hayo juzi alipokwa kwenye ziara yake ya kukagua utekelezwaji wa ilani ya uchaguzi wilayani humo kwa kufanya mikutano katika kata ya Mkata ikiwemo kukutana na wapiga kura wake.

"Haikuwa kazi rahisi kufanikisha kupitisha bajeti ya ujenzi wa barabara hizi za Handeni-Mkata, Handeni-Korogwe na Handeni-Mvomero. Namshukuru sana Rais Jakaya Kikwete pamoja na Bunge kwa kuweza kupitisha ujenzi wake," alisema Dk Kigoda.

Alisema anapotumia barabara hizo amekuwa akiwafikiria watu wake wa karibu, ambao walipigania kupata barabara hizo kwa kiwango cha lami. Lakini sasa hawapo tena duniani, hivyo alitamani nawao waone matunda ya kuwa na subira.

Kuhusu suala la maji mbunge huyo alisema wanakabiliwa na mkakati mzito wa kujenga upya Mradi wa Maji wa Handeni Trank Man (HTM), wa kutoka mto Pangani (Ruvu) ili wananchi walio wengi waweze kuondokana na kero ya maji.

Waziri huyo alisema changamoto kubwa iliyobaki wilayani humo sasa ni upungufu wa maji, akisema kwa hesabu ya mwaka jana 2011, Handeni ilikuwa inahitaji kiasi cha Sh 120 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo wa HTM ambao tangu umejengwa mwaka 1978 na rais wa sasa wakati huo akiwa Waziri wa maji, haujafanyiwa ukarabati.

Alisema hata hivyo wanaendelea na jitihada za kutafuta wafadhili na Bajeti ya Serikali, ambapo wanaendelea kuchimba visima virefu na vifupi pamoja na mabwawa katika maeneo mbali mbali ili kupunguza makali ya uhaba wa maji kwa wananchi.

Dk Kigoda aliwashukuru na kuwapongeza wafanyabiashara wilayani humo hasa wa mjini Handeni, kwa kuiunga mkono Serikali kuchimba visima virefu ambavyo vimesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza shida ya maji mjini hapa, ambapo sasa ndoo ya maji huuzwa Sh 100 visimani, badala ya Sh 500 za awali.

No comments:

Post a Comment