Pages

Pages

Wednesday, August 10, 2016

Kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart yanyakua tuzo Kimataifa

Mwenyekiti wa  Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, Yono Kevela, akionesha tuzo za kimataifa ya ufanisi bora wa kazi baada ya kukabidhiwa.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KAMPUNI ya Udalali ya Yono Auction Mart, imekabidhiwa tuzo ya Mshindi wa Kimataifa ya Ufanisi na Ubora wa Kazi, baada ya kushindanishwa na kampuni nyingine 49 za nchi tofauti duniani hatua iliyotokana na utendaji wake katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza Jijini Dar es salaam jana, Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Yono Kevela, alisema ushindi huo unatokana na ufanisi wao wa kazi zikiwepo za ukusanyaji madeni ya kodi kutoka kwa wadaiwa sugu wa serikali .

Kevela alisema baadhi ya kazi walizofanya baada ya kupata zabuni ya kukusanya madeni ya wadaiwa ni za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wizara mbalimbali, taasisi za fedha na wakala wa serikali pamoja na wadau wengine.

Alisema ushindi wa tuzo hiyo ni faida ya ufanisi wa kazi zao katika kukusanya kodi za serikali huku akiahidi kutobweteka katika jukumu hilo alilopewa na Serikali hadi kushinda tuzo hiyo na badala yake atazidi kuongeza juhudi ili kampuni hiyo izidi kufanya vizuri.

“Tunashukuru kazi na huduma zetu kutambuliwa kimataifa, tumekuwa mabalozi wazuri wa Tanzania, tumetumia fursa hiyo kuitangaza nchi na kuwahimiza wawekezaji kuja kuwekeza “, alisema. Kevela

Alisema Tuzo hiyo ilitolewa Ufaransa na sherehe za kukabidhi washindi tuzo hizo zilifanywa Juni 25, mwaka huu Rome Italia ambako kampuni hiyo imeshinda ikitoka sekta binafsi, huku upande wa serikali ukishinda sekta ya Utalii kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Kampuni hiyo ya Yono imejizolea umaharufu hivi karibuni bada ya kupewa kazi ya kukusanya madeni ya wadaiwa 24 wa TRA, yenye thamani ya Sh bilioni 18.95 baada ya wadeni hao kutorosha kontena za mizigo yao kwenye Bandari Kavu (ICD) ya Azam mwishoni mwa mwaka jana.

Hata hivyo baada ya kampuni hiyo kuanza kazi, baadhi ya wadaiwa walifanikiwa kulipa madeni yao huku wengine wakilipa kiasi na wengine mali zao walikubali zikamatwe na kuuzwa ili kulipa madeni hayo, ambapo hadi sasa zaidi ya Sh bilioni saba zimeshakusanywa.

Maeneo mengine ambayo kampuni hiyo inafanya kazi ya kukusanya madeni dhidi ya wadaiwa mbalimbali ni pamoja na maeneo ya ardhi, mahakama, mabenki na taasisi zingine.

No comments:

Post a Comment