Pages

Pages

Monday, January 16, 2017

Watoto wawili waliokufa kwa kukosa hewa ndani ya gari waagwa

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mtakatifu Therese wakitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili wa mwanafunzi mwenzao Maria Masala wakati wa ibada ya kuuaga mwili huo iliyofanyika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Therese Ukonga Madafu Dar es Salaam jana.
Jeneza lenye mwili wa mtoto huyo likiombewa kabla ya 
kuingizwa kanisani
Wanafunzi wenzake na mtoto huyo wakiwa katika ibada ya kumuaga mwenzao.
Padre aliyekuwa akiendesha ibada hiyo akilinyunyuzia mafuta ya baraka jeneza lenye mwili wa mtoto Maria.
Msemaji wa familia ya ASP Masala akitoa taarifa na historia 
fupi ya marehemu Maria.
Baba wa marehemu, ASP Masala (wa pili kulia aliyevaa shati la kitenge), akiwa na ndugu zake na waumini waombolezaji katika ibada ya kuuaga mwili wa mtoto wake kabla ya kuondoka kwenda nyumbani kwao mkoani Rukwa kwa mazishi.
Padre aliyekuwa akiendesha ibada hiyo akilinyunyuzia mafuta ya baraka jeneza lenye mwili wa mtoto Maria.
Watawa wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Therese wakitoa 
heshima za mwisho.
Waombolezaji wakiwa wamejipanga foleni wakati wakienda 
kutoa heshima za mwisho.
Waombolezaji wakiwa katika foleni ya kutoa heshima za mwisho.
Mtawa wa kanisa hilo akisaidiwa baada ya kushindwa kuvumilia uchungu wa kuondokewa na mpendwa wake mtoto Maria.
Ngugu yake Maria akisaidiwa baada ya kutoa heshima 
zake za mwisho.
Baba ya mtoto huyo ASP Masala akilia kwa uchungu wakati 
akitoa heshima zake za mwisho kwa mwanaye.
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mtoto Maria wakati wakitoka katika kanisa hilo.
Jeneza likiingizwa katika gari tayari kwa safari ya kwenda 
mkoani Rukwa kwa mazishi.
Waombolezaji wakiwa wamepigwa na bumbuwazi 
kufuati vifo hivyo.
Ni huzuni na simanzi wakati wa kuuaga mwili wa mtoto huyo.

Na Dotto Mwaibale

WINGU zito vilio majonzi na simanzi vilitanda kutokana na vifo vya watoto wawili wa maofisa wa Jeshi la Magereza waliofariki  dunia kwa kukosa hewa baada ya kujifungia kwenye gari la mmoja wa wazazi wao walimokuwa wakicheza.        

Tukio hilo limetokea juzi jioni katika Kota za Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam, wakati wazazi wao walipokuwa wakitengeneza gari hilo lililogoma kuwaka.

Watoto waliopoteza maisha ni mtoto wa Mrakibu wa Jeshi la Magereza (ASP), Demetrus Masala, aitwaye Maria (6), ambaye alikuwa darasa la kwanza katika Shule ya Mtakatifu Therese Ukonga na Sajini Francis, ambaye ni Esther (4), mwanafunzi wa shule ya awali katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakupenda majina yao yaandikwe kwenye vyombo vya habari kwa sababu si wasemaji wa familia walidai kuwa  watoto hao walipoteza maisha katika gari lenye namba ya usajili T 291 CXR aina ya Toyota Passo ,mali ya ASP Masala.

Mashuhuda hao walidai kuwa siku ya tukio gari hilo liligoma kuwaka na ndipo Masala alipokwenda kumuomba jirani yake ambaye anaishi mlango wa pili Sajini Francis aende kumsaidia kulibusti ambapo alichukua betri katika gari yake ili amsaidie jirani yake huyo.

Ilielezwa kuwa licha ya kuibusti betri ya gari  la ASP Masala haikupokea moto ikiashiria kuwa Alternator ilikuwa ni mbovu kwani ilikuwa haifui umeme.

Baada ya kushindikana kuiwasha gari hilo waliamua kuachana nalo na kushauriana ASP Masala aende kumfuata fundi na ndipo alipolifunga gari lake na kuondoka pasipo kujua watoto wao walikuwa ndani ya gari hilo kwani walipokuwa wakilitengeneza walionekana wakiwa pembeni yake.

Wazazi hao hawakujua watoto hao waliingia saa ngapi ndani ya gari hilo lakini ilidaiwa kuwa awali wakati wakicheza jirani na gari hilo waliwafukuza ambapo baadae waliingia tena bila ya wao kufahamu hasa kutokana na gari hilo kuwa na vioo vya giza isipokuwa cha mbele ambapo walikuwemo ndani ya gari hilo kuanzia saa 7 mchana hadi saa 11 jioni.

