Pages

Pages

Thursday, November 17, 2016

Mchakato wa ndege za Saudi Arabia na Tanzania waanza kusukwa

*Ni matokeo ya kikao kati ya balozi Mgaza na Mkurugenzi Mkuu Saudi Arabian Airline
*Vivutio vingi vya utalii nchini Tanzania vyatajwa kwenye kikao hicho cha aina yake
Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Balozi Hemedi Mgaza kulia, akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Saudi Arabian Airlines, Mh Saleh Bin Nasser Al Jasser, katika kikao chao maalum cha kujadili namna ya ndege za shirika hilo kuanza safari za kutoka Saudi Arabia hadi nchini Tanzania. Picha zote kwa Hisani ya Ofisi ya Balozi wa Tanzania Saudi Arabia.


Na Mwandishi Wetu, Saudi Arabia
WATALII, wafanyabiashara, mahujaji wa Watanzania pamoja na watu kutoka nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia, huenda wakapata fursa ya kuwasili Tanzania kwa urahisi endapo mchakato Shirika la Ndege la Saudi Arabian Airlines wa kutoa ndege za kutoka Saudi Arabia hadi nchini Tanzania utakapofanikiwa kama ulivyoanza kushughulikiwa.
Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Balozi Hemedi Mgaza kulia akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Saudi Arabian Airlines, Mh Saleh Bin Nasser Al Jasser kushoto. 
Mapema wiki hii Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Balozi Hemedi Mgaza alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Saudi Arabian Airlines, Mh Saleh Bin Nasser Al Jasser, ambapo shughuli mbalimbali za utalii na vivutio vya Tanzania vilijadiliwa, kama njia ya kuangalia namna bora ya ndege hizo kufanya safari zake vizuri kwa kuzingatia mkataba wa ushirikiano wa mambo ya anga baina ya Tanzania na Saudi Arabia Bilateral Air Service Agreement (BASA).

Kikao kinaendelea kati ya balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Balozi Hemedi Mgaza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Saudi Arabian Airlines, Mh Saleh Bin Nasser Al Jasser kushoto. 
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Mgaza alisema kuwa Tanzania ni nchi yenye vivutio vingi vya Utalii kama mbuga nzuri za wanyama pamoja na Mlima wa Kilimanjaro ambao ni alama bora za utalii nchini humo inayochochea wageni wengi kuingia na kutoka katika nchi hiyo yenye amani na upendo.


Alisema endapo kutakuwa na ndege za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi nchini Tanzania, Shirika linaweza kutoa huduma bora bora kwa kupitia sekta ya utalii pamoja na ile ya mahujaji.

“Unapozungumzia sekta ya utalii, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna vivutio vingi vinavyosisimua, hivyo naamini kuna kila sababu ya Shirika hili la Ndege kuangalia jinsi ya kuanzisha safari za moja kwa moja.

“Nchi yetu imepiga hatua katika sekta mbalimbali na viwanja bora vya ndege vipo katika hali nzuri, huku tukiamini kuwa endapo wazo hili litafanikiwa nchi yetu Tanzania itapiga hatua kubwa kwa sababu watu wengi watahamasika kufika kutalii bila kusahau watakaotaka kuwekeza kwenye mbio za serikali za kuifanya nchi yetu kuwa nchi ya viwanda,” Alisema Balozi Mgaza.

Kwa sasa mashirika makubwa yanafanya safari zake kama vile Emirates, Oman Air, Etihad Airways, Fly Dubai, Qatar Airways, Egypt Air na Turkish Airlines jambo linalochochea kiu kubwa kwa abiria wa Saudi Arabia na Tanzania wanaopenda kuingia na kutoka kwenye nchi hizi mbili.

No comments:

Post a Comment