Pages

Pages

Friday, April 06, 2018

Wazanzibar waaswa kuwa wazalendo na nchi yao

Na Mwandishiwetu, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dkt. Ali Mohamed Shein  amewaasa vijana wa Zanzibar kuwa Wazalendo na nchi yao  kwa kuisoma na kuijua historia ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuenzi mchango wa Mwasisi wa Taifa hilo Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Dkt. Shein  ameyasema hayo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi katika  kongamano la kwanza la kumbukumbu ya Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa kwanza wa Baraza la mapinduzi Hayati Sheikh Abeid Amani Karume,  lililofanyika katika Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere   katika kampasi ya Zanzibar, iliyopo Bububu  mjini Magharibi siku ya Alhamis tarehe 5 April, 2018.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dkt. Ali Mohamed Shein akitoa hotuba ya ufunguzi wakati wa kongamono la kumbukumbu ya hayati sheikh abeid amani karume lililoandaliwa na chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere kampasi ya zanzibar.


“Hayati Sheikh Abeid Amani Karume,   alikuwa ni mtu mvumilivu na mstahimilivu, aliyeipenda Zanzibar na wananchi wake, hivyo ni vyema mchango wake katika kuleta maendeleo ya Zanzibar ukakumbukwa na kuenziwa.

Rais Karume ametumia fursa hiyo pia kukipongeza Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuona umuhimu wa kuandaa Kongamano hilo ambalo ni la kwanza kufanyika visiwani Zanzibar.

“Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imeandaa Kongamano hilo  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya kuwaenzi waasisi wa Taifa ambao ni Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume ambao wanamchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa,” amesema Rais Shein.

Katika taarifa yake, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere  Prof.Shadrack Mwakalilia  alieleza kuwa Hayati sheikh Abeid Amani Karume alipigania mengi kwaajili ya ustawi wa Zanzibar,  na ndio sababu Chuo kikaona umuhimu wa kuandaa kongamano  hilo kwa lengo la kujikumbusha na kujadili falsafa na ndoto za Sheikh Abeid Amani Karume katika ustawi wa Zanzibar ya leo.

Naye  Mwenyekiti wa bodi ya Chuo Prof.Mark Mwandosya alimuahidi  Dkt. Shein kuwa Chuo kitaendeleza utamaduni wa kufanya makongamano kila mwaka  kwa lengo la kumuenzi  muasisi wa  Zanzibar na  pia  kuwakumbusha vijana historia ya Zanzibar ya sasa kupitia mchango mkubwa uliotolewa na Mwasisi wa Zanzibar Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Mwenyekiti wa Kongamano hilo alikuwa Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Pandu Ameir Kificho ambapo watoa mada walikuwa ni Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Said Ali ambae alitoa mada kuhusu “Fikra za Abeid Amani Karume na mapinduzi ya Uchumi Zanzibar” na Mhe. Mohamed Seif Khatib ambae alitoa mada kuhusu “Fikra za Abeid Amani Karume katika kujenga umoja na mshikamano wa kijamii Zanzibar.
  
Wadau mbali mbali wakiwemo baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walishiriki na kuchangia katika mada hizo.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Shein aliwatunuku vyeti na zawadi wanafunzi wa skuli za msingi na sekondari Zanzibar ambao walifanya vizuri katika shindano la uandishi wa insha kuhusu mchango wa Sheikh Abeid Amani Karume katika maendeleo ya Zanzibar.

Hayati Sheikh Abeid Amani  Karume alifariki April 7, 1972.
  Mkuu wa Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila akisalimiana na Rais wa Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein wakati alipowasili kwenye kongamano la kumbukumbu ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume
   Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo  cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Mark Mwandosya akiongea wakati wa kongamano hilo.
  Waziri wa Vijana,Sanaa, Utamaduni na Michezo Balozi Ali Karume akizungumza wakati wa kongamano hilo.waliokaa ni watoa mada Balozi Amina Salum Ali na Mohamed Seif Khatib
 Mwenyekiti wa kongamano Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar  Pandu Ameir Kificho akiongoza majadiliano  wakati wa kongamano hilo.
 Mgeni rasmi katika kongamano Rais  wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akiwa katika picha ya pamoja na meza kuu pamoja na wajumbe wa bodi ya chuo.

1.     Mgeni rasmi katika kongamano Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akiwa katika picha ya pamoja na meza kuu pamoja na Wanafunzi wa skuli za msingi na sekondari waliofanya vizuri katika uandishi wa insha juu ya mchango wa Sheikh Abeid Amani Karume katika maendeleo ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment