Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
NAAM! Macho
na masikio ya wengi katika nchi yetu kwa sasa ni namna gani Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kitaingia kwenye mabadiliko makubwa kutokana na aina ya utendaji wa Mwenyekiti
wake, Dr John Pombe Magufuli.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dr John Pombe Magufuli, pichani.
Dr Magufuli ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anajulikana kama kiongozi asiyependa ujinga na mtumbua majipu, aliyerithi mikoba ya Uenyekiti wa CCM Taifa kutoka kwa Mwenyekiti Mstaafu, Dr Jakaya Mrisho Kikwete.
Dr Kikwete
alikuwa mwenyekiti wa CCM Taifa huku akitawaliwa na huruma, tabasamu kiasi cha
watendaji wake kutumia mwanya huo kuwa wala rushwa, wachumia tumbo na ‘majipu’ yanayostahili
kutumbuliwa bila ganzi. Ndio ni majipu.
Tena majipu makubwa kuliko hata yale ya watendaji wa serikali, ukizingatia kuwa
kushamiri kwao wengi wao wamezalishwa na kuchochewa na mfumo mbovu wa
upatikanaji wa viongozi wa CCM kwa miaka ya hivi karibuni.
Dr Magufuli akiwasalimia wajumbe wa CCM.
Hakuna
asiyefahamu majipu hayo. Hata alipokuwa anahutubia wajumbe mjini Dodoma wakati anakabidhiwa
nafasi ya uenyekiti wa CCM Taifa, Dr Magufuli alilizungumzia kwa kina,
akionyeshwa kukerwa na aina watendaji na mfumo wa chama chake. Mwenyekiti
huyo alifahamu kati ya matatizo mengi ya kupata viongozi wasiokuwa wasafi, wala
rushwa, wasiokuwa na uchungu na Taifa lao, baadhi yao wanatokea kwenye chama chake.
Naye ni
muathirika mkubwa baada ya kupata wakati mgumu katika mchakato wa kuomba
wadhamini alipochukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama cheke kuwania Urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia CCM, huku baadhi ya makada wake
wakituhumiwa kumwaga fedha kama njugu ili kuongeza ushawishi kutoka kwa baadhi
ya viongozi na wanachama katika vijiji, kata, wilaya na mikoa mbalimbali ya
nchi yetu.
Licha ya
ukongwe wake, CCM ilianza kupoteza sifa na imani kwa wananchi wengi wa mijini huku
wa vijijini nao wakianza kuangalia uwezekano wa kuongozwa na wapinzani. Wakaiona
CCM ni chama cha mafisadi, wala rushwa na watoa rushwa.
Viongozi
wakaanza kupatikana kwa ukwasi wa fedha. Nafasi zote za uongozi ndani ya CCM na
zile za ubunge na udiwani ziliuzwa kwa fedha nyingi. Walalahoi wachache
walipita. Tena kwa kufanya kazi ya ziada ama kulazimika kuwa kwenye mtandao wa
wenye nazo. Kuweka
mamilioni ya fedha ili kuongeza ushawishi wa kupata madaraka ndani ya CCM
kilikuwa mazoea. Na kila mtu alijua hilo. Mgombea anaulizwa, “Mzee unatuachaje”?
Wakati huu
tunapoelekea kwenye matazamio ya kuundwa upya kwa chama cha CCM, nashawishika
kusema Dr Magufuli ana kazi kubwa ndani ya chama chake. Wengi wanaomzunguuka
hawastahili kuachwa waendelee kuwapo ndani ya nafasi zao, haswa makatibu wa
wilaya, mikoa na watendaji wengine ndani ya chama hiki.
Wengi wao
waligeuka kuwa madalali wa wataka uongozi ndani ya CCM. Kamwe hawaangalii sifa
yoyote isipokuwa fedha, urafiki, undugu na ujirani kama karata ya kupata
viongozi wao. Hata wale
waliokuwa chaguo halisi la wananchi, hawapewi nafasi na walijikuta wakikanyagwa
wakati wote. Hawakuwa na haki yoyote ndani ya chama chao. Viongozi wao wa chama
ngazi ya wilaya na mikoa walicheza kamari mchana kweupe.
Mtindo huo
na mingineyo iliiweka CCM katika wakati mgumu kwenye chaguzi mbalimbali nchini
kwetu. Na utafiti usiokuwa rasmi ulionyesha kati ya wagombea wengi walioangushwa
katika majimbo au kata, ni wale waliopitishwa kwa hila bila kuwa chaguo halisi
la wengi.
Wagombea wa
nafasi za ubunge ama udiwani wakabaki kuwa chaguo la kikundi kidogo cha watu, wanapitishwa
bila kuangalia mtaji wao kwa wapiga kura mitaani. Hili linakatisha tamaa. Matokeo yake
watu wanapiga kura za chuki dhidi ya chama tawala. CCM kinaonekana ni chama cha
wachache. Aliyetaka kugombea nafasi yoyote kwanza angeangaliwa fedha zake. Angeulizwa
juu ya mtaji wake kifedha alionao.
Na kama hana
fedha, jua angeonekana si lolote katika siasa za chama kwa wakati huu. Ni
tofauti na CCM ya wazee wetu, akina Julius Kambarage Nyerere na wenzake. Wao waliijenga
CCM ya Watanzania wote, wengine wameifanya ya wachache wenye nazo. CCM kilikuwa
chama cha walalahoi. Wote walijivunia nacho bila kujali dini zao, ukabila wao
na maeneo watokayo.
Inashangaza
kuona umeundwa mfumo mbovu wa nafasi za uongozi ndani ya chama hiki kikongwe.
Viongozi hawajui wajibu wao. Si Katibu wa wilaya, mwenyekiti wala MNEC anayefahamu
wajibu wa kusimamia sheria, taratibu wala maadili ya uongozi. Kazi yao
ikabakia kuwa wapambe wa wabunge katika maeneo yao. Hakuna jingine walilojua
zaidi ya hilo. Kama walisema juu ya utendaji mbovu wa Mkurugenzi wa
Halmashauri, basi mtendaji huyo atakuwa hayupo kwenye mtandao wa mbunge wake.
Mfumo huu
ulichelewesha maendeleo. Wakageuka Bendera, wapambe ama makatibu wa wabunge majimboni
mwao. Wataalamu kama walimu, afya na wengineo nao wakalazimika kutii matakwa ya
wabunge hao, wakielekezwa kufanya hata yale yasiyokuwa na tija katika nafasi
zao kwa mujibu wa sheria.
Wasiofanya
hivyo wakanyanyasika na wengineo kujikuta wanahamishwa kwingine bila sababu za
msingi. Viongozi wa chama wilaya na mikoa hawajui wajibu wao wala ufahamu wa
kusimamia watendaji wa serikali kama chama tawala.
Wakajikuta wao
ndio wanasimamiwa na wengine. Hakuna hata anayeweza kuinua mdomo wake kumkemea
mbunge, Mwenyekiti wa Halmashauri ama Meya. Watawezaje wakati walinunuliwa katika
mchakato wa kura za maoni? Uwezo wa kusema wautoe wapi? Ndio CCM
ilivyokuwa kabla ya Dr Magufuli kupewa nafasi ya kuwa Mwenyekiti Taifa. Sasa ana
kazi ya kuitoa CCM katika mikono ya wajanja na kuileta panapostahili.
Kuirudisha CCM kutoka kwa walioiendesha kwa mbinu za kimtandao.
Vipi hii ya
Magufuli? Ataiweza? Atawaweza wajanja hawa? Katika kuangalia kama ataweza au
atashindwa ni budi kwa wanachama wote kuhakikisha kwamba mwenyekiti wao
anaweza. Na kwanini
ashindwe? Kazi anayoifanya kurudisha nidhamu serikalini ni ishara kuwa uwezo
huo anao. Aungwe mkono. Kila mwanachama wa CCM atimize wajibu wake, awe mlinzi
kwa mwenzake.
