Pages

Pages

Monday, October 15, 2012

Wema, Aunt Ezekiel wawaomba radhi Watanzania


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WASANII wawili wa filamu wenye majina makubwa hapa nchini, Wema Sepetu na mwenzake Aunt Ezekiel wamewaangukia Watanzania kwa kusema hawajajua kama watawakera watu haswa baaada ya picha zao kuzagaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari.

Wema na Aunt walipokuwa katika ziara ya tamasha la Fiesta, walipigwa picha za utupu, walipokuwa jukwaani hivyo kuwakera watu wengi, ukizingatia kwamba wao ni kioo cha jamii na wanastahili kuishi kwa staha na sio kuanika nyeti zao.



Hivi ndio vivazi vya Wema Sepetu kushoto na Aunt Ezekiel kulia vilivyozua balaa hadi kuomba radhi leo kwa Watanzania, katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo. Katikati ni JB wakati wapo kwenye shoo ya Fiesta ya mjini Moshi.


                                          Wema Sepetu akiomba radhi kwa Watanzania

Wema na Aunt Ezekiel waliitumia siku ya jana katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuzungumza na waandishi wa habari, ili wafikishe vilio vyao, wakisindikizwa na Katibu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAF), Willsona Makubi pamoja na msanii mwingine wa fgilamu, Tino Muya.

Akizungumzia sakata hilo, Wema alisema hawana uzoefu wa kupanda katika majukwa makubwa, hivyo baada ya kufanya hivyo, baadhi ya wapiga picha na wananchi wengine waliingia kwenye kazi hiyo na kusambaza picha zao.

“Sikujua kabisa kama picha zangu zingezagaa kwenye mitandao maana sina uzoefu huo kama waliokuwa nao wasanii wengine wa muziki wanaopanda jukwaani kila wakati, ila kwa sasa nimejua na naamini sitawakera tena Watanzania.

“Nipo chini ya miguu yao na mkawaeleze kwamba tabia yangu inawachosha pia hata ndugu zangu, maana nao ni waathirika kwakuwa wanazipata kwenye vyombo vya habari na jinsi ninavyoonyeshewa vidole,” alisema Wema.

Naye Aunt alisema tangu sasa amekuwa msanii mpya naa kioo cha jamii, maana atajilinda katika kila jambo analofanya ili aendelee kuheshimiwa na kutumainiwa kama msanii mwenye dhamana na kutangaza utamaduni wa Mtanzania.

Huku akiwa na masikitikio makubwa, Aunt alisema,“ Hata mimi na mwenzangu Wema tunapata tabu sana, hivyo tuliamua kukutana na viongozi wetu ili tutumie fursa hii kuzungumza na nyie tukijua fika mtafikisha vilio vyetu kwa Watanzania wote,” alisema mwanadada huyo ambaye jana alivaa vazi la heshima na kuahidi kuwa mtu mwenye maadili.

Akielezea sakata hilo, Makubi alisema wanaamini wasanii hao watafuata maadili ya Mtanzania katika kujiheshimu katika maisha yao yote, ndio maana baada ya tabia zao kuwa mbaya waliamua kujishusha na kutaka suluhu na jamii yao.

“Wasanii hawa wasamehewe na naamini watakuwa watu wenye maadili kuanzia hapa, hivyo ni jukumu letu kujua kuwa kadri siku zinavyokwenda wanazidi kupanuka kiakili na kujua wataacha tabia zao za kukera,” alisema.

Katika tamasha la Fiesta liliiofanyika katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, wasanii hao waliambatana kwenye ziara hiyo na kupanda jukwaani kuwasalimia mashabiki wao, jambo ambalo hata hivyo liliwakera baadhi ya watu baada ya kupanda na vivazi vya utupu na kujiachia jukwaani hivyo kupigwa picha mbaya.

No comments:

Post a Comment