Pages

Pages

Monday, October 15, 2012

Tumeshindwa werevu, tujifunze na ujinga

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI aibu kila siku kuendeleza kilio kile kile cha ubabaishaji wa soka la Tanzania, linaloongozwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF). Wadau wa michezo wamekuwa wakilia sana juu ya uendeshaji mbovu wa soka, hasa uamuzi wa utata wa marefa, timu kutumia fedha nyingi, rushwa katika kusaka ushindi kwenye mechi zao.
 
Ratiba isiyokuwa na mashiko kwa baadhi ya timu, huku wasimamizi wa soka, wakiwa wepesi wa kuangalia zile mechi zenye faida, yani zinapokutanisha timu za Simba na Yanga.
 
Ni kama vile tumeshindwa werevu, hivyo walau sasa tujifunze na ujinga katika kudidimiza zaidi soka letu, maana sioni mipango inayoweza kuinua michezo, ukiwamo mpira wa miguu unaopendwa kwa kiasi kikubwa hapa nchini.
 
TFF inayoongozwa na Rais wake, Leodgar Tenga, akiwa na watendaji wake wengine, kama vile Angetile Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni na wengineo, wamekuwa hohe hahe hadi kuchelewesha Kampuni ya kuendesha ligi.
 
Haya yanasababisha ligi na mpira wa miguu kwa ujumla kuwa wa kusua sua, maana yale yanayofanywa leo ndiyo yale yale yaliyolidumaza soka la Tanzania, huku likiachwa na nchi nyingine, kama vile Kenya, Uganda na kwingineko.
 
Leo hii timu ya Taifa ya Tanzania, inafanya kazi kubwa sana kuweza kuibuka na ushindi katika mechi zake zinapokutana na nchi za Uganda na Kenya. Lakini, timu hizo ni zile zilizokuwa zinafungwa mara kwa mara na Taifa Stars.
 
Ukiyasema haya, watashindwa kukuelewa, hivyo kuchelewesha kwa kiais kikubwa maendeleo ya michezo hapa nchini. Angalia, ligi kutoendeshwa na Kampuni kama invyotakiwa na wadau, kunaroa ladha halisi.
 
Watu wanajiendesha wanavyotaka wao. Timu inajiandaa na mechi yake, lakini inapelekewa barua ya haraka, ikitangaza kusogeza mbele au kurudisha nyuma mechi husika. Timu ya African Lyon, inazuiliwa kudhaminiwa na Kampuni ya Zantel, maana ligi ipo chini ya Kampuni ya Vodacom Tanzania.
 
Sawa, ila fedha zinazotolewa na vodacom zinatosha k,wa timu hizo? Kama zinatosha, je, hao Vodacom wanazitoa kwa wakati? Kumekuwa na ghiriba nyingi katika uendeshaji wa ligi ya Tanzania, hivyo kusababisha kutoelewana.
 
Kwa mfano, baadhi ya timu ikiwamo African Lyon zinalalamika kuwa hawajashirikishwa katika udhamini huo wa Vodacom. Wanfika mbali zaidi kwa kusema kuwa hawajapa nafasi ya kuangalia aina ya mkataba huo.
 
Pamoja na hayo, mkataba wa Vodacom na TFF juu ya ligi hiyo ulisumbua kwa wiki kadhaa, hadi kuchelewesha kutoka kwa ratiba na kuanza kwa ligi hiyo. Haya ni maajabu makubwa na matatizo ya ligi hiyo ya Tanzania Bara.
 
Ukiangalia kwa haraka, yote hayo ni majibu kuwa ligi haiwezi kuwa na tija kama kutakuwa na malalamiko ya kupitiliza. Timu zinalalamikia ukandamizaji huo ambao kwa kiasi kikubwa unachekewa na hao TFF.
 
Nalisema hili bila kuficha, maana ni ajabu ya mipango yenye matege. Tutawezaje kuwa na wachezaji bora wakati ligi yetu haieleweki? Sisi ni wa hapa hapa kwanini tunakuwa na mipango ya kucheza Kombe la Afrika au Dunia?
 
Hii ni aibu kubwa. Ndio maana hata ukiangalia mechi hizo, utagundua kwamba hakuna mikakati wala ufundi zaidi ya ushindi wa lazima. Kwa wale wenzetu wa Simba na Yanga ndio kabisa.
 
Kwanza wana mtaji mkubwa wa mashabiki na wanachama wenye  nazo hivyo kuweza kufanya lolote wanalohitaji. Haya lazima tuyaangalie upya. Tuwe na dhamira ya kweli na kuacha udanganyifu, ubabaishaji katika kuinua michezo.
 
Kunyume cha hapo hatutakuwa na jipya katika uendeshaji wa soka, ndio maana Taifa linaachwa nyuma na harakati za nchi nyingine za Afrika juu ya kuendeleza michezo.
 
Sikatai Taifa lina wachezaji imara na wenye vipaji vya hali ya juu, ingawa nao wanaangushwa na aina ya viongozi wa soka la Tanzania. Ubabaishaji ni mkubwa katika kila nyanja, ikiwamo uwanjani na usajili kwa ujumla.
 
Kumekuwa na janja janja nyingi, huku Simba na Yanga zikisikilizwa kupita kiasi, ingawa ukisema hili watakataa. Huwezi kubisha kuwa tuna vijana mahiri lakini hawawezi kusonga mbele kama hatutakuwa na mipango endelevu.
 
Wachezaji kama vile Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, Nurdin Bakari, Juma Nyoso, Nadir Haroub Canavaro, Haruna Moshi Boban na wengineo wana vipaji vizuri na wanaweza kufanikisha maendeleo ya michezo hapa nchini.
 
Tatizo hawawezi kwenda mbele bila kuongozwa na hao wanaowaongoza ndio wameoza kabisa. Haya lazima yasemwe kama tuna lengo la kuboresha soka letu. Huo ndio ukweli wa mambo.
 
Vinginevyo tutakuwa tunacheza soka la nyumbani bila kuwa na maendeleo yoyote, inagwa Mataifa mengine yanazidi kuchanja mbuga. Viongozi wa soka kuanzia ngazi ya klabu, mikoa na Taifa kwa ujumla wajipange katika hilo.
 
Wasiopenda kasi ya mabadiliko wawekwe kando kwa ajili ya Tanzania. Nasema hivyo huku nikiamini kuwa mashabiki wanaopenda soka ni wengi mno. Ukitaka kuhakikisha hilo, hudhuria mechi za Simba, Yanga au timu ya Taifa.
 
Kama mipango itawekwa, basi soka la Tanzania litapanda kwa timu zetu zote, kama vile Coastal Union, Kagera Sugar, Azam FC, Mtibwa Sugar, African Lyon, Toto African na nyinginezo, hivyo kuingiza mashabiki wengi katika mechi zao.
 
Mashabiki wa soka hawatachagua tena mechi za kuingia. Wataingia kwa kila mechi, maana wanapokwenda huko wanapata kitu kizuri. Nasema hivyo kwasababu, leo hii mashabiki wanaingia kwa Simba na Yanga kwakuwa ndio timu zao wanazopenda.
 
Hawapendi soka lao, ila wanapenda timu hizo kongwe. Kama hivyo ndivyo, tunawezaje kuwabadilisha watu juu ya mtazamo wao? Hakika ni mikakati. Mipango imara pamoja na kuacha ubabaishaji katika aina ya viongozi wetu.
 
Sheria zifuatwe na dhamira ya kweli iendelee kuwekwa kwa ajili ya kuinua kiwango cha michezo kwa nchi yetu. Huo ndio ukweli wa mambo. Tusipofanya hivyo, tutajiweka kwenye mtihani na kulaumu wakati hatuna mikakati.
 
Hakuna mtu asiyejuwa mambo mazuri ya kufanya. Wote waliokuwapo kwenye nafasi za uongozi wa soka, hakika ni wenye akili zao timamu. Hivyo watumie vichwa vyao kubuni na kuendeleza mambo yenye tija kwa Taifa letu.
 
Nasema haya kwa kujua kuwa tumekuwa na mapungufu mengi katika uendeshaji wa soka letu, hivyo nadhani huu  ni wakati sasa wa kujifanyia marekebisho kama kweli ipo chembechembe za kuinua soka la Tanzania.
 
Kwa sasa, bila kuangalia ni Simba inayoongoza ligi, Azam FC, Yanga, Mtibwa Sugar, ila hakuna soka linalosuuza nyoyo za watazamaji zaidi ya wengi wao kutumia rushwa aidha ya fedha au ya mapenzi yao kwa timu hizo, hasa hizo kongwe.
 
Kama tumeshindwa werevu sio mbaya tukiendelea kujifunza na ujinga, ila wasipite watu vichochoroni wakijifanya wana uchungu na soka letu, maana wakati huu wapo kimya wakiendelea kutafuna kile wanachopata.
 
Wakati ni huu. Tujisahihishe ili kulifanya Taifa lisiwe kichwa cha mwendawazimu kama alivyowahi kusema, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
 
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment