Pages

Pages

Thursday, October 22, 2015

Dkt John Magufuli mgombea Urais wa CCM sasa kuomba kura kwa njia ya simu

CHAMA cha Mapinduzi CCM kimezidi kujitengenezea mazingira mazuri ya ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka unaotarajiwa kufanyika Jumapili, Oktoba 25 baada ya kubuni mkakati mpya wa ushindi ambapo mgombea wa nafasi ya urais Dk. John Magufuli kuwapigia simu wananchi akiomba wampigie kura. 

Ujumbe huo unaokwenda kwa watumiaji wa simu za mitandao mbalimbali humfikia mmiliki wa simu kupitia namba +255622333333 na mara baada ya simu hiyo kupokelewa husikika sauti ya Dk. Magufuli akiwaomba watanzania kumpigia kura ili aweze kushinda na hatimaye aweze kuwa rais. Hatua hiyo ni moja ya njia muhimu za kuwafikia watanzania wote bila kujali itikadi zao na zaidi wale baadhi ya wananchi waliokosa fursa ya kusikia mambo yapi yatafanywa na mgombea huyo endapo kama atafanikiwa kuwa rais. Ukiacha utaratibu wa kampeni za moja kwa moja majukwaani, mabango, mahojiano katika televisheni, hatua ya Chama cha Mapinduzi kubuni njia ya kutuma ujumbe huo kwa wananchi utawasaidia kujiongezea kura katika uchaguzi huo unaonekana kuwa na ushindani mkubwa.

Pengine hili ndio bao la mkono lililowahi kusemwa kipindi cha nyuma na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Nape Nnauye kutokana na hatua hiyo kuwa muhimu hususani wakati huu ambao watanzania wengi wanamiliki simu za mkononi. Kutokana na hatua hiyo ina maana kuwa watanzania wengi wataweza kumsikia mgombea huyo akiwaomba kura mbali na maeneo mengine waliyozoea kusikia sauti yake ikiomba kumchagua katika uchaguzi huo unalenga kumpata rais wa awamu ya tano wa taifa hili. Chama cha Mapinduzi CCM kimemsimamisha Waziri huyo wa Ujenzi kushika kijiti kinachotarajiwa kuachwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete siku chache zijazo.

No comments:

Post a Comment