Pages

Pages

Thursday, November 26, 2015

MGODI UNAOTEMBEA: Ardhi ni mali, Magufuli aungwe mkono kwa vitendo

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI Dr John Pombe Magufuli tu, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kila kona anatajwa yeye. Kwenye usafiri wa umma, daladala na mabasi anatajwa yeye. Kwenye maeneo ya huduma za kijamii kama vile hospitali, shuleni na kila kona anazungumziwa yeye. Hii inaonyesha ni dalili njema za kukubalika kwa mwanasiasa huyo ambaye hivi karibuni alitangazwa kuwa rais wa Tanzania. Kutajwa kwa Magufuli kumetokana na kuanza vema katika ngwe yake ya uongozi, akifanyia kazi kwa vitendo yale aliyozungumzia kwenye kampeni zake, akiwa mgombea urais wa Tanzania, kwa kofia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli, pichani.
Siku chache tangu alipoingia madarakani, Magufuli amepiga marufuku safari za nje ya nchi kwa viongozi wa serikali ili serikali yake kuokoa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa yanatumika katika kugharamia safari. Mbali na hilo la safari, pia amezuia sherehe za Siku ya Uhuru, 9 Desemba, akiamini kuwa ni njia ya kuokoa pesa. Awali Magufuli alitangulia pia kuzuia pesa za wabunge zilizotengwa kwa ajili ya sherehe yao. Jambo hili na mengine linatia moyo mno. Angalau sasa watu wanaweza kupata picha ya namna gani Dr Magufuli ataiongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa. Ni kutokana na hilo, naamini Dr Magufuli anastahili pongezi naa kuungwa mkono pia kwa aliyozungumza na hata yale asiyozungumzia pia. Kwa mfano, asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini.

Na watu wa vijijini wanaishi kwa kutegemea kilimo. Kama hivyo ndivyo, kazi ya kilimo haiwezi kukamilika kama hakuna ardhi ya kutosha. Maeneo mengi ya nchi, hususan vijijini kumekuwa na shida kubwa ya ardhi.Vigogo na wafanyabishara wamekuwa wakigawana ardhi kubwa, jambo linalowafanya wananchi masikini wakose maeneo ya kulima. Hili halikubaliki. Serikali ya Magufuli ilifanyie kazi suala hili kwa vitendo. Ndio alionyesha kulipinga wakati wa kampeni zake, ila kwakuwa ameshafanikiwa kuwa rais, ni wakati wa kulitatua. Utumike utaratibu mzuri wa kuipima ardhi na kufanya utafiti ni kwa kiasi gani ardhi imeporwa na watu wasiokuwa na nia njema kwa walalahoi. Tunajua si wote wameipora, ila pia wapo waliofanya hivyo. Tuwajue wanaomiliki ardhi kihalali na wale waliojimilikisha wenyewe.

Wapo watu wanaomiliki heka zaidi ya 120 na bado wanaingia kwenye vieneo vya walalahoi. Kesi nyingi za ardhi zinazoendeshwa vijijini zinaishia kwa masikini kuonekana wana makosa. Hili linasikitisha. Namna gani Dr Magufuli ataungwa mkono? Nadhani ili suala hilo lifanyiwe kazi kwa vitendo, ni wakati wa Wakuu wa Mikoa kujipanga kikamilifu. Kila Mkuu wa Mkoa asimamie kuundwa kwa Kamati ya Ardhi katika wilaya husika. Kamati ya Ardhi iwe na wajumbe mchanganyiko, akiwamo Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi. Kamati hii na Mwenyekiti, Katibu na wajumbe wake kadhaa. Kamati hii iwe na mamlaka ya kutembelea katika maeneo mbalimbali ya wilaya husika kuchunguza, kusikiliza kero za ardhi. Kamati hii pia iwe na mamlaka ya kutatua kero ndogo ndogo. Baada ya kukamilisha utendaji kazi wake, Kamati hii itawasilisha kwenye Kamati ya Ardhi ya Mkoa, ambayo hapana shaka Mwenyekiti wake anaweza kuwa Mkuu wa Mkoa husika, ambapo baadaye itawasilisha mezani kwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Rais. Utaratibu huu utumike katika kila wilaya na Mkoa.

Tukifanya hivi, tunaweza kunusuru muda na gharama za maisha kwa Watanzania. Tunashuhudia miji na majiji makubwa yakipokea wageni wengi wanaotoka vijijini kwao. Ujio wa watu hao hususan vijana unadai kuwa katika maeneo yao hakuna ajira, maisha magumu. Ni kweli wanaishi maisha magumu. Ikiwa unaishi vijijini na huna eneo la kulima, utaishi vipi? Vijana hao ambao wengi wao ni nguvu kazi ya Taifa, wanaingia katika miji na majiji ili kutafuta maisha yao. Acheni waje tu. Kama hatupendi waje mijini, basi wapatiwe ardhi, walime. Tunaambiwa kwamba kilimo ndio uti wa mgongo. Kwa Tanzania ya leo, kilimo hakiwezi kuwa uti wa mgongo. Watalimaje? Hakuna ardhi, pembejeo. Wanaolima wanatumia nguvu kubwa na mavuno ni hafifu. Wataalam wa kilimo nao wapo ‘busy’ na maisha yao. Hatuwezi kufika. Tunapaswa kujitazama upya. Wapi tunapotoka na wapi tunataka kwenda kama nchi.

