Pages

Pages

Friday, December 04, 2015

TRA yawabana wafanyabiashara wakwepa kodi, wafanyakazi 35 watimuliwa

Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Philip Mpango (Kulia)akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa ya upatikanaji wa makontena 43 pamoja na malipo ya kodi ya Zaidi ya shilingi bilioni tano kutoka kwa wakwepa kodi,kushoto kwake ni kaimu Kamishna Mkuu wa TRA Bw.Lusekelo Mwaseba.
LU2
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Bw.Lusekelo Mwaseba(Kushoto) akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,kulia kwake ni Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Philip Mpango.


LU3
Mkurugenzi wa Huduma na elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Bw. Richard Kayombo akieleza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, kushoto kwake ni Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Philip Mpango

Na Lorietha Laurence
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kodi ya zaidi ya shilingi bilioni tano kutoka kwa wafanyabiashara waliokuwa wamekwepa kulipa kodi. Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA Dkt. Philip Mpango amesema hatua hiyo imekuja kufuatia agizo kutoka kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Kassim alipofanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam Novemba 27 mwaka huu . Katika Maagizo hayo ya Mhe.Kassim aliitaka TRA kubaini wamiliki wa makontena 329 yaliyoondolewa kwenye bandari kavu kinyume na taratibu pamoja na kutaja bidhaa zilikuwemo ndani ya kontena hizo ikiwemo wakwepaji wa kodi na kuwachukulia hatua watumishi wa TRA walihusika katika mchakao huo.

Aidha Dkt. Mpango aliongeza kwa kusema mpaka sasa wamefanikiwa kubaini jumla ya kampuni 43 zilizohusika katika uigizaji wa makontena ambayo yaliondolewa katika bandari kavu kinyume na taratibu. “Katika kontena tulizozikamata hizo tumekuta bidhaa za matairi ya magari,samani mbalimbali,betri za magari,vifaa vya ujenzi,nguo na bidhaa mchanganyiko” alisema Kamishna Mpango.

Kwa upande wa watumishi wa TRA mpaka sasa watumishi 35 wa ngazi mbalimbali wamesimamishwa kazi wakiwemo 27 waliokamatwa wiki hii katika geti namba 5 ambao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano na uchunguzi zaidi. Pia aliendelea kufafanua kuwa Uongozi wa TRA unawataka watumishi wote kuorodhesha mali zao ili kuhakiki uhalali wa mali hizo na endapo watabainika kuwa wamezipata mali hizo kinyume na sheria hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao.

Naye Naibu Kamishna Mkuu Lusekelo Mwaseba ameeleza kuwa kwa sasa TRA inapitia kwa upya taratibu za utoaji wa leseni ili kuondoa mianya pamoja na kuweka udhibiti katika uondoshaji wa mizigo katika bandari zote,ICDs na bohari za forodha. “Sambamba na kufuatilia taratibu hizo,TRA pia itahakikisha inawafuatalia mawakala wote wa forodha walioshiliki katika upotevu wa makontena na kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafungia leseni na adhabu nyingine kulingana na sheria zilizowekwa” alisema Mwaseba.

Kaimu Kamishna Mkuu Mpango alitoa wito kwa wote wanaohusika na uondoshwaji wa makontena kutoka bandari kavu kinyume na taratibu kujitokeza na kulipa kiasi cha kodi yote wanayodaiwa kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli aliaagiza kwamba wadaiwa wote walipe madeni yao ndani ya siku saba baada ya hapo watachukuliwa hatua kufuatana na mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment