Pages

Pages

Tuesday, October 11, 2016

LHRC waadhimisha siku ya mtoto wa kike duniani

Ndugu wanahabari,

Leo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaungana na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, siku ambayo ilipitishwa na  Umoja wa mataifa mnamo  Oktoba 11, 2011.  Kauli mbiu ya kitaifa kwa mwaka huu ni ‘‘Mimba na ndoa za Utotoni zinaepukika, Chukua hatua kumlinda mtoto wa kike’’. 


Hivyo basi katika kuadhimisha siku hii Kituo kimeangazia mtoto wa kike hapa Tanzania na changamoto anazokumbana nazo. Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto wa kike kati ya umri wa miaka 0-17 hapa Tanzania ni  11,263,891 idadi ambayo ni sawa na asilimia 48.8 ya watoto wote chini ya miaka 17, ambapo Tanzania bara  kuna watoto wa kike  elfu 10,943,846 na Tanzania visiwani idadi  yake ni laki 320,045. 


Hivyo basi nusu ya idadi hii ni wanawake na watoto  ikilinganishwa na idadi ya watanzania wote ambao ni milioni 44,928,923 ambapo  kati yao wanawake ni milioni 23,058,933. 

Inasikitisha kuona kuwa mtoto wa kike hapa nchini bado amekuwa akikabiliwa na changamoto nyingi na cha kusikitisha zaidi mtoto huyu anaanza kubaguliwa kuanzia katika ngazi ya familia. 

Katika familia nyingi za kitanzania mtoto wa kike amekuwa akikosa fursa ya kupata Elimu ukilinganisha na mtoto wa kiume na katika mazingira mengine wazazi wamediriki hata kuwaozesha watoto wao wa kike kwa ajili ya kupata fedha ya kusomesha watoto wa kiume. Ukiangalia pia katika suala zima la Elimu ni ukweli usiofichika kuwa idadi ya wasichana wanaoshindwa kumaliza masomo kwa sababu za kupata mimba imekuwa ikiongezeka.



 Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la watoto duniani UNICEF kumekuwa na ongezeko la mimba mashuleni kutoka asilimia 23 hadi 26 yaani takribani watoto wa kike 8000 hapa Tanzania kila mwaka hukatisha masomo kwa ajili ya ujauzito. Vile vile idadi ya watoto wa kike ambao wamekuwa wakimaliza Elimu ya msingi lakini kutokupewa nafasi ya kujiendeleza kielimu hata pale wanapokuwa wamefaulu nayo pia imekuwa ikiongezeka na badala yake mabinti hawa wamekuwa wakilazimika kuingia katika ndoa katika umri mdogo.



Ndugu wanahabari,

Hali hii ya Watoto wakike kutokupata fursa ya elimu husababisha ongezeko kubwa la watoto wa kike wanaosafirishwa kutoka vijijini na kuletwa mijini kwa minajili ya kuja kuendelezwa kielimu na matokeo yake mabinti hawa wamejikuta katika wakati mgumu kwa kufanyishwa kazi za ndani bila malipo stahiki na wakifanyiwa vitendo vingi vya kikatili na vya kuwadhililisha. 

Hali hii imepelekea mabinti wengine kutoroka kutoka kwa waajiri wao na kuanza kuishi mtaani na hivyo kurubuniwa na kujiingiza katika biashara za ngono na wengine hata madawa ya kulevya.


Tumeendelea pia kushuhudia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kingono kama ubakaji na ulawiti kwa Watoto wa kike na cha kusikitisha zaidi vitendo hivi vimekuwa vikifanywa na Ndugu wa karibu sana wa Watoto hawa wakiwemo wazazi, walezi, majirani na hata walimu huko mashuleni. matukio haya yamekuwa hayafikishwi Katika vyombo vya Sheria kwani mengi huzungumzwa kifamilia na kuwaacha watuhumiwa wakiendelea na maisha yao.


Ndugu wanahabari,

Tanzania pia ni nchi moja wapo yenye idadi kubwa ya ndoa za utotoni kwa takribani  ya asilimia 35 watoto wa kike hapa nchini huozeshwa nchini ya umri wa miaka 18 na hivyo kukatishwa ndoto zao za kujiendeleza kielemu na hata ustawi mzima wa maisha yao.

Inasikitisha zaidi kuona pia pamoja na juhudi mbalimbali za utetezi na ushawishi wa wanaharakati katika kupinga vitendo hivi viovu na mila kandamizi bado Ukeketaji umekuwa ni tatizo kubwa sana hapa nchini. Kwa mujibu wa takwimu za Viashiria vya Idadi ya watu na afya 2010, asilimia 14.6% ya wanawake Tanzania wamekeketwa na wengi wao ni watoto wa kike. 


Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa mbinu mpya zimekuwa zikibuniwa ikiwemo  kukeketa watoto mara wanapozaliwa. 