Tuwe na mipango imara kama tunataka maendeleo. Natambua, tukiwekeza kwenye kilimo, walau tutakuza uchumi wetu. Kila mtu atakuwa na sehemu ya kumuingizia kipato katika maisha yake. Si kama ilivyokuwa sasa. Mtu yupo kijijini, ila hana eneo la kulima.
Katika kuliangalia suala la ardhi na migogoro yake, maeneo mengi imesababishwa na viongozi wa vijiji husika. Wameuza ardhi bila kuangalia athari wanazoweza kupata watoto wao miaka michache ijayo. Viongozi hao wameshindwa pia kutambua sera ya ardhi inayoelekeza namna gani wanapaswa kutoa ardhi kuanzia heka 50 kwa mtu binafsi, kampuni au shirika. Hali hiyo imewafanya wauze ardhi yao kama njugu. Na wilaya zinazoongoza kwa matatizo haya ni Handeni na Kilindi, mkoani Tanga. Katika kila Kata za wilayani Handeni wananchi wanalia. Mtu mmoja ana heka nyingi zilizokaa tu. Miaka 20 ijayo, wananchi wa Handeni wataanza kukodisha ardhi kwa walioingia kwa wingi na kuinunua ardhi yao kwa fedha za chai. Mapungufu haya na mengine yamulikwe. Tufanye tathimini ya ardhi yetu. Ipigwe marufuku kuuza ardhi.

Serikali Kuu itoe amri kurudisha ardhi inayomilikiwa na watu wachache. Hii inawezekana. Mtu anayemiliki heka nyingi, basi aachiwe heka 50 na zinazoongezeka wapewe wananchi wasiokuwa na mashamba ili walime. Na wananchi hao watakaopewa ardhi hiyo, wapigwe marufuku kuiuza kwa watu wengine. Na mtu anayemiliki heka 50 na asiyezilima, abakiziwe heka 10 hadi 20. Utaratibu huo utakuwa mchungu kwa wachache lakini ni mtamu kwa wengi. Itakuwa ni funzo na mpango wenye tija kwa wananchi.
Binafsi naamini hili linawezekana. Ni kuamua na kufanyia kazi kwa vitendo. Utendaji mwema na ushirikiano kwa watendaji wa serikali na wananchi husika jambo hilo linawezekana. Huo ndio ukweli wa mambo.

Kama nilivyosema hapo juu, wasimamizi wa kwanza wa suala hilo la kuokoa ardhi iwe kwa Wakuu wa Mikoa na wilaya. Kwa mfano, Mkuu wa Wilaya ndio Mwenyekiti wa Ulinzi wa Usalama wa wilaya husika. Hivyo anapoingia kwenye harakati hizo ni jambo la busara. Najua ni kiasi gani suala la migogoro ya ardhi ni zito, ila hatuna jinsi. Wengi wanaomiliki ardhi kubwa si watu wadogo. Wana ukwasi. Na pengine wana mtandao mpana. Hata hivyo sidhani kama nguvu za mabeberu hao wa ardhi zinaweza kufanikiwa, maana suala hilo litaendeshwa na serikali. Ilikuwa kwenye ahadi za mgombea urais. Na hata baada ya kushinda, ameendelea kulizungumzia jambo hilo kwa nguvu kama kawaida yake. Aungwe mkono. Apewe ushirikiano wa kutosha. Kila mtu afanye kazi yake kwa vitendo ili miaka miwili ijayo, kila mtu awe na eneo la kulima kwa ajili ya kumuingizia kipato.

Kwanza wapate ardhi ya kulima, kisha wapewe elimu ya namna bora ya kulima kwa mafanikio badala ya kuendelea kulima kwa mazoea, jambo linalowafanya washindwe kupiga hatua miaka nenda rudi. Asichekewe wala kuonewa huruma yoyote anayemiliki ardhi kubwa wakati wananchi wanakosa maeneo ya kulima. Wawekezaji walioyageuza mapori ni vichaka vya kufuga nyani wamulikwe. Wapo waliokwenda vijijini na kununua heka nyingi za ardhi kwa gia ya kulima, kumbe ni kukata mkaa. Baadaye wakapata kibali cha kusafisha shamba, wakakata mkaa, wakapakia kwenye magari na kwenda kuuza. Shamba likaachwa. Serikali ianze na hao kwanza. 

Kwa bahati nzuri, wananchi wana Imani kubwa na serikali ya Dr Magufuli. Huu ndio wakati mzuri wa kuwafanya wananchi wajivunie na serikali yao kwa kusimamia kila lenye tija kwao. Kinyume cha hapo hakutakuwa na jipya. Dhihaki zitaendelea. Serikali itaonekana ya kujuana, kuchezeana kiasi cha kuwafanya wananchi washindwe kusonga mbele, huku utendaji kazi wote wa Dr Magufuli ukionekana si lolote wala si chochote.
0712053949

No comments:

Post a Comment