Pages

Pages

Sunday, January 10, 2016

Mbwana Samatta, alistahili, anastahili na atastahili pia, HONGERA

Nyakati fulani nilipokuwa Msemaji Mkuu wa klabu ya African Lyon, tuliweka kituo chetu Morogoro Mjini wakati tunaelekea Turiani, mkoani Morogoro kucheza na timu ya Mtibwa Sugar. Tuliingia Mjini Morogoro jioni na kufikia tulipopangiwa. Baada ya kushukuru kwa kufika salama Morogoro, 
Mbwana Samatta, pichani
Kocha Mkuu Charles Boniface Mkwassa, akatoa neno kwa msafara mzima na wachezaji wake, akiwamo nyota wetu Mbwana Samatta. Namsema ni nyota kwa sababu tangu wakati huo tulikuwa tunategemea uwezo wake, akishirikiana na nyota wengine kwa ajili ya kupata ushindi. Mkwassa akasema, " Jamani sisi wote ni watu wazima, hivyo sioni sababu ya kuanza kuchungana chungana. Lazima wachezaji mjue nidhamu, kujituma ndio njia ya kufika mbali katika sekta ya mpira wa miguu. 

Hivyo natumaini kila mtu anajua kilichotuleta Morogoro kwa ajili ya kwenda kucheza na Mtibwa Sugar. Hakuna wa kuwachunga," Mwisho wa kunukuu. Kisha watu wakachanguka. Lakini dakika 20 zilipotimu, nikamuona Samatta anaingia kwenye room yake, mimi nilikuwa nimekaa mapokezi, nasubiri wachezaji wangu warudi ndani, huku nikiangalia tv na kubadilishana mawazo tuliokuwa hapo. 

Nikamshangaa Samatta, nikamuuliza. Vipi, mbona mapema? Akajibu, kwamba hana cha kufanya mtaani. Ameona arudi ndani haraka apumzike kwa ajili ya mechi yake na Mtibwa. Pia akasema kuna mechi anataka kuangalia kidogo kabla ya kulala. Wakati wote huo nilikuwa namheshimu sana Samatta. 

Na kitendo hicho kikazidi kunipa imani kuwa akiendelea na nidhamu ile, hakika atakuwa super star kuliko masuper star wengine wa soka ndani na nje ya nchi. Baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani, nikasubiri wote wapongeze, ndio namimi nifuate sanjari na kuelezea kidogo jinsi ninavyomfahamu Samatta na kuheshimu sana uwezo wake uwanjani. 

Hongera sana Samatta. Mafanikio hayo hayajakuja kama ndoto. Juhudi, bidii, nidhamu na kujituma uwanjani wakati wote ni sababu tosha. Watanzania wote tuna imani kubwa na wewe. Naamini utaibua hamu kubwa ili ufike mbali zaidi, utaibua ari pia kwa wachezaji wengine wa Tanzania ili muwe wengi na sisi tujivunie, tutembee kifua mbele. Mbona vipaji mnavyo. Aisee, asante sana Samatta.
Mwandishi wa makala haya aliwahi kuwa Msemaji wa African Lyon

No comments:

Post a Comment