Mwana CCM asikubali
kununuliwa wala asinunue mwenzake. Atakayeonekana anahonga ili achaguliwe katu
hastahili kuachwa badala yake amulikwe na awajibishwe. Kitendo cha
kununua uongozi kinachelewesha maendeleo. Watu hawafanyi kazi kwa moyo badala
yake wanawaza kurudisha fedha walizotumia kwenye chaguzi zao.
Watoa rushwa
waone sasa mwisho wao umefika. Mwisho wa kuondosha makapi na kuleta watu
wanaokubalika kwa sifa zao umewadia. Wana CCM wasioneane haya. Waambiane ukweli
na ikiwezekana watumbuane.
Hii itawezekana
kama watakubali kubadilika. Isiwe CCM ya wajanja tena ila iwe ya walalahoi na
Watanzania kwa ujumla. Mapambano haya yaanzie kwenye uchaguzi wa nafasi za
ndani kuanzia shina, tawi, kata, wilaya na Taifa mwaka 2017.
Asitokee wa
kupitishwa kwa ghiliba. Ili jambo hili lifanikiwe, Dr Magufuli na safu yake ya
juu ya CCM anapaswa kuwahamisha kama sio kuwafukuza kazi baadhi ya watendaji wa
chama ngazi ya wilaya na mikoa ili aisuke upya kwa kuwa wao ndio tatizo kubwa. Hawa wakiachwa
kwenye nafasi zao haswa Makatibu wa Wilaya na Mikoa watamuangusha Mwenyekiti.
Hii ni kwa sababu wengi hawajui wajibu wao. Wanalalamikiwa kila kona ya nchi
yetu.
Ni wachache
waliofanya kazi zao kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa. Ikiwa
Dr Magufuli ataanza kuisuka CCM huku akiwabakiza kwenye nafasi zao niliowataja
hapo juu ni wazi atachelewa kutimiza malengo ya kuisuka upya. Afanye
uchunguzi wa kina. Watendaji mizigo watimuliwe. Wateuliwe wengine watakaokubali
kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa na kutoa haki kwa watu wote.
Lazima
lifanywe jambo nyeti na lenye tija kwa mustakabali wan chi yetu kama njia ya
kukifanya kiendelee kuheshimika kwa miaka 50 ijayo.
Sisemi kama
wenyeviti waliopita ukiwamo uongozi wa Dr Jakaya Mrisho Kikwete haukufaa. Kikwete
alifanya mengi ya msingi, hata hivyo mkazo na mabadiliko zaidi yanahitajika.
Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015 ulikuwa mgumu. Isingekuwa juhudi za ziada, huenda mambo yangekuwa
mabaya kwa chama hiki. Pia tulishuhudia jinsi Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Abdulrahaman
Kinana na timu yake walivyohangaika kufanya mikutano katika Kata, Wilaya na Mikoa
mbalimbali kwa ajili ya kujua kero na kusimamia watendaji wa juu wa serikali,
hususan mawaziri.
Ziara za
Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi ambaye ni Waziri wa Habari, Michezo,
Sanaa na Utamaduni wa serikali ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Nape Nnauye zilizaa
matunda. Huu si
wakati wa kuchekea ujinga unaokihujumu chama. Utakiangamiza. Kila mtu atimize wajibu
wake. Viongozi na watendaji wa chama waifanye kazi yao wakati wote na si kusubiri
Uchaguzi Mkuu kama njia za kusaka pesa kutoka kwa wagombea.
Watendaji,
Makatibu na Wenyeviti wacheza kamari wakati wa kura za maoni hawahitajiki tena.
Waondoshwe. Kwa mfano, wapo Makatibu wa CCM na wana mtandao wenzao wanaomba
rushwa kutoka kwa wagombea ili watoe ushindi ama nafasi nzuri ya kura. Nazungumzia
nafasi ya kwanza hadi ya tano, ambayo kiuhalisia makada watatu wanaofikishwa
Kamati Kuu mmoja wapo anaweza kuteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM.
