Pages
▼
Pages
▼
Wednesday, December 13, 2017
Serikali yaipongeza Bikosports kuijaza mapesa Stand United
*Waziri Mwakyembe asema mpira ni pesa
*Ataka wadau wengine wawekeze
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni, chini ya Waziri wake, Mheshimiwa Dr Harrison Mwakyembe, ameipongeza Kampuni ya Bikosports kwa kitendo chake cha kuidhamini timu ya Stand United ya Shinyanga kwa Sh Milioni 100.
Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni, Mheshimiwa Harrison Mwakyembe, akiangalia jezi yake aliyokabidhiwa na wadhamini wa klabu ya Stand United ya Shinyanga, Bikosports, wakiwa kwenye tukio la klabu hiyo kukabidhiwa hundi ya Shilingi Milioni 100 kama sehemu ya udhamini kwao. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Bikosports, Charles Mgeta, akiwa sambamba na Mbunge wa Shinyanga Mheshimiwa Steven Masele na kulia ni Mwenyekiti wa Stand United, Dr Ellyson Maeja.
Serikali imetoa kauli hiyo leo katika makabidhiano ya hundi ya Sh Milioni 100, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Akemi na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa serikali, viongozi wa TFF na wadau wengine muhimu wa michezo.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Mwakyembe alisema duniani kote mpira ni pesa, hivyo kitendo cha Kampuni ya Bikosports kuamua kuidhamini Stand kutachochea ari ya mafanikio katika nyanja ya mpira wa miguu nchini.
"Serikali inawapa hongera Bikosports kwa kuingia kwenye mpira wa miguu, hivyo ni matumaini yetu nitaongeza wigo wenu wa udhamini sanjari na kuingia pia kwenye klabu nyingine, tukiamini sasa mpira utachezwa uwanjani, hivyo Stand United lazima waitumie vizuri fursa ya kupata mdhamini," Alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bikosports Tanzania, Charles Mgeta wa kwanza kushoto, akimkabidhi hundi ya Shilingi Milioni 100 mwenyekiti wa klabu ya Stand United ya Mjini Shinyanga, Dr Ellyson Maeja mwenye shati la kitenge, kama sehemu ya udhamini wao kwa timu hiyo. Wengine ni Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni katikati akiwa na Mbunge wa Shinyanga, Mheshimiwa Steven Masele wakiwa kwenye makabidhiano hayo. Picha zote na Mpigapicha Wetu.
Aidha Waziri Mwakyembe alisema wameamua kubadili kanuni za Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambapo sasa kila mtu anaweza kuwekeza kwenye klabu za wanachama, lakini ni lazima awe na hisa zisizozidi 49, huku wananchi wakimiliki hisa 51.
Alisema sharti hilo ni kwa klabu zinazomilikiwa na wanachama, ukiacha timu za watu binafsi, akiamini kuwa masharti hayo hayatapora klabu za wananchi na kwenda kwa wenye fedha, huku akiongeza kuwa wakati klabu hizo zinaanzishwa wananchi hawakujua kuwa kuna siku klabu zao zitamilikiwa na wawekezaji.
"Tumebadilisha kanuni za BMT, ambapo uwekezaji umeruhusiwa lakini kwa masharti ya asilimia 49 ya hisa za mwekezaji na zilizosalia zitabaki kwa wananchi wenye timu zao, alisema Mwakyembe, huku akiwapongeza bikosports na kuwataka wadau wengine waige mfano wao.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bikosports, Charles Mgeta, alisema wameamua kuidhamini Stand United kwa Sh Milioni 100 sambamba na vifaa vya michezo, jambo linaloweza kuleta tija kwa timu hiyo na Tanzania kwa ujumla.
"Tunajivunia kuidhamini Stand United na tunaamini tutaendelea kushirikiana kwa namna moja ama nyingine, hivyo wanachotakiwa kufanya wachezaji na viongozi wa timu ni kucheza kwa bidii ili watuaminishe kuwa kweli uwezo wanao na wanaweza kufanya maajabu katika ulimwengu wa mpira wa miguu.
"Bikosports tuna dhamira ya kukuza mpira na michezo kwa ujumla, hivyo wanachotakiwa kufanya Watanzania ni kutuunga mkono katika mchezo wetu wa kubashiri matokeo ya michezo mbalimbali ili wavune fedha nyingi kutoka kwetu, tukiamini itakuwa ni fursa adimu ya kuiletea maendeleo nchi yetu," Alisema Mgeta.
Awali wakati anazungumza na waandishi wa Habari kwenye makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa Klabu hiyo ya Stand United, Ellyson Maeja, alisema sasa hawana kisingizio chochote isipokuwa kucheza kwa nguvu zote ili kuipaisha timu yao katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Naye Mlezi wa Stand United ya Shinyanga, ambaye pia ni Mbunge wa Shinyanga, Mheshimiwa Steven Masele, alisema bikosports wamekuja wakati muafaka kwa ajili ya kuendeleza klabu za Tanzania, akisema hayo ni matokeo mazuri ya ushirikiano baina ya wananchi wa Shinyanga, viongozi na wadau wote wa michezo nchini.
"Timu yetu ilianzia chini na tumeipeleka kwa tabu, hivyo wale waliokuwa wanadhani eti nimeitupa klabu hii naomba mkawaeleze kuwa nipo na lazima makali ya timu yetu yarudi, ukizingatia kuwa hakuna malalamiko sasa ya kifedha na lazima tukubaliane kuwa fedha hizi tutaziangalia kwa kina ili zilete tija iliyokusudiwa, "Alisema.
Bahati Nasibu ya kubashiri matokeo ya bikosports marufu kama jamvi la Bikosports ni mchezo rahisi kucheza na kushinda, huku ikiwa sio lazima kujisajili, huku kianzio cha kucheza kikiwa ni Sh 500, ambapo namba ya kumbukumbu ni 101010.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa bikosports, mchezo huo unachezwa kwa simu za Tigo Pesa, M-Pesa na Airtel Money huku ukitoa fursa ya nafasi 250 za kiubashiri kama vile magoli yatakayofungwa, mshindi wa mechi, muda wa magoli kufungwa na mengineyo.
No comments:
Post a Comment