Vilevile, kwa mujibu wa taarifa ya haki za Binadamu ya mwaka 2015 inayotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kila mwaka ongezeko la matukio ya Ukatili kwa watoto ikiwemo watoto wa kike kupewa adhabu kali ambazo hazilingani na makosa waliyoyafanya, mfano unakuta mtoto anachomwa mikono moto kwa kosa la kuunguza mboga.


Kwa kifupi watoto wa kike wanapata athari mbalimbali ikiwemo;

1.      Kuendelea kudidimiza nafasi ya mwanamke katika Jamii na taifa zima kwa ujumla na kuendeleza mfumo dume kwani ukatili mwingi huanzia katika ngazi ya familia

2.      Kutokuendelezwa kielimu kwa mtoto wa kike na hii hupelekea kuendelea kuwa na idadi kubwa ya Wanawake ambao hawana Elimu na hivyo kuendelea kuwa tegemezi kwa wanaume na pia kushindwa kujikwamua kiuchumi.


3.      Idadi kubwa ya athari za kiafya zinazowapata watoto wa kike kwa ajili ya kujifungua katika umri mdogo ambayo husababisha wengine kupoteza maisha, kupatwa na fistula na maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na magonjwa mengine ya zinaa.


4.      Malezi duni ya watoto kwa kuwa watoto hawa wanakuwa bado ni wadogo kuweza kukabiliana na jukumu kubwa la malezi na matunzo ya familia.


5.      Kuendelea kuongezeka kwa Ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwani watoto hawa mara nyingi huolewa na watu waliowazidi umri sana na hivyo kutokuwa na maamuzi yoyote katika nyumba.


Hivyo basi tunapendekeza yafuatayo:


1.      Katika ngazi ya familia wazazi na walezi kuthamini na kuwajali watoto bila ubaguzi wa jinsi zao. Watoto wote wapewe fursa sawa kielimu na kujiendeleza kimaisha. Wazazi kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili hasa Ukatili unaoanzia majumbani,sambamba na hilo kutoa taarifa za matukio ya Ukatili wanayofanyiwa watoto na sio kutatua matatizo haya katika ngazi ya familia ilihali haki ya mtoto inapotezwa.


2.      Wito kwa Jamii kuwajibika katika kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili. Kuthamini nafasi ya kila mtoto na kuona mtoto wa mwenzako ni wa kwako; pia kutoa taarifa ya matukio ya Ukatili katika maeneo wanayoishi na sio kufumbia macho na kuwaficha waovu.


3.      Serikali kuhakikisha kuwa sheria zilizopo zinasimamiwa na zinatekelezwa pale zinapovunjwa kwa kuweka mifumo iliyowazi na rahisi ya kupata na kufuatilia haki. Vile vile kubadilisha sheria ambazo bado zimekuwa ni kandamizi kwa mtoto wa kike ikiwemo Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoafiki mtoto wa kike kuolewa katika umri wa miaka 15. Serikali itekeleze agizo lilitolewa na Mahakama Kuu Julai 8 2016 la kubadili kifungu na 13 cha sheria ya ndoa 1971 juu ya ndoa za utotoni


4.      Serikali kwa kupitia taasisi zake kama polisi na mahakama kuhakikisha kuwa Mashauri yanapolekwa Mahakamani yanasikilizwa bila vikwazo na kutolewa maamuzi kwa wakati stahiki maana ‘justice delayed is justice denied’ - ‘kuchelewesha haki ni kunyima haki’.


5.      Wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa ya matukio ya Ukatili wanayofanyiwa watoto ili wale wanaofanya vitendo hivi waaibishwe na waadhibiwe kwa mujibu wa sheria; tunavitaka vyombo vya Habari visiishie tu kuripoti matukio haya pindi yanapofanyika bali hata kuendelea kufuatilia mashauri yaliyopo mahakamani ili kusaidia mashauri haya yafanyiwe kazi kwa wakati.


6.      Pamoja na hilo tunaviomba vyombo vya habari kuwa makini jinsi wanavyoripotia matukio haya ya Ukatili kwa watoto kwani utoaji wa taarifa hizi wakati mwingine umekuwa pia ukiendelea kuwavunjia haki watoto hawa kwa kutozingatia sheria inayotaka utoaji wa taarifa za watoto kutunza majina halisi ya watoto na hata sura zao.


7.      Na mwisho kabisa tunaomba viongozi wetu katika ngazi zote za kijamii na hata kitaifa kuibeba ajenda ya haki za watoto na hususani haki za watoto wa kike kama ajenda ya kitaifa ili kuhakikisha wanalindwa dhidi ya vitendo viovu na wana mazingira salama ya kukua na kuwa watu wema na mustakabali mzuri wa maisha yao ya sasa na ya baadae.


Tunawashukuru sana.


Wasalaam, Kituo cha Sheria na Haki za Binada


Dr. Helen Kijo-Bisimba Mkurugenzi Mtendaji


No comments:

Post a Comment