Hayo na
mengine mengi yaliwafanya makada wafanye kila wawezalo kuhonga wasimamizi wa
uchaguzi wa chama katika majimbo, kila mtu akitaka nafasi za juu. Ni jambo la
kusikitisha. Na hapo
ndipo linapotokea swali la akiba ya fedha kutoka kwa mgombea husika. Mtoto wa
mkulima, mlalahoi hata akubalike vipi jimboni kwao ni ngumu kupenya.
Hivyo
kuibuka kwa Dr Magufuli na kuapa kuisuka upya CCM, aghalabu matumaini mapya
yametokea. Matumaini ambayo wapo wasiyotaka, wakiamini ule ufalme wao
unatoweka. Hata hivyo
ifikie wakati tuseme imetosha. Chama kisukwe upya na wale wasiostahili
washughulikiwe haraka kama walivyoshughulikiwa watendaji wa serikali.
Endapo
kwenye CCM hakutakuwa na majipu, hata dhamira ya kuwa na watendaji wenye kujali
maslahi ya Watanzania kwenye serikali itafanikiwa kwa vitendo. Hakutakuwa
na njia za panya tena. Viongozi wababaishaji, wala rushwa, mafisadi na wasaka
tonge watatoweka na kuifanya nchi iwe kwenye mstari mzuri wa kimaendeleo.
Si tu
uongozi ndani ya CCM ulinunuliwa na wataka madaraka na kuuzwa na makatibu wa
wilaya na mikoa, bali pia watu hao walishindwa kusimamia rasilimali za chama
katika maeneo mengi hapa nchini. Kila kona ni ujanja ujanja tu. Mikataba
isiyokuwa rafiki na isiyokuwa na tija kwa chama iliingiwa kila siku.
Wakaifanya
CCM ya maslahi yao. Wakazichapa kadi feki za CCM ili mabwana wakubwa wao
washinde. Kama hiyo haitoshi, wakapeleka mihutasari na ripoti feki ili
kuaminisha ushindi huo. Mwisho wa
uchafu huo ni kukataa kwa Watanzania juu ya wanaopitishwa katika kata na
majimbo husika. Na ndio maana idadi ya viti vya udiwani na ubunge kwa upande wa
upinzani inaongezeka maradufu nchini.
Nani wa
kusema? Ni dhahiri wamedhamilia kukiangamiza chama hiki kikongwe hapa nchini.
Hivyo anapotokea Dr Magufuli na kuamua kwa dhati kurudisha misingi na dira ya
chama hiki, kwanini asiungwe mkono?
Ndio maana
nasema nina hamu ya kuiona CCM ya Dr Magufuli. Mtu pekee atakayerudisha heshima
ya CCM mitaani. Mabadiliko makubwa atakayofanya yataleta imani kwa Watanzania
wote, mijini na vijijini.
Kwa bahati
nzuri hakuna wakati mzuri wa kuisuka upya CCM kama mwaka ujao wa 2017, ambao
chama kitafanya chaguzi zake katika ngazi zote, jumuiya zote. Hata hivyo
narudia tena, mabadiliko hayo na dhamira ya kusukwa upya kwa chama hiki yaanzie
katika kuwabadilisha ama kuwafukuza kazi watendaji wabovu, waliofanya kazi kwa
matakwa yao binafsi haswa makatibu wa wilaya, makatibu wa mikoa na makatibu wa
jumuiya za chama ili kuhakikisha kwamba CCM inazaliwa upya na inakuwa katika
misingi ya kuongoza nchi kama chama tawala. Chama kikongwe chenye historia
murua kwa Taifa letu.
Naamini Dr
Magufuli na safu yake uwezo huo wanao. Kilichobaki ni kuombewa na kupewa
ushirikiano kwa wanachama wote bila kuangalia vyeo vyao, majina yao, fedha zao
na mengineyo.
+255
712053949
No comments:
Post a Comment