Na Rahim Kambi, Dar es Salaam
NI kilio kwa
wakazi wa jiji la Dar es Salaam. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli kuwatangazia wakazi na
wananchi wa jiji la Dar es Salaam kuwa sherehe za Miaka 55 ya Uhuru zinaweza
kuwa za mwisho kufanyika jijini hapa.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli
akihutubia wananchi waliojitokeza katika sherehe za miaka 55 ya Uhuru wa
Tanzania Bara katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Rais
Magufuli alisema kuwa tamko lake kwa Watanzania linakuja kutokana na kuazimia
sherehe kama hizo miaka ijayo zitafanyika mkoani Dodoma ambapo serikali yake
itakuwa imehamia huko ikitokea jijini Dar es Salaam.
Dr Magufuli
aliyasema hayo katika Maazimisho ya Miaka 55 ya Uhuru zilizofanyika katika
Uwanja wa Uhuru na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, ambapo majeshi ya Tanzania
yalionyesha uwezo mkubwa katika kuonyesha umahiri wao.
“Naweza
kusema kwamba sherehe kama hizi katika jiji la Dar es Salaam zitakuwa za mwisho
kwa sababu mwaka ujao zitafanyika Makao Makuu ya nchi yetu, mjini Dodoma, hivyo
tukio kama hili litakuwa rasmi kwa ajili ya kuwaaga wana Dar es Salaam,”
alisema Rais Magufuli.
Mbali na
kuhama kwa sherehe hizo, Rais Magufuli pia alitumia muda huo kuwapongeza
Watanzania wote kwa kuazimisha miaka 55 ya Uhuru, akisema nchi imeendelea
kupiga hatua kubwa ya kiuchumi, kielimu na kiutamaduni.
Aliwataka
Watanzania wote kumuunga mkono yeye na serikali yake pamoja na watumishi wake
ili kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa nguvu zote ili kurahisisha maendeleo.
Aidha Rais
Magufuli alitumia muda huo kuwaasa watu wanaoendelea kuendekeza vitendo vya
rushwa na ufisadi akisema kuwa ataendelea kula nao sahani moja ili kuhakikisha
kwamba nchi yake inaondokana na adha hiyo inayochelewesha maendeleo.
No comments:
Post a Comment