Pages

Pages

Tuesday, October 20, 2015

Dkt John Magufuli aendelea kufunika katika kampeni zake, jana atua mkoani Geita na kufanya mikutano katika wilaya mbalimbali mkoani humo

MGOMBEA urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema kutokana na kukubalika kwake katika mikoa yote aliyokwenda kufanya mikutano ya kampeni, ana uhakika wa kupata ushindi wa tsunami katika uchaguzi wa mwaka huu. Amesema katika mikoa yote aliyokwenda kufanya kampeni, wananchi wamemkubali na kumuhakikishia kumpigia kura nyingi ili aweze kuwa Rais wa awamu ya tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. PICHA ZOTE NA CATHBERT KAJUNA.

"Ushindi wa mwaka huu ni wa tsunami. Kote nilikokwenda wananchi wanasema ni Magufuli. Wapinzani wataisoma namba. Wao ni wasindikizaji tu," alisema Dk. Magufuli jana, alipohutubia mkutano wa kampeni, uliofanyika kijiji cha Nkome, Jimbo la Geita Vijijini, mkoani Geita. Aidha, akihutubia mkutano uliofanyika Nyehunge, Jimbo la Buchosa, Wilaya ya Sengerema mkoani Geita, mgombea huyo aliwataka Watanzania wasikubali kuuziwa mbuzi kwenye gunia kwa kisingizio cha kuuchukia umasikini.
Dk. Magufuli akiongea Mgombea ubunge wa Nkome.
Ujumbe.
Msafara wa Dk. Magufuli ukiwa umesimamishwa.
Alisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakijinadi kuwa wanauchukia umasikini, lakini ndio walioifilisi nchi na kuifikisha mahali ilipo na kuwafanya wananchi wake wawe masikini. Amesema wanasiasa wa aina hiyo hawapaswi kupewa uongozi wa nchi kwa sababu hawana uwezo wa kuiletea nchi maendeleo zaidi ya kutaka kujinufaisha wao binafsi. Akihutubia mkutano huo huku manyunyu ya mvua yakinyesha, Dk. Magufuli alisema wapo wanasiasa wanaodai kuwa serikali haijafanya lolote kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita, wakati baadhi yao walikuwa mawaziri wakuu wa serikali mbili tofauti na pia washauri wakuu wa rais. "Hawa ndio waliotucheleweshea maendeleo. Wanadai kwamba serikali haijafanya lolote, wakati waliwahi kuwa viongozi wa serikali. Na wanadai kwamba wanauchukia umasikini," alisema mgombea huyo na kuzielezea kauli hizo kuwa ni sawa na kuwauzia wananchi mbuzi kwenye gunia.
Alisema binafsi licha ya kuwa waziri kwa miaka 20, hakuwahi kupokea rushwa ama kutaka kutajirika, japokuwa wizara yake ilikuwa ikihusika kutia saini mikataba yenye fedha nyingi kuliko wizara zingine. Alisema umasikini wa Watanzania na kiu ya kuwaletea maendeleo ni miongoni mwa mambo yaliyomshawishi na kumfanya ajitose kuwania urais wa Tanzania kwa lengo la kuwaletea maendeleo. Dk. Magufuli alisema baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wamekuwa wakijinadi kuwa watatoa kila kitu bure kwa wananchi, lakini hawaelezi watatumia njia zipi kuzifanya huduma hizo ziwe za bure.
Aliwataka wananchi iwapo watapewa pesa na wapinzani siku ya kupiga kura, Jumapili ijayo, wazipokee na kuzila, lakini kura zao wazielekeze kwa wagombea wote wa CCM. "Msichague watu wasiokuwa na uchungu na wananchi. Mabadiliko ya kweli ni kufanyakazi na kuwasaidia Watanzania walio masikini,"alisema mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi hao, ambao hawakujali manyunyu ya mvua yaliyokuwa yakiwanyeshea. Alisema ishara zinazotolewa na wapinzani za kuzungusha mikono hewani kama watu wanaoendesha baiskeli au pikipiki, haziwezi kuwaletea mabadiliko. Alisema shida ya Watanzania sio vyama vya siasa, bali wanataka maendeleo.
Aidha, Dk. Magufuli alisema uamuzi wake wa kufanya kampeni kwa kutumia barabara umelenga kufika katika maeneo mengi nchini na pia kushuhudia kero zinazowakabili wananchi ili aweze kuzitafutia ufumbuzi. Aliwaahidi wananchi wa Bushosa kuwa atakapoapishwa na kuwa rais wa Tanzania, atatoa kipaumbele kwa ujenzi wa barabara ya Kamanga hadi Sengerema kwa kiwango cha lami. Hata hivyo, aliwataka wavuvi katika jimbo hilo na mkoa wa Geita, kujiepusha na uvuvi wa kutumia sumu aina ya thiodan kwa vile unasababisha kutoweka kwa samaki kwenye Ziwa Victoria.
Alisema samaki mmoja aina ya sangara anakuwa na mayai zaidi ya milioni moja na nusu, hivyo anapouawa kwa sumu ni sawa na kupoteza idadi hiyo ya samaki. Aliwataka wavuvi hao kutunza mazalia ya samaki kwa kuwa iwapo wataendelea kuwaua kwa sumu, watakosa kazi ya kufanya siku zijazo na hivyo kudumaza maisha yao. "Japokuwa nimekuja kuwaomba kura, lakini lazima niwaambie ukweli. Tumepewa ziwa hili na Mungu, lazima tulitumie vizuri," alisema.
Kabla ya kufika Bushosa, msafara wa Dk. Magufuli ulisimamishwa katika vitongoji vinane, kutokana na wananchi kuwa na kiu ya kumuona na kusikiliza sera zake. Vitongoji hivyo ni Kamanga-Kivukoni, ambako msafara wake ulianza saa 3.30 asubuhi. Msafara wa Dk. Magufuli pia ulisimamishwa katika vitongoji vya Nyamatongo, Katungulu, Kasenyi, Nyamazugo, Ruchili, Bukokwa na Kalebezo. Akiwa Kalebezo, Dk. Magufuli alisema amefurahi kufika tena katika kitongoji hicho kwa sababu ndiko alikobatizwa katika Kanisa la Kalebezo.

No comments:

Post a Comment