Ilidaiwa kuwa baada ya kukaa kwa muda mrefu Francis ambaye ni dereva ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali alibaini watoto hao wawili hawaonekani katika eneo hilo ndipo walipoanza kuwatafuta katika nyumba za jirani bila mafanikio.

Inadaiwa wakati wakiendelea kuwatafuta kuna kijana aliwadokeza kuwa wakati gari hilo likiendelea kutengenezwa watoto hao walikuwa ndani ya gari hilo.

Kauli hiyo inadaiwa ndiyo iliyomshtua Francis na kuamua kuchungulia ndani ya gari hilo ambapo waliwaona watoto hao wakiwa wamekaa siti ya nyuma wamelala fofofo huku mwingine akivuja damu puani.

Hali hiyo ilisababisha Francis na watu wengine waliokuwepo eneo hilo kusogea na kuvunja kioo kidogo cha gari hilo na kuwatoa watoto hao wakiwa katika hali mbaya.

Imedaiwa kwa sababu ya hali waliyokuwa nayo waliamua kuwakimbiza katika Hospitali ya Kardinal Rugambwa Ukonga kwa ajili ya matibabu ya haraka lakini hata hivyo walibaini mtoto Maria tayari alikuwa amekwisha fariki dunia.

Madaktari walijaribu kumpa huduma ya kwanza mtoto Esther kwa kumuongezea Oksjeni na baadaye walimkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Ilala ya Amana ambapo naye walibaini kuwa tayari alikuwa amekwisha fariki.

Baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki la Ukonga la Mtakatifu Therese wakizungumza na wanahabari walielezea kusikitishwa na tukio hilo, wakidai mtoto Maria juzi asubuhi walishiriki naye Jumuiya ya Mtakatifu Maria Consolata ambayo ilifanyika nyumbani kwao.

Walisema kwa nyakati tofauti mtoto huyo alishiriki na wazazi wake kupanga viti tayari kwa maandalizi ya jumuiya.

Mkazi mmoja wa eneo hilo alidai, kifo cha watoto hao ni pigo kwa wazazi hao ambao ni majirani na marafiki wa muda mrefu.

Imedaiwa kuwa wazazi hao kila mmoja alikuwa na watoto wawili, wa kwanza wote wakiume na wapili wa kike ambao ndio waliofariki katika tukio hilo la kusikitisha.

“ Kifo hiki kimeacha pengo kwani wote wameondokewa na watoto wao wa pili kuzaliwa na wote ni wa kike wamebaki wakiume tu…inauma sana na ni funzo kwetu kuwa tayari wakati wowote,” ilielezwa.

Mwili wa mtoto Maria ulisafirishwa jana kwenda mkoani Rukwa kwa mazishi ambayo yanatarajia kufanyika kesho.

Hata hivyo inadaiwa mama mzazi wa Maria hayupo jijini Dar es Salaam alisafiri kwenda Rukwa kwa ajili ya sherehe za mwisho wa mwaka na bado yupo huko.

Familia ya Francis inatarajia kufanya mazishi ya mtoto wao Esther leo katika Makaburi ya Segerea, Ukonga.

Padre aliyeongoza ibada ya kuuaga mwili wa mtoto Maria aliwataka wazazi na waumini wa kanisa Katoliki la Mtakatifu Therese kutohusisha tukio hilo na imani potofu na kusema kila binadamu anakuja duniani kwa mpango wa mungu na kuondoka kwa mpango wa mungu ingawa vifo vya watoto hao ni vyakusikitisha hasa ukizingatia umri wao mdogo waliokuwa nao na kuwa kazi ya mungu haina makosa.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu, Deus Nchimbi alisema, kifo cha watoto hao ni pigo kwa familia hizo marafiki. 

“Kikubwa ni kuomba amani na kuwaombea marehemu lakini watoto wamekufa kifo cha uchungu kwa kukosa hewa huenda wangekuwa na wakubwa wangeweza kufungua gari,”alisema Nchimbi.

Alisema kilichobaki ni kuikumbusha jamii kuwa makini na vyombo vya moto na kuwapa uhuru watoto waweze kufahamu aina ya mali zilizopo nyumbani.

Changamoto kubwa iliyoibuka katika tukio hilo ni kwa wazazi wote wa pande mbili kugoma kulizungumzia tukio hilo kwa waandishi wa habari kwa madai kuwa  wanaopaswa kulizungumzia ni Jeshi la Magereza wakati suala hilo ni la kifamilia zaidi na linagusa maisha ya kijamii.

"Tumepewa maagizo kutoka juu kuwa waandishi wa habari hampaswi kuchukua taarifa hii kwani ndugu za marehemu bado wanamajonzi hivyo subirini wakisha zika mje kuwahoji wafiwa hayo ndiyo maagizo na jeshini hatuna kauli nyingi ni moja tu" alisema ofisa mmoja wa jeshi hilo ambaye hakujitambulisha jina lake. 

No comments:

Post a Comment