Pages

Pages

Thursday, March 31, 2016

Mbunge Mkuranga asaka uwezeshwaji wa wananchi wake



Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji la Taifa, Bengi Issa mwenye kilemba, akizungumza kwenye kikao cha pamoja na Mbunge wa Mkuranga, Mheshimiwa Abdallah Ulega kushoto kwake kwa ajili ya kuangalia namna ya kushirikiana naye kuwasaidia na kuwawezesha wananchi wa Mkuranga.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MBUNGE wa Jimbo la Mkuranga, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, Abdallah Ulega, jana amefanya kikao na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Taifa (NEEC), Bengi Issa, kwa ajili ya kutafuta fursa ya kuwawezesha wananchi wilayani humo.
Mbunge wa Mkuranga, Mheshimiwa Abdallah Ulega, akizungumza jambo katika kikao cha pamoja na Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji la Taifa (NEEC), Bengi Issa, hayupo pichani.
Kikao hicho pia kilihusisha Mkurugenzi wa Uwezeshaji, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuranga, ambapo pamoja na mambo mengine, kilijadili namna ya kusaidia vikundi vilivyosajiliwa 285, vikundi vya vicoba 109, ufugaji wa nyuki, vikundi vya wanawake, vijana na waendesha bodaboda.
Akizungumza baada ya kikao hicho kumalizika, Ulega aliyewahi pia kuwa Mkuu wa wilaya Kilwa, alisema kwamba lengo ni kuona wanananchi wa Mkuranga wanapiga hatua kutoka kwenye hali ya ukata na kufikia kiwango kizuri, sanjari na kufanikisha maendeleo kwa wananchi wote.
Alisema kwamba kikao hicho kimemalizika kwa mafanikio ambapo ilishauriwa kuwa vikundi vya kukopeshana (VICOBA) inabidi viwekwe chini ya mwamvuli mmoja utakaoviwakilisha vyote.
“Hili litakapofanyika, Benki ya Posta Tanzania ina utaratibu wa kutoa mikopo ya riba ndogo kupitia mwamvuli huo unaowakilisha vikundi vyote kwa pamoja, tukiamini kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha ndoto zetu.
“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaiweka Mkuranga katika kiwango kizuri ukizingatia kwamba wilaya hii ipo karibu na jiji la Dar es Salaam, hivyo inaweza kukua kwa kasi kwa sababu mtu anaweza kuishi Mkuranga na akafanya kazi au kuingia na kutoka kwa urahisi wilayani kwetu,” alisema.
Aidha imeshauriwa pia kuanzisha SACCOS ya wafugaji wa nyuki ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo ya vifaa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa wa nyuki, ambapo wana vikundi wanatakiwa kuandaa mpango kazi wao utakaopelekwa Benki ya Maendeleo kwa ajili ya mkopo, ikiwa na lengo la kuhifadhi misitu na kuacha utafutaji wa kipato kwa njia ya kukata miti ili kuzalisha mkaa.

No comments:

Post a Comment