Pages

Pages

Monday, February 15, 2016

Mwanachama wa Coastal Union Hafidh Kido asema mwenyekiti wao ni jipu

Niliamua kukaa kimya kuhusu kinachoendelea katika Klabu ya Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ hasa katika kipindi hiki tunachopambana tusishuke daraja. Uzalendo umenishinda.
Niliwahi kuwa msemaji wa timu, lakini mbali ya utumishi huo ndani ya nafsi yangu ninaipenda Coastal Union. Natamani siku zote iwe inanipa raha hata nikikaa na wenzangu nijisifie kuzaliwa Tanga.

Mdau wa soka na mwanachama wa klabu ya Coastal Union, Hafidh Kido, pichani.
Kuna kitu wengi hawakijui, Coastal Union iliyoanzishwa mwaka (1948) ni miongoni mwa timu zilizofanya vizuri katika miaka ya mwanzo ya kuanzishwa ligi kuu wakati huo ikiitwa ligi daraja la kwanza.  Hata Simba na Yanga hazikufua dafu, katika miaka ya mwanzoni baada ya uhuru timu zilizokuwa zikishika nafasi za juu katika msimamo wa ligi ni Simba, Yanga, African Sports na Coastal Union. Lakini kwa sasa mambo yamebadilika, timu za Tanga zinaonekana kituko.

Tulishawahi kukaa chini tukajadiliana tatizo ni nini, majibu tuliyopata ni uongozi; hiyo ni baada ya kupima vitu vinne, Kocha, Mashabiki, Wachezaji na Uongozi. Tulipoangalia morali ya mashabiki tukabaini ipo juu, maana yake kila mechi hamasa inatolewa. Tukaangalia nafasi ya wachezaji labda hawana uwezo, tukabaini wachezaji kuna baadhi ya mechi wakiamua kukaza wanapata ushindi, maana yake uwezo wanao.


Tukaangalia upande wa makocha, wengi baada ya kutimuliwa walifanya vizuri katika timu walizokwenda, tukianzia na Yusuf Chippo, Juma Mgunda, Hemed Morocco, Ally Jangalu, Mayanja na wengine wengi ambao walipita Tanga wakaonekana wabovu lakini baadaye walifanya vizuri kwengine.



Lakini tatizo kubwa likabaki kwa uongozi, tulianza kumfanyia vurugu aliyekuwa Mwenyekiti Hemed Hilal ‘Aurora’ akajiondoa mwenyewe. Tukamkaimisha Makamu Mwenyekiti Steven Mnguto. Huku Katibu na Meneja, Kassim Siagi na Akida Machai hawakutaka kuondoka.
Ukafanyika uchaguzi, siku ya kupiga kura zikafanyika vurugu zisizo na maana. Nilitoa neno kwa baadhi ya jamaa zangu waliomchagua Dk. Ahmed Twaha, nikawaambia mimi simuafiki kwa sababu ni dhaifu.


Udhaifu wake umeonekana sasa kwa sababu wanaoharibu timu ni Meneja Akida Machai na Katibu wake Kassim Siagi, ambao kikatiba ni watu wanaoteliwa. Wanaweza kufukuzwa kwa barua moja tu itakayotiwa saini na Mwenyekiti, lakini hataki kufanya hivyo. Mimi natamka wazi Mwenyekiti ni jipu, anatakiwa kutumbuliwa. Ingawa tumepata ushindi jana dhidi ya Azam FC, lakini kuna mambo ya hovyo ndani ya klabu yanaendelea na hakuna wa kumsimamia mwenzie. Tunazo taarifa Wajumbe wa Kamati Tendaji wanalalamika kwenye vikao kila siku lakini hakuna kinachofanyiwa kazi.


Wachezaji hawana motisha, posho wanapata kupitia mashabiki, mishahara haitolewi kwa wakati, basi la timu kubwa kama hii bado lipo gereji mwaka mzima sasa. Dereva wa timu hajulikani ana shughuli gani.  Viongozi wameshindwa kushawishi wadhamini kutoa fedha, wanategemea fedha za kampuni ya unga wa ngano ‘Pembe’ ambazo zinatolewa kishkaji, hazina mtiririko mzuri.  Hatuwezi kufika kwa mtindo huu, tupo nafasi ya 12na point 16. Haiwezekani tumecheza mechi 19 tumeshidna tatu tu na kutoa suluhu saba tumefungwa mechi tisa tena nyingine uwanja wa nyumbani, aibu hii.
@Aliyevia
Ambaye ameumizwa anipigie 0713 593894.

Makala haya yameandikwa na Hafidh Kido, mwanachama wa klabu ya Coastal Union

No comments:

Post